2018-01-29 07:47:00

Mshikamano wa Papa Francisko na watu wa Ukraine katika sala na sadaka


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 28 Januari 2018 majira ya jioni, ametembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Sofia lililoko mjini Roma, linalowahudumia waamini wa Jumuiya ya Wagiriki Wakatoliki kutoka nchini Ukraine, kielelezo na ushuhuda makini wa upendo na mshikamano wa Baba Mtakatifu Francisko na familia ya Mungu inayoteseka sana nchini Ukraine. Tukio hili limehudhuriwa na waamini wa Jumuiya hii kutoka ndani na nje ya Roma, ili kusali kwa ajili ya kuombea amani, utulivu na usalama huko nchini Ukraine, ambayo kwa sasa inaonekana kusahauliwa na wengi, licha ya juhudi za Jumuiya ya Kimataifa na Kidiplomasia kutaka kupata suluhu ya kudumu juu ya mgogoro huu!

Baba Mtakatifu Francisko amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba, Kanisa linawasaidia wananchi wa Ukraine kupambana na hali yao kwa hali na mali. Jumuiya ya Wagiriki Wakatoliki kutoka nchini Ukraine wanaoishi mjini Roma, inakadiriwa kuwa ni zaidi ya waamini elfu kumi na nne wanaohudumiwa katika Parokia kuu tatu zinazojihusisha na huduma ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji kutoka Ukraine. Baba Mtakatifu kabla ya kuingia na kutembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Sofia, alisimama mlangoni na kusali kwa ajili ya kuombea amani nchini Ukraine. Amewashukuru waamini kwa kuendelea kuwa waaminifu kwa Mwenyezi Mungu na Khalifa wa Mtakatifu Petro, kwa gharama kubwa ya maisha yao!

Baba Mtakatifu katika hotuba yake, amewakumbuka kwa namna ya pekee, viongozi wakuu watatu ambao wameandika historia ya maisha na utume wa Jumuiya ya Wagiriki Wakatoliki kutoka nchini Ukraine, Umuhimu wa Parokia hai kama mahali mubashara pa kukutana na Kristo Yesu Mfufuka pamoja na kutambua dhamana na mchango wa wanawake wakatoliki katika maisha na utume wa Kanisa bila kusahau madhara ya vita huko nchini Ukraine. Baba Mtakatifu anakaza kusema, upendo wa Mungu umefunuliwa kwa namna ya pekee kabisa na Kardinali Slipyj, aliyezaliwa miaka 125 iliyopita, ndiye muasisi na mjenzi wa Kanisa kuu la Mtakatifu Sofia, mjini Roma, kielelezo cha unabii wa uhuru wa kuabudu, wakati ambapo, uhuru huo ulikuwa umebanwa sana kwa wakati ule. Lakini kwa njia ya mateso na mahangaiko makubwa, Mwenyezi Mungu aliweza kujenga Hekalu kubwa, zuri na takatifu ambalo ni waamini wenyewe kutoka Ukraine. 

Baba Mtakatifu amemkumbuka pia Askofu Chmil, aliyefariki dunia takribani miaka 40 iliyopita na kuzikwa ndani ya Kanisa kuu la Mtakatifu Sofia, mjini Roma. Baba Mtakatifu katika maisha yake ya ujana, alibahatika kutumikia Ibada ya Misa Takatifu iliyokuwa inaongozwa na Askofu Chmil. Ndiye aliyemfunza namna ya kuhudumia Altareni, kusoma Kigiriki, kujibu na kushiriki kikamilifu katika Ibada ya Misa Takatifu, kiasi cha kufurahia kushiriki katika Liturujia iliyokuwa inaadhimishwa ndani ya Kanisa hili. Askofu Chmil ni shuhuda wa imani iliyojaribiwa sana katika Karne ya 20! Ni shuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake aliyepandikiza mbegu ya maisha kwa Njia ya Msalaba kwa kutambua kwamba, ushindi wa Mkristo unafumbatwa katika Fumbo la Msalaba, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu, chemchemi ya matumaini mapya.

Baba Mtakatifu amemkumbuka pia Kardinali Husar, ambaye alitangazwa na kusimikwa pamoja naye, kielelezo cha mkuu wa Kanisa la Ukraine, Baba na Kaka ya waamini wengi. Alikuwa ni kiongozi mwema, aliyeokesha na kusali hadi dakika ya mwisho wa maisha yake hapa duniani! Alikuwa kipofu, lakini, macho yake ya imani, yalikuwa yanaangalia mbali zaidi! Viongozi hawa wamekuwa ni chemchemi ya matumaini, changamoto na mwaliko wa kuendelea kuwakumbuka na kuwaombea, kwani wamekuwa ni waalimu wa Injili waliyoifundisha kwa njia ya ushuhuda wa maisha!

