2018-01-24 11:07:00

Papa Francisko ataja yale "yaliyomkuna" huko Amerika ya Kusini


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa katekesi yake, Jumatano tarehe 24 Januari 2017, ametumia fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyemwezesha kufanikisha hija yake ya kitume huko Chile na Perù na hivyo, kubahatika kukutana na watu wa Mungu, ili kuwatia shime katika mchakato wa maendeleo endelevu. Anawashukuru viongozi wa Serikali, Kanisa na wale wote waliojisadaka bila ya kujibakiza, ili kufanikisha hija yake ya kitume kuanzia tarehe 15 – 22 Januari 2018.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kabla ya kuwasili nchini Chile, kulikuwepo na maandamano na matukio ya uchomaji moto Makanisa kutokana na sababu mbali mbali, ndiyo maana kauli mbiu ya hija ya kitume nchini Chile ilikuwa na maana sana kwa wakati huo yaani “Amani yangu nawapa”. Haya ni maneno ya Kristo Yesu kwa wanafunzi wake, yanayorudiwa wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu. Zawadi ya amani inatolewa na Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa mtu anayejiaminisha kwake!

Baba Mtakatifu anasema, alipokutana na viongozi wa kisiasa na vyama vya kiraia nchini Chile, amekazia umuhimu wa kukuza na kudumisha mchakato wa demokrasia kama fursa ya kujenga utamaduni wa kukutana na kushikamana hata katika tofauti zao msingi; kwa kusikilizana! Lakini zaidi kwa kuwasikiliza maskini, vijana wa kizazi kipya, wazee, wakimbizi na wahamiaji pamoja na kusikiliza kilio kinachotoka kwenye mazingira. Katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi takatifu, mkazo unawekwa zaidi katika ujenzi wa haki na amani kama njia ya kuwa ni watoto wa Mungu.

Huu ni ukweli wa mtindo wa maisha unaofumbatwa katika ujirani mwema, kwa kushirikiana, ili kuimarisha neema ya Kristo inayomwilishwa katika maisha ya Jumuiya ya waamini na jamii katika ujumla wake. Katika mazingira kama haya, matendo yana nguvu zaidi kuliko maneno. Baba Mtakatifu anasema, akiwa nchini Chile, alibahatika  kutembelea Gereza la wanawake wa Santiago. Akabahatika kukutana na wanawake wafungwa pamoja na watoto wao, licha ya mateso na mahangaiko ya gerezani, bado walikuwa wanaonesha matumaini. Amewataka wanawake hawa kupiga moyo konde, ili kujiandaa kikamilifu kuanza kuandika upya kurasa za maisha yao kama mwelekeo sahihi wa maisha ya kila siku.

Baba Mtakatifu anasema, alipata bahati ya kukutana na kuzungumza na wakleri pamoja na watawa na kuona shida, mateso na mahangaiko ya viongozi wa Kanisa kutokana na madonda yanayoendelea kuliandamana Kanisa nchini Chile. Amewataka wakleri kusimama kidete kupambana kufa na kupona na nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo pamoja na wakleri kupyaisha maisha na utume wao kwa kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anasema amebahatika kukutana na wananchi mahalia na huko amekazia umuhimu wa ujenzi wa amani na utulivu hatika utofauti za ona hivyo kukataa kishawishi cha kutaka kutumia nguvu kudai haki zao.

Kwa wananchi wanaoishi Kaskazini mwa Chile, Baba Mtakatifu anasema, ameshuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kiasi hata cha kuonja imani hiyo katika maisha ya kawaida. Alipokutana na vijana na wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Chile, Baba Mtakatifu anasema, hawa ni vijana wanaohitaji majiundo makini na endelevu ili kuwa na mang’amuzi ya maisha. Kwa kufuata mfano wa Mtakatifu alberto Hurtado, amewataka vijana kusoma alama za nyakati na kujikita katika majiundo endelevu yanayomwilisha utambulisho wa Kikristo ili kusaidia mchakato wa ujenzi wa jamii inayoshikamana katika umoja na utofauti; mahali ambapo kinzani na mipasuko mbali mbali haifumbiwi macho bali inashughulikiwa kikamilifu.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, kauli mbiu ya hija yake ya kitume nchini Perù ilikuwa ni “Umoja wa matumaini”. Huu ni umoja unaowaunganisha wananchi wote wa Perù katika utajiri na tofauti zao walizorithi katika historia na tamaduni. Amekutana na kuzungumza na wenyeji mahalia wa Amazonia. Ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali kutoka katika eneno hili ameamua kuitisha Sinodi ya Maaskofu wa Amazonia, itakatoadhimishwa kunako mwaka  2019. Amekutana na kushuhudia utajiri wa wananchi Puerto Maldonado; watoto yatima na wale wanaosihi katika mazingira magumu na hatarishi. Pamoja wamekataa ukoloni mamboleo unaofumbatwa uchumi na sera zake.

Kwa viongozi wa kiserikali na kiraia, Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kutambua na kudumisha urithi mkubwa wa mazingira nyumba ya wote, utamaduni  na maisha ya kiroho, ili kupambana na saratani ya rushwa na uharibifu wa mazingara kwani haya ni madonda makubwa yanayoendelea kuitesa jamii na kwamba, haya ni mapambano ya wote. Baba Mtakatifu anasema, ameadhimisha pia Ibada ya Misa Takatifu huko Trujillo ili kuwafariji waathirika wa tetemako la ardhi na kuwataka wananchi pia kusimama kidete dhidi ya ukosefu wa elimu, fursa za ajira pamoja na makazi salama. Kwa mapadre na watawa amewataka wajikite katika maisha na utume wa Kanisa kwa kujizatiti kujenga Kanisa nchini Perù pamoja na kuendeleza Ibada kwa Bikira Maria: Mama wa  huruma na matumaini.

Baba Mtakatifu anasema, amehitimisha hija yake ya kichungaji nchini Perù, Jumapaili tarehe 21 Januari 2018 kwa kukutana na kusali na watawa wa ndani 500. Amesali na kutoa heshima yake kwenye Masalia ya watakatifu wa Perù na baadaye kukutana na kuzungumza  na Maaskofu Katoliki wa Perù na kuwataka kuiga mfano bora wa Mtakatifu Turibius Mogrovejo. Baba Mtakatifu anakaza kusema, amewataka vijana wa kizazi kipya kuiga mifano bora ya watakatifu kwa kuondokana na unafiki, huku wakiongozwa na matumaini. Mwishoni wakati wa hija yake, amewataka waamini kutubu, kuongoka na kuiamini Injili, ili kupokea amani inayobubujujika kutoka kwa Kristo ili hatimaye wote waweze kudumisha umoja wa matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa,

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.