2018-01-26 12:28:00

Kardinali Zenari: Sikilizeni kilio cha Siria na kukipatia majibu!


Kardinali Mario Zenari, Balozi wa Vatican nchini Siria anasema, bado kuna kilio cha damu kinachoendelea kusikika nchini Siria; watu wasiokuwa na hatia bado wanaendelea kuteseka kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara na kwamba, kuna watoto ambao kwa sasa madhara ya vita yamekuwa kama sehemu ya vinasaba vya maisha yao ya kila siku! Kuna haja kwa viongozi wenye dhamana ya kulinda na kudumisha, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kusikiliza na kujibu kilio cha mahangaiko ya wananchi wa Siria. Katika kipindi cha miaka saba, wananchi wasiokuwa na hatia wameteseka na kunyanyasika sana, baadhi yao wamelazimika kuyakimbia makazi yao; nyumba za ibada, huduma ya afya na shule zimeharibiwa sana! Kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujipanga vyema, ili kuhakikisha kwamba, amani na utulivu vinarejea tena nchini Siria.

Serikali ya Siria hivi karibuni imekanusha kwama, inatumia silaha za sumu katika mashambulizi dhidi ya vikosi vya waasi nchini humo. Hivi karibuni, nchi 24, ambazo wawakilishi wake wamekutanika huko Paris, zimeamua kulivalia njuga sula ya Siria kutumia silaha zenye sumu, ili kuhakikisha kwamba, vikwazo vilivyowekwa vinafanya kazi! Wanajeshi kadhaa wameuwawa, wengine wametekwa nyara na kuteswa sana, hali ambayo inaonesha kwamba, kuna uvunjifu mkubwa wa haki msingi za binadamu huko Mashariki ya Kati.

Kardinali Mario Zenari anasema, familia ya Mungu nchini Siria ilitegemea kuona amani kwa Mwaka 2018, lakini bado inaendelea kutembea katika giza na ombwe la wasi wasi wa mashambulizi ya kushtukiza. Wazazi bado wanahofu na wasi wasi wa kuwapeleka watoto wao shuleni kwani hawana uhakika kwamba, watoto wao wataweza kurejea salama salimini. Ni matumaini ya wapenda amani duniani kwamba, mazungumzo ya amani nchini Siria yataanza tena kuchukua mkondo wake, mwishoni mwa mwezi Januari, 2018, ili suluhu ya kisiasa iweze kupatikana huko Siria kwani vita imeendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa hawana budi kusikiliza kilio cha watoto wa Siria wanaotaka amani ya kudumu; kusikiliza kilio cha wazazi na walezi wanaotaka kuwajengea watoto wao leo na kesho iliyo bora zaidi kwa njia ya elimu. Kuna watoto wanatesema kwa baa la njaa na utapiamlo wa kutisha kutokana na vita ambayo imedumu kwa takribani miaka saba! Watu wanakufa kutokana na baridi na utupu! Kilio cha mahangaiko ya wananchi wa Siria hakiwezi kuendelea bila kusikilizwa na Jumuiya ya Kimataifa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.