2018-01-26 07:00:00

Manabii ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu!


Moja ya jukumu tunalopewa na Mama Kanisa ni kutangaza na kushuhudia Neno la Mungu kwa watu wote. Huu ni wajibu wa kinabii ambao unatufanya kila mbatizwa kuwa chombo cha kuwatangazia watu wengine, waliokwisha kulisikia Neno na wale ambao bado hawajalisikia ukweli ambao wanafunuliwa na Mungu. Ni wajibu ambao unahitaji utulivu ili kulisikia neno lenyewe na utayari wa kutoka na kuwaambia waliokusudiwa ujumbe uliotumwa. Nabii anatumika kama sauti, kile anachokitangaza si kutoka kwake bali ni kutoka kwa Mungu anayemtuma. Neno la Mungu ambalo nabii hutumwa kulitangaza linanuia kutamalakisha uwezo na Mungu katika jamii ya mwanadamu na hivyo kuwezesha yote kufanyika kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Dominika ya Nne ya Kipindi cha Mwaka B wa Kanisa inatufafanulia dhana hii ya unabii. Katika somo la kwanza tunaona jinsi ambavyo manabii walivyochipuka katika jamii ya Waisraeli. Wana wa Israeli huko Horebu waliomba kuwa na nabii kusudi wasimsikilize Mungu moja kwa moja. Mwenyezi Mungu aliwajibu kwa kusema: “mimi nitawaondokeshea nabii miongoni mwa ndugu zao… nami nitatia maneno yangu kinywani mwake, naye atawaambia yote nitakayomwamuru”. Hapa tunaona mantiki ya kuwa na nabii katikati yetu. Yeye anakuwa ni mtu tunayeishi naye na tunafahamiana naye vizuri kabisa. Zaidi ya hayo anayafahamu vema mazingira yetu na changamoto zake. Kupitia kwake mwenyezi Mungu anafikisha ujumbe wake na akitegemea utafika katika namna iliyozoeleka na itakayoeleweka. Hivyo, tunaweza kuona dhana ya unabii ni mithili ya utamadunisho, ambapo makusudio ya Mungu yanafikishwa mahali mahsusi katika muktadha ulizoeleka na wote na kwa namna hiyo unategemewa kueleweka na kupokelewa vizuri.

Sehemu hiyo ya somo la kwanza inatufafanulia kuwa maudhui ya ujumbe wa unabii ni kutoka kwa Mungu mwenyewe. Neno la Mungu linasema: “nami nitatia maneno yangu kinywani mwake”. Kutokusikiliza ujumbe huo utatugharimu lakini pia kama nabii ataelezea maneno yake kwa ajili ya  manufaa yake mwenyewe naye pia ataadhibiwa. Ni msisitizo wa kuheshimu maelekezo ya ujumbe wa neno la Mungu. Hapa tunataadharishwa kuepuka vishawishi vya aina yoyote ambavyo vinaweza kutuhadaa na kulipa kisogo Neno la Mungu au wakati mwingine kutafuta njia za kulipindisha au kulichakachua. Pengine ni hamu ya kutaka kuendelea sifa za kidunia au kukuza jina lako au kudhulumu jirani yako na pindi Neno la Mungu linapokukumbusha wajibu wako unatoa mwitikio hasi. Hapo utakuta mmoja anashindwa kulitangaza kikamilifu kama nabii au anashindwa kulipokea na kulifanyia kazi neno la nabii.

Kristo ambaye ndiye Neno lenyewe la Mungu anaifunua nguvu ya Neno la Mungu. Yeye Neno anayemwilika anaonekana moja kwa moja kwa matendo yake na uwepo wake unawafanya hadhira yake kuuona mkono wa Mungu. Watu “walimshangaa sana kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa anafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi”. Unabii wake unadhihirika katika Nafsi yake na matendo yake hayawi ya kinafki kama ya waandishi na wakuu wa dini wa wakati wake. Mafarisayo na waandishi walijikinai kutoa ujumbe wa neno la Mungu ili hali wao wenyewe hawakuwa wanautimiza. Unabii wao ulikuwa si kulifunua neno la Mungu bali kujitukuza wao wenyewe. Neno la Kristo ni ukweli kwa sababu yeye mwenyewe ndiyo  huo kweli yenyewe. Yeye anaufunua uwezo wa Mungu na hivyo anakuwa ni mwiba kwa ibilisi na mawakala wake. Ujio wake kati yetu unafukuza giza la dhambi na mauti.

Katika Ubatizo wetu tunapokea wajibu wa kinabii. Kwa Sakramenti hii tunafanywa kuwa wana warithi wa Mungu na kuwa ndugu zake Kristo. Kwa maneno mengine uweza wa Kristo unadhihirika ndani mwetu. Hivyo, uwepo wa wakristo duniani unapaswa kuwa ni mwiba kwa uovu wa ulimwengu huu. Uovu unapoendelea kutamalaki ni mashitaka kwetu kwamba tumeshindwa kuwa neno la Mungu na uwepo wetu hauzitetemeshi nguvu za mwovu. Hii inatokea pale tunapoisahau hadhi yetu na kujisawazisha na ulimwengu huu. Daima tutambue kwamba, hadhi yetu ya kikristo inapaswa kuhuishwa mara kwa mara kwa muunganiko wa kudumu na Mungu. Maisha yetu ya kiroho ndiyo nyenzo pekee ya kuufanya hai uwepo wa Kristo ndani mwetu na hivyo kutufanya kuwa vyombo vya kulieneza neno la Mungu na tishio kwa uwepo wa nguvu za giza.

Mtume Paulo anatuwekea mazingira mbalimbali ya miito yetu ambayo kila mmoja anapaswa kuicheza vyema nafasi yake kwa ajili ya kutekeleza kikamilifu kazi ya kinabii. Mmoja katika maisha ya ndoa anakuwa nabii pale tu anapotimiza wajibu wake kama anavyotegemewa ndani ya maisha ya wito wa ndoa. Kwao wote msisitizo wa kufanya yote kikamilifu kwa ajili ya furaha ya kweli ya mwenzi wake. Kwa upande wao wanaojiweka katika maisha ya wakfu wanakumbushwa kutekeleza kwa ajili ya Bwana. Paulo anahitimisha kwa kusema: “Nasema hayo niwafaidie; si kwamba niwategee tanzi, bali kwa ajili ya vile vipendezavyo, tena mpate kumhudumia Bwana pasipo kuvutwa na mambo mengine”. Ni wito ambao unaturudisha katika wazo moja tunalotafakari leo hii kwamba: yote yanapaswa kufanyika kwa ajili ya kudhihirisha ukuu wa Mungu. Kristo anatufunulia ukuu na utukufu wa Mungu katika Nafsi yake. Sisi tulio wajumbe wake tunaalikwa kutimiza nyajibu zetu mbalimbali kiaminifu ili kazi zetu na maisha yetu yawafikishie wengine ujumbe wa Mungu. Tukumbuke kwamba, Neno lake halirudi bure bila kuzaa matunda. Kulipokea ni baraka na fanaka kwa mwanadamu na kulipinga ni chanzo cha kuanguka na mauti.

Mimi ni Padre Joseph Peter Mosha

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.