Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Yesu alifundisha kama mtu mwenye amri, bila kupepesa pepesa macho!

Kristo Yesu katika maisha na utume wake alifundisha kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko.

24/01/2018 14:32

Huyu ni nani? Kuanzia jumapili hii na nyingine 12 zifuatazo, Neno la Mungu litajikita katika swali hili – huyu ni nani?. Jibu la swali hili tutalipata katika jumapili ya 24 ambapo injili ya Marko inatoa jibu kwa swali hili. Ni katika ufunuo wa yule askari wa kirumi tunapata jibu – Mk. 15:39 – akida aliyesimama mbele yake, alipoona jinsi alivyokata roho alisema, hakika, huyu alikuwa Mwana wa Mungu.  Katika injili ya leo tunaona Yesu akiingia katika Sinagogi. Kila sabato walikuwa wanapata mafundisho, lakini leo fundisho lake ni tofauti – aliwafundisha kama mtu mwenye mamlaka – Mk. 1:22 – maana yake nini kufundisha kwa mamlaka? Tukilinganisha mafundisho ya Yesu na Walimu wa Sheria tunaona tofauti kuu tatu.

Tofauti kubwa ya kwanza ipo katika chanzo cha fundisho lenyewe, yaani fundisho linatoka wapi.  Fundisho la Yesu lilitoka moyoni na si kichwani au katika hali ya kufikirika tu! Lina mwelekeo wa roho mpya na si sheria tu.  Ni changamoto ya kuwa tayari kuanza upya. Mafundisho ya Yesu yamejaa uhakika kwa vile anajua anaongea ukweli wenye uzima. Angalia Yoh. 3:11 – amin, amin, nakuambia, twasema tunayoyajua, tunashuhudia tuliyoyaona, lakini hampokei ushuhuda wetu. Mafundisho yake ni ushuhuda wa uhusiano wake na Mungu. Walimu wa sheria, chanzo cha mafundisho yao ni sheria.

Tofauti kubwa ya pili kati ya mfundisho ya Yesu na yale ya walimu wa sheria ipo katika maana ya fundisho lenyewe.  Yesu anaangalia thamani ya sheria na maana yake.  Waandishi wa sheria wanakazia ufafanuzi wa maneno mfano kuhusu sabato lini sabato inaanza na lini inaisha na kazi ipi ya kufanya na ipi siyo.  Yesu anaelezea mpango kazi wa Mungu. Maana mpya ya sabato ni kujiacha kwa ajili ya Mungu ili kufanya kazi ya Mungu – Yoh. 5:17 – Yesu akasema, Baba yangu anaendelea na kazi yake, nami ninafanya vivyo hivyo. Yesu anaponya siku ya sabato. Kwa Wayahudi ikawa ni dhambi ya mauti. Sasa kati ya kuacha mgonjwa aendelee kuteseka, kushika sabato kwa sababu sheria inasema hivyo na kumponya mgonjwa ni ipi ina maana zaidi? Hii ndiyo taarifa tofauti  ya Kristo ya ukombozi, taarifa inayokomboa. Tofauti ya tatu ipo katika ujumbe wenyewe. Ujumbe wa Kristo watualika kubadilika moyoni.  Ujumbe wa walimu wa sheria unafanya watu wajisikie vibaya, unatisha, unaogofya. Yesu alipopelekewa yule kipofu, alimponya. Walimu wa sheria walitafuta ni nani aliyetenda ile dhambi. Yesu anafundisha na kutibu.  Wayahudi wanalaumu na kuona kufuru.

Ndugu zangu, huu mtazamo mpya wa Kristo uwe leo changamoto kubwa katika maisha yetu. Ni vizuri pia tukatumia neno la Mungu siku ya leo kuangalia maisha yetu ya ufuasi. Ni vizuri kuangalia sheria zetu na sheria au amri za Mungu na kuona tuko wapi au tukoje. Kama Kristo alivyofanya, tukumbuke kuwa jukumu la kwanza ni kumkomboa mwanadamu na hali yake mbaya. Hatuna budi kuweka katika matendo kile ambacho tunakiamini katika imani yetu kama Kristo alivofanya na alivyotufundisha kuishi. Neno la Mungu dominika hii ya leo latualika kuitikia sauti ya Mungu. Tumeona katika somo la kwanza jinsi mwandishi anavyotambua mapenzi ya Mungu. Mungu anaahidi nabii, mtu mpole, msemaji mwaminifu wa neno, mtu wa imani na mlinzi wa huruma ya Mungu. Ndiyo sisi leo. Sote tunatakiwa kuwa huyo nabii wa Mungu katika mazingira yetu ya leo. Katika injili, Yesu anasema waziwazi kuwa alipo yeye upo pia ufalme wake na wa Baba yake. Hivyo shetani hana nguvu tena. Uwepo wa Kristo ni uzima mpya na wa milele.

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.

24/01/2018 14:32