Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Mahubiri

Mfalme Daudi hata katika fahari zake, alinyenyekeshwa kama mdhambi!

Mfalme Daudi hata katika fahari zake, alinyenyekeshwa akatubu na kumwongokea Mungu!

29/01/2018 16:04

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 29 Januari 2018 amesema, hakuna fadhila ya unyenyekevu bila mtu kunyenyekeshwa. Mfalme Daudi katika fahari yake yote na mafanikio makubwa aliyojipatia vitani, akasifiwa na kuimbiwa nyimbo za ushindi. Alikuwa ni kiongozi mwenye moyo mkuu ambaye hakupenda kulipiza kisasi kwani mwenyezi Mungu alikwisha mweka Mfalme Sauli mikononi mwake, lakini hakumtenda mabaya. Mfalme Daudi, alikuwa pia mtenda dhambi mkubwa, aliyempeleka Uria na kuuwawa kikatili kwa upanga na hata mtoto Bathsheba akauwawa. Lakini, Kanisa linamwona Daudi kama Mtakatifu wa Mungu, kwani baada ya kutambua kwamba, ni mdhambi, akatubu na kumwongokea Mungu.

Absalomu, alimwasi baba yake Daudi, lakini Daudi alijitaabisha zaidi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wake. Alitaka kuliokoa Hekalu ambalo lilikuwa ni alama na utambulisho wa uwepo wa Mungu kati ya watu wake. Alitaka kuhakikisha kwamba, Sanduku la Agano linalindwa kwa nguvu zote, lakini pamoja na changamoto zote, hizi, Daudi akatimua mbio, kwa unyenyekevu mkubwa, huku Shimeni akimtukana Daudi na kumtupia mawe, huku akimlaani. Kama alama ya unyenyekevu, Mfalme Daudi alitembea miguu peku! Ufalme wake ukawekwa chini ya ulinzi na usimamizi wa mtoto wake Absalomu aliyetoka viunoni mwake.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Daudi akajiaminisha kwa huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake. Daudi akapanda kwenda mlimani, ili kuyamimina maisha yake, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu alipopanda Mlimani Kalvari, hali inayoonesha unyenyekevu mkuu ulioshuhudiwa na Kristo Yesu katika Njia ya Msalaba. Baba Mtakatifu anakaza kusema, unyenyekevu hauna maana ya kutokumbana na patashika nguo kuchanika katika maisha, au kutembea huku umejiinamia kama “Kondoo” asiyekuwa na mchungaji, kwani huu si unyenyekevu unaomwezesha mwamini kuokoa roho yake. Hakuna unyenyekevu wa kweli bila kunyenyekeshwa, ili kufundishwa adabu upate kujenga moyo wa uvumilivu na matumaini kama ilivyokuwa kwa Mfalme Daudi aliyetambua mapungufu yake ya kibinadamu, akakimbilia huruma na upendo wa Mungu. 

Kristo Yesu, Mtakatifu wa Mungu, alionesha moyo wa upendo na mshikamano na binadamu mdhambi, akawa tayari kunyenyekeshwa chini ya Msalaba na kutukanwa kwa aibu katika Njia ya Msalaba. Yesu amekuwa ni sababu ya matumaini ya waamini wake kutokana na unyenyekevu aliouonesha na kuushuhudia katika maisha. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia fadhila ya unyenyekevu hata pale wanaponyenyekeshwa na kuupuzwa na watu. Waamini wawe na ujasiri wa kuomba fadhila hii kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

29/01/2018 16:04