2018-01-27 14:15:00

Vietnam na Vatican kuendelea kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia


Hivi karibuni, Monsinyo Antoine Camilleri, Katibu mkuu msaidizi wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican aliongoza ujumbe wa Vatican huko Vietnam kuanzia tarehe 16 - 20 Januari 2018 kama sehemu ya utekelezaji wa sera na mipango ya kikosi kazi kilichoundwa kunako mwaka 2009 baina ya nchi hizi mbili ili kuangalia mikakati ya kuboresha mahusiano kati ya Vatican na Vietnam kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa Vietnam. Hizi ni juhudi ambazo zimekuwa zikifanywa na Askofu mkuu Leopoldo Girelli, aliyekuwa Balozi wa Vatican nchini Vietnam kwa muda wa miaka saba iliyopita na tangu mwezi Oktoba, 2017 ameteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Balozi wa Vatican nchini Israeli na Palestina.

Monsinyo Antoine Camilleri na ujumbe wake wakiwa nchini Vietnam wamepata nafasi ya kukutana na viongozi wa Serikali chini ya Waziri Mkuu Nguyen Xuam Phuc. Wameonesha umuhimu wa Vatican kuteuwa Balozi mpya ili kuendeleza mchakato wa mahusiano ya kidiplomasia sanjari na kuhakikisha kwamba, majimbo ambayo bado yako wazi, yanajazwa kwa kupata Maaskofu wapya. Kuna baadhi ya majimbo ambayo yamebaki wazi kutokana na misiba, uhamisho na baadhi ya Maaskofu kufikia umri wa kung’atuka kutoka madarakani.

Baraza la Maaskofu Katoliki Vietnam linakaza kusema, dhamana na wajibu wa kuteuwa Maaskofu Katoliki ni wa Khalifa wa Mtakatifu Petro peke yake huku akisaidiana na viongozi wa waandamizi wa Kanisa na wala si suala linaloigusa Serikali ya Vietnam. Kumekuwepo na hali ya kutoelewana kati ya Kanisa na Serikali kuhusiana na uteuzi wa Maaskofu kwani hata Serikali inataka kuweka mkono wake, jambo ambalo linapingana na Kanuni, sheria na taratibu za Kanisa Katoliki. Ujumbe wa Vatican umeonesha nia ya Kanisa kutaka kuanzisha taasisi za elimu zinazoendeshwa na kusimamiwa na Mama Kanisa. Kwa sasa, Mashirika ya kitawa na kazi za kitume peke yake ndiyo yaliyopewa uhuru wa kuanzisha na kuendesha shule za awali. Kikosi kazi cha ushirikiano kati ya Serikali ya Vietnam na Vatican kilianzishwa kunako mwaka 2009, ili kuendeleza majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wengi wa Vietnam. Serikali ya Vietnam inalishauri Kanisa kuendelea kutoa majiundo makini na endelevu kwa waamini wake, ili waweze kuchangia katika sera na mikakati ya maendeleo endelevu ya binadamu mintarafu sheria na sera za nchi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.