2018-01-25 08:17:00

Bweni la Seminari ndogo ya St. Mary, Mbalizi, Mbeya lawaka moto!


Zaidi ya wanafunzi 52 wa Seminari ndogo ya St.Marys ya Mbalizi inayomilikiwa na kuendeshwa na Jimbo Katoliki la Mbeya, Tanzania wamenusurika kifo kutokana na ajali ya moto ulioteketeza bweni lote na vifaa vilivyomo katika bweni hilo la Mtakatifu James,  Jumapili, Januari,21,2018 majira ya mchana. Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishna wa Polisi,Mohamed Mpinga amethibitisha kutokea kwa tukio hilo katika Seminari ya St. Mary iliyopo Kijiji cha Mapinduzi, Kata ya Nsalala,Tarafa ya Usongwe,Wilaya ya Mbeya Vijijini mkoani mbeya. Kamanda Mpinga amefafanua kuwa bweni moja la St. James liliwaka moto na kuteketea lote pamoja na mali zote za wanafunzi wa Seminari zilizopo ndani ya bweni hilo, hakuna madhara yeyote yaliyojitokeza kwa binadamu, tathmini halisi ya thamani ya uharibifu bado haijafahamika na chanzo cha moto huo bado hakijajulikana na uchunguzi wa Jeshi la Polisi unaendelea. Aidha tukio jingine la aina yake lililojitokeza la ajabu ni kutoungua kwa vitabu vitakatifu vya Biblia na Rozali Takatifu zilizokuwa zimehifadhiwa katika masanduku ya bati ya wanafunzi licha ya kukuta vitu vingine vyote vikiwemo vitabu, madaftari, magodolo, vitanda, mashuka, nguo, mabati na jengo zima kuteketea kwa moto.

Padre Edwin Mwimba, Gombera wa Seminari hiyo amesema kuwa tukio hilo limetokea siku ya jumapili mara baada wanafunzi kutoka katika misaa majira ya saa 5 asubuhi na kuendelea na msasomo darasani wakashtukia kuona moshi ukitokea katika bweni hilo na bahati nzuri hakukuwa na mwanafunzi yeyote aliyekuwepo ndani ya bweni hilo na wote wapo salama. Padre Mwimba amesema bado haijafamika kiwango cha athari zilizojitokeza kutokana na ajali hiyo ambayo pia haijafahamika chanzo licha ya kila kitu kilichokuwepo ndani ya bweni hilo kuteketea kabisa na kufanikiwa kuvikuta vitabu vitakatifu vya Biblia vya wanafunzi pamoja na rozali ambavyo havikupata athari yeyote ya kuungua maandishi.

"Kwa kweli tumekumbana na changamoto hiyo katika Bweni la St.James baada ya wanafunzi kutoka katika misa na baada ya kuona moshi ukifuka walipiga kelele na hivyo baadhi ya majirani na wazazi waliokuwepo jirani walifika tukasaidiana kuuzima moto huku tukijaribu kupiga nambari za simu za kikosi cha zimamoto ambazo hazikuwa na majibu hadi tulipowasiliana na Padre aliyepo jimboni alifika kutoa taarifa katika Ofisi za Kikosi cha Zimamoto na hatimaye, walifika na kufanikiwa kuuzima ingawa hakuna kitu tulichookoa," alisema.

Gombera huyo alisema bweni hilo ambalo lilikuwa linahifadhi wanafunzi awali wa kidato cha kwanza limeteketea lote ingawa wameweza kuwahifadhi katika majengo mengine yaliyokuwepo wazi na wanaendelea na masomo kama kawaida. "Kwa ujumla kutakuwepo na uhitaji mkubwa wa mavazi, magodoro, vitanda, vitabu, madaftari na mavazi ya wanafunzi kwani wamebakiwa na mavazi waliyokuwa wamevaa na hiyo ndiyo changamoto kubwa,"amefafanua zaidi. Hadi sasa bado haijafamika chanzo cha ajali hiyo licha ya kuwepo kwa taarifa zisizo rasmi zinazodai hitilafu ya umeme iliyosababishwa kwa kukatika na kuwashwa inaweza ikawa ndiyo sababu ya chanzo cha ajali hiyo.

Na Thompson Mpanji,Mbeya,Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.