Baba Mtakatifu anasema, wanawake wamekuwa mstari wa mbele kuwarithisha watoto wao amana na utajiri wa imani kwa ujasiri, ari na moyo mkuu! Wakathubutu kuwabatiza watoto wao na kwama, hata leo hii, wanawake kutoka Ukraine bado ni moto wa kuotea mbali kutokana na mchango wao katika ustawi, maendeleo na mafao ya wakazi wengi wa Roma na Italia katika ujumla wake. Ni wanawake wa shoka, wanaojitaabisha kuwalea watoto, kurithisha imani katika familia lakini daima, wamekuwa ni akina mama jasiri wanaopaswa kushukuriwa na kupongezwa!

Sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa Jumuiya ya Wagiriki Wakatoliki kutoka nchini Ukraine inafumbatwa katika dhana ya Parokia hai, mahali pa kukutana mubashara na Kristo Yesu aliye hai. Hii ina maanisha kwamba, Kanisa ni mahali pa watu kukutana ili kuganga na kuponya upweke na kishawishi cha kutaka kujitenga na kujifungia katika ubinafsi. Jumuiya ya Kikristo, inakuwa ni mahali muafaka pa kushirikisha Injili ya furaha, magumu na majonzi katika maisha; matatizo, fursa na changamoto mbali mbali zinazomwandama mwanadamu! Hapa ni mahali ambapo Mwenyezi Mungu anawakirimia waja wake Injili ya matumaini inayopyaisha maisha yao yote! Hapa ni mahali pa kujipatia chakula cha hija ya maisha ya kila siku, ili kuonja faraja moyoni na hatimaye, kuganga na kuponya madonda ya ndani!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, yu hai na anakutana na waja wake ndani ya Kanisa, wanapoadhimisha Liturujia, Mafumbo ya Kanisa na wanaposikiliza na kulitafakari Neno la Mungu. Kila Jumuiya ya waamini ni harufu safi inayopamba maisha ya waamini na wala si makumbusho ya mambo ya kale! Ni alama ya uwepo wa Kanisa mahalia, kitovu cha maisha na utume wa Kanisa, mahali ambapo, waamini wanajipatia maisha mapya; ni mahali pa kushinda dhambi na ubaya wake; kifo na majonzi moyoni, ili kutunza upya wa moyo wa ujana. Ni mahali ambapo imani na maisha vinakutana na kubusiana, tayari kurithishwa kwa vijana wa kizazi kipya. Vijana wanapaswa kutambua kwamba, Kanisa ni chemchemi ya  maisha mapya na kwamba, ndani mwake yumo Mwenyezi Mungu na Kristo Yesu aliye hai!

Baba Mtakatifu Francisko amependa kukazia kwa namna ya pekee kabisa mchango na dhamana ya wanawake kutoka Ukraine katika mchakato mzima wa kutangaza na kushuhudia Injili ya huduma inayomwilishwa katika mchakato mzima wa kurithisha imani na kwamba, kazi yao hata kama inawapatia mshahara kidugu, waitambue kuwa ni utume wao na kwamba, wao ni rejea ya wazee na wagonjwa wengi wanaoshuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Baba Mtakatifu anasema, anatambua madhara ya vita kwa wananchi wengi wa Ukraine na kwamba, amependa kuwa kati yao ili kuwaonjesha mshikamano wake katika sala na adhimisho la Ekaristi Takatifu, ili kweli Bwana wa amani, aweze kunyamazisha milio ya silaha; wawe ni mashuhuda na vyombo vya matumaini, daima wakiwa na ujasiri wa kusonga mbele na kuanza upya.

Amewaambia kwamba, daima katika maisha na utume wake, amekutana na wananchi kutoka Ukraine kwa njia ya zawadi ya Picha ya Bikira Maria, Mama wa upendo ambayo ameitundika chumbani mwake kama ushuhuda endelevu wa urafiki na viongozi wa Kanisa kutoka Ukraine. Kati ya mambo aliyoyachukua kutoka Argentina anasema Baba Mtakatifu ni Picha ya Bikira Maria, Mama wa huruma na Breviari kwa ajili ya Sala ya Kanisa. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuondoka, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Sofia mjini Roma, amewashukuru waamini kwa udumifu wao katika imani, kiasi hata cha kuthubutu kuwarithisha watoto wao na kwamba, hii ndiyo zawadi kubwa wanayoweza kuwapatia watoto wao kama urithi. Amewaomba kuendelea kusali kwa ajili ya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.