2018-01-23 13:32:00

Yaliyojiri katika mahojiano kati ya Papa Francisko na wanahabari


Baba Mtakatifu Francisko akiwa njiani kurejea mjini Vatican mara baada ya kuhitimisha hija yake ya 22 ya kitume kimataifa huko Amerika ya Kusini, kuanzia tarehe 15 hadi 22 Januari 2018 amepata fursa ya “kuchonga” na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake kwa takribani dakika 50 kavu! Amejibu maswali na kuondoa dukuduku za waandishi wa habari, kwa kuwapatia ukweli wa mambo ambao hata wakati mwingine si rahisi kuweza kuumeza, kwani unaumiza. Amewashirikisha mambo msingi yaliyomgusa katika sakafu ya moyo wake wakati wa hija yake ya kitume huko Amerika ya Kusini.

Baba Mtakatifu anasema, Liturujia ya Misa Takatifu Jimbo kuu la Lima, kama sehemu ya kuhitimisha hija yake ya kitume nchini Perù imeacha alama ya kudumu katika sakafu ya moyo wake. Anashukuru pia shuhuda mbali mbali zilizotolewa na waamini katika mikutano na ibada mbali mbali alizoziongoza wakati wote wa hija yake ya kitume! Huu ni ushuhuda wa imani ya watu wa Mungu inayomwilishwa katika furaha ya Injili. Anasema, kwa namna ya pekee kabisa, ameguswa na hali ya maisha na ushuhuda wa wafungwa; kipaji chao cha ugunduzi; ari na moyo mkuu wa toba na wongofu wa ndani, ili kufanya mageuzi makubwa katika maisha yao kwa nguvu ya mwanga wa furaha ya Injili. Kwa kukutana na kuzungumza na wafungwa hawa pamoja na watoto wao, watu wamefanikiwa kuona ushuhuda wa furaha ya Injili ukibubujika kutoka katika sura za wafungwa hawa.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, moyo na akili yake, bado imeguswa na ushuhuda wa watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu; watoto ambao kwa njia ya elimu na malezi makini, wamepata nafasi ya kusonga mbele wakiwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Hija hii ya kitume, imekuwa na chapa ya sera na mikakati ya kichungaji kwa kuwatembelea watu katika maeneo na mazingira yao; kwa kuonesha ari na moyo wa upendo na mshikamano kwa waathirika wa majanga asilia pamoja na kuanza kujenga utamaduni wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, ili kukuza na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo!

Baba Mtakatifu Francisko amezungumzia kwa masikitiko makubwa kuhusu kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo, iliyosababishwa na Padre Fernando Miguel Karadima huko Chile. Kashfa hii, ilizua mpasuko mkubwa kati ya wananchi wa Chile, waliomshutumu Askofu Juan Barros wa Jimbo Katoliki Osorno kwa kumfisha Padre Karadima ambaye alipaswa kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria. Kutokana na shinikizo la baadhi ya wananchi wa Chile, Askofu Juan Barros mara kadhaa alimwandikia Baba Mtakatifu Francisko barua ya kutaka kung’atuka madarakani kwa manufaa ya watu wa Mungu, lakini akamtalia baada ya kufanya uchunguzi wa kina na kubainisha bila wasi wasi kwamba, hizi zilikuwa ni njama za baadhi ya watu kutaka kumchafulia jina. Siku ya kusimikwa kwake kama Askofu wa Jimbo Katoliki Osorno, baadhi ya watu walimshambulia si tu kwa maneno, bali hata kwa kutumia nguvu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, ana amini kwamba, Askofu Juan Barros hana hatia kwa shutuma zinazotolewa dhidi yake, kumbe ataendelea na utume wake kama Askofu. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, kuna baadhi ya watu wamekwazika kwa maneno yake, aliposema kwamba, hakuna ushahidi unaomtia hatiani, “alitibua nyongo ya waathirika” wa nyanyaso za kijinsia, kiasi hata cha kumkatisha tamaa Kardinali  Sean Patrick O’Malley, Mwenyekiti wa Tume ya Kipapa ya Kulinda Watoto Wadogo, PCPM. Baba Mtakatifu anaomba msamaha kwa maneno ambayo ameyatumia bila kuwa na lengo la kutaka kuwakwaza watu, bali alikua anakazia ukweli wa mambo. Askofu Juan Barros ataendelea kubaki kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Osorno. Baba Mtakatifu anakaza kusema, amemshukuru Kardinali Sean Patrick O’Malley kwa msimamo na mchango wake katika mapambano dhidi ya nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa. Vitendo kama hivi, havitavumiliwa tena katika maisha na utume wa Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake kitume nchini Chile, wakati akitoka Jimbo kuu la Santiago kuelekea Jimbo Katoliki la Iquique, nchini Chile, Alhamisi tarehe 18 Januari 2018 aliwahoji na hatimaye, kupokea nia njema ya kufunga ndoa wafanyakazi wawili wa Shirika la Ndege lililokuwa linamsafirisha Baba Mtakatifu pamoja na msafara wake. Wanandoa hawa wapya ni Paula Podestà Ruiz mwenye umri wa miaka 39 na Carlos Cuffando Elorriaga, mwenye umri wa miaka 41, walilazimika kuhailisha kufunga ndoa yao Kanisani kunako mwaka 2010 kutokana na tetemeko kubwa lililoitikisa Chile na kuacha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Baba Mtakatifu anasema, wanandoa hawa walikuwa tayari wameandaliwa barabara, kumbe, hakuona sababu ya msingi kusubiri tena miaka kumi ili wao kuweza kufunga ndoa.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, sera na mikakati ya utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote haina budi kwenda sanjari na mchakato wa kulinda na kumisha haki msingi za binadamu, utu na heshima yake! Wanaharakati wasipiganie haki za kulinda misitu na kusahau maisha ya watu wanaoishi msituni humo. Umefika wakati kwa Amerika ya Kusini kujizatiti katika mapambano dhidi ya saratani ya rushwa na ufisadi ambayo ni hatari sana kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hata rushwa ndani ya Kanisa ina madhara yake makubwa kwa maisha na utume wa Kanisa.

Kuhusu shutuma dhidi ya Kardinali Oscar Rodríguez Maradiaga kwamba, amekula fedha ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki Cha Honduras, Baba Mtakatifu anasema, Kardinali Maradiaga alikwisha kujibu tuhuma hizi kwani fedha ya Kanisa inatumika vyema kwa ajili ya ustwi na maendeleo ya Kanisa. Shutuma zinalenga kukwamili mchakato wa mgeuzi mjini Vatican.Chile katika kipindi cha miaka 20 iliyopita imepunguza idadi ya kiwango cha umaskini kutoka asilimia 40% hadi kufikia asilimia 11%. Kumbe, sera na mikakati ya maendeleo inapaswa kuashiriksha wananchi wote pasi na ubaguzi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.