Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Maisha Ya Kanisa Afrika

Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya atabaruku Kanisa la Parokia ya Nkuhungu

Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo kuu la Dodoma, Tanzania hivi karibuni ametabaruku Kanisa la Parokia ya Mt. Gemma Galgan, Nkuhungu na kutoa Sakramenti ya Kipaimara kwa waamini 310. - AFP

27/01/2018 13:53

Mama Kanisa kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara anakamilisha muungano wa wabatizwa na Kanisa, kwani Wakristo wanatajirishwa na nguvu ya pekee ya Roho Mtakatifu na hivi hulazimika kwa nguvu zaidi kuitangaza, kuishuhudia na kuitetea imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, si tu kwa maneno na matendo, lakini zaidi sana  kama mashuhuda wa kweli wa Kristo Yesu. Wakristo waliomarishwa kwa Roho Mtakatifu wanapokea Mapaji ya Roho Mtakatifu. Kwa njia ya Sakramenti ya Kipaimara hukuza na kuzamisha neema ya Sakramenti ya Ubatizo katika maisha ya waamini pamoja na kuwakirimia alama ya kiroho isiyofutika!

Hivi karibuni, Askofu mkuu Beatus Kinyaiya ametoa Sakramenti ya Kipaimara kwa waamini 310 wa Parokia ya Mtakatifu Gemma Galgan, Nkuhungu, Jimbo kuu la Dodoma sanjari na kutabaruku Kanisa la Parokia ya Nkuhungu ambalo limegharimu kiasi cha milioni 756.8 hadi kukamilika kwake sanjari na maboresho ya nyumba ya Mapadre na Ofisi ya Halmashauri walei. Kutabarukiwa kwa Kanisa hili kunawawezesha waamini kupata huduma zote za kiroho Parokiani hapo. Huu ni mwaliko kwa waamini kulilinda, kulitunza na kulidumisha, ili liweze kuwa ni chemchemi ya maadhimisho ya Mafumbo ya Mama Kanisa. Huduma za kichungaji zimesogezwa zaidi kwa waamini anasema Askofu mkuu Beatus Kinyaiya.

Kanisa hili sasa ni mahali patakatifu panapowawezesha waamini kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, Kuabudu, Kusali na Kutafakari Matendo ya Mungu katika maisha yao. Kigango cha Nkuhungu kilianzishwa kunako mwaka 1991 baada ya waamini kuanza kuongezeka na hivyo likaonekana hitaji la uwepo wa Kanisa la Parokia. Kunako mwaka 1992 huduma ya Ibada ya Misa Takatifu ilianza kutolewa kwenye Shule ya Msingi Nkuhungu chini ya usimamizi wa Parokia ya Mwenyeheri Maria–Theresa Ledochowska, Jimbo Katoliki la Dodoma. Kanisa la Parokia ya Mtakatifu Gemma, Nkuhungu, Jimbo kuu la Dodoma, lilitabarukiwa tarehe 7 Januari 2018 wakati maadhimisho ya Siku kuu ya Tokeo la Bwana.

Takwimu za sensa ya mwaka 2015 zinaonesha kwamba,  kuna familia za Wakristo Wakatoliki 2, 232, zenye waamini zaidi ya 10, 668. Padre Camilius Luambano, Paroko wa Parokia ya Mt. Gemma Galgan, Nkunhungu, Jimbo kuu la Dodoma, amewashukuru waamini waliojitoa bila kujibakiza kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa miundo mbinu ya Kanisa na kwamba, sasa wana Kanisa lenye hadhi, wanaloweza kulitumia kwa ajili ya maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Kama Parokia, kuna sera na mikakati ya shughuli za kichungaji ili kuhakikisha kwamba, huduma za maisha ya kiroho zinawafikia waamini kwa haraka zaidi!

Na Rodrick Minja, Jimbo kuu la Dodoma.

Na kuhaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Vatican News!

 

 

27/01/2018 13:53