2018-01-25 09:12:00

Frt. Richard Joseph Masanja kupewa Daraja la Ushemasi, Roma!


Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo Yesu. Sakramenti ya Daraja huwapa chapa isiyoweza kufutwa na hufananishwa na Kristo aliyejifanya Shemasi, yaani mtumishi wa watu. Dhamana na wajibu wa Shemasi katika maisha na utume wa Kanisa ni kuwa shuhuda na chombo cha huduma na huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Shemasi ni mhudumu wa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa. Mashemasi wanawekwa wakfu kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu. Ni mashuhuda wa utakatifu wa watu wa Mungu unaopata chimbuko lake katika maisha ya Sala za Kanisa, Tafakari ya Neno la Mungu na Nidhamu katika maisha ya Utii, Useja na Ufukara kama kielelezo makini cha ufuasi wa Kristo kwa njia ya maisha ya wakfu!

Mimi naitwa Frt.  Richard Joseph Masanja wa Shirika la Mapendo (Institute of Charity I.C au Rosminians).  Ni mzaliwa wa Kigango cha Igoko, Parokia ya Ndala Jimbo Kuu Katoliki la Tabora, nchini Tanzania. Ni mtoto wa pili katika familia ya watoto sita. Msichana mmoja na wavulana watano. Nilisoma katika Shule ya Msingi Igoko baadaye nikaenda Shule ya Sekondari Kazima iliyopo katika Manispaa ya Tabora. Baada ya masomo ya kidato cha nne nilikwenda kufanya kozi ya ualimu kwa ngazi ya Astashahda katika Chuo cha Ualimu Mpwapwa na kidato cha Sita. Baadaye nilijiunga na Chuo cha Ualimu Tabora kwa ngazi ya Stashahda ya Elimu katika masomo ya Jiografia na Kiswahili. Baada ya kufanya kazi kidogo nilijiunga na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino tawi la Mwanza (SAUT) kwa ngazi ya Shahada katika masomo ya Jiografia na Kiswahili.

Nikiwa Chuoni Mwanza nilivutiwa sana na wahadhiri wangu hasa Mapadre wa Shirika la Yesu (Jesuit Fathers) walivyokuwa wana Niliipenda sana kazi ya ualimu tangu nikiwa mtoto mdogo. Kwa hiyo nilipokutana na Mapadre hawa hamasa yangu iliongezeka zaidi ya kutaka kuwa Padre na Mhadhiri wa Chuo Kikuu.  Hivyo nikiwa SAUT, nikaamua kuulizia taratibu za mimi kujiunga na Shirika hilo la Yesu (Jesuits Fathers). Nilipewa kitabu kidogo kilichokuwa na anwani mbalimbali za wakurugenzi wa miito katika mashirika mbalimbali ya kitawa na kazi za kitume. Mojawapo lilikuwa ni Shirika la Mapendo (Rosminians) na Shirika la Yesu(Jesuit Fathers). Niliandika barua mbili moja kwa Rosminians na nyingine kwa Shirika la Yesu. Nilipata barua kutoka Shirika la Mapendo wakati niko mwaka wa pili naelekea kuingia mwaka wa tatu, Chuo Kikuu cha SAUT.

Baada ya kupata barua hiyo sikuwa na mpango tena wa kujiunga na Shirika la Yesu. Hivyo nilipomaliza masomo yangu ya Shahada mwaka 2010 nikawasiliana na Mkurugenzi wa Miito wa Shirika la Mapendo na kuniambia kuwa nijiandae kuanza malezi ya awali. Niliwaeleza wazazi wangu wote wawili nia yangu ya kujiunga na maisha ya utawa. Namshukuru Mungu wazazi wote walikubali ombi langu kwa kauli moja. Na hiyo ndiyo ikawa mwanzo wa safari yangu ya wito katika Shirika hili la Mapendo. Nilianza taratibu za malezi ya awali kwa ngazi ya Upostulanti mwishoni mwa mwaka 2011 kwa miezi michache, kisha  mnamo mwaka 2012 nikapokelewa kuanza rasmi hatua ya Unovisi.

Unovisi ni kipindi cha miaka miwili. Hivyo nilimaliza na kufunga nadhiri zangu za kwanza mnamo mwaka 2014. Mara baada ya nadhiri za kwanza nilitumwa kuja Roma katika Chuo cha Kipapa cha Mtakatifu Beda (Pontifico Beda College) kilichopo karibu na Kanisa la Mtakatifu Paulo. Nilifunga nadhiri zangu za daima mwishoni mwa mwaka 2017. Kwa neema na uwezo wa Mwenyezi Mungu nategemea kupewa Daraja la Ushemasi wa Mpito, hapo tarehe 27 Januari 2018 majira ya 11: 00 Jioni kwa Saa za Ulaya, katika Kanisa la Mtakatifu Yohane lililopo katika nyumba yetu ya malezi ya Porta Latina hapa Roma pamoja na ndugu zangu katika Shirika Davide Busoni Cottini kutoka Italia na Benny Dennis kutoka India. Ibada hii ya Misa Takatifu itaongozwa na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya. Mungu ni mwema kila wakati. Amina.

Na Shemasi mtarajiwa Joseph Masanja wa Shirika la Mapendo.

Roma.








All the contents on this site are copyrighted ©.