2018-01-26 08:13:00

Papa Francisko: Tambueni: Utakatifu, Asili na Ukuu wa Yerusalemu!


Mji wa Yerusalemu  kimsingi ni kwa ajili ya mafao ya Jumuiya ya Kimataifa. Huu ni Mji Mtakatifu unaoheshimiwa na waamini wa dini ya Kiyahudi, Kikristo na Kiislam, kumbe, kwa waamini wa dini hizi, huu ni Mji mkuu wa maisha ya kiroho na kitovu cha majadiliano ya kidini, upatanisho na amani huko Mashariki ya Kati! Ili kuweza kupata ufumbuzi wa kudumu, kuna haja pia ya kuzingatia maoni ya viongozi wa kidini badala ya kujikita katika maamuzi ya kisiasa peke yake! Utakatifu, Asili na Tunu msingi za Mji wa Yerusalemu vinapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wengi.

Hivi karibuni, kumefanyika mkutano wa kimataifa ili kuunga mkono juhudi za viongozi wa kidini kutambua na kuthamini utakatifu, asili na tunu msingi za maisha ya kiroho zinazofumbatwa katika mji huu ambao kwa siku za hivi karibuni, umekuwa ni chanzo cha mpasuko wa Jumuiya ya Kimataifa. Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, alimwalika Baba Mtakatifu Francisko kushiriki katika mkutano huu wa kimataifa, lakini kutokana na sababu za kichungaji, kwani wakati huo, Baba Mtakatifu alikuwa kwenye hija yake ya kitume huko Amerika ya Kusini, aliamua kumwandikia ujumbe, akimtia shime, kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa amani ya kweli na kwamba, anaendelea kusali ili kuwaombea viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa na Kisiasa kujielekeza zaidi katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya: utulivu, amani na usalama ili viweze kutawala katika Nchi Takatifu.

Vatican kwa upande wake, inapenda kutoa changamoto kwa Israeli na Palestina kuanzisha tena mchakato wa majadiliano yanayolenga kudumisha amani na utulivu kati ya mataifa haya mawili; kwa kuheshimu mipaka iliyotengwa na Jumuiya ya Kimataifa sanjari na kuheshimu umaarufu wa Mji wa Yerusalemu, kwa kuzingatia utume, utakatifu na asili yake kama chemchemi ya amani na upatanisho kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi huko Mashariki ya Kati. Haya ndiyo matumaini ya waamini wa dini mbali mbali wanaoendelea kusali kwa ajili ya kuombea Mji wa Yerusalemu, ili uweze kudumisha umoja na udugu. Baba Mtakatifu aliwapatia wajumbe wote waliohudhurua mkutano huu kuanzia tarehe 17- 18 huko Al-Azhar, Misri, baraza zake za kitume.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.