2018-01-23 11:14:00

Jukwaa la Uchumi Duniani 2018: Utu, haki msingi na maendeleo!


Kanisa Katoliki linaunga mkono sera na mikakati ya uchumi na maendeleo endelevu ya watu yanayozingatia: haki msingi za binadamu, utu na heshima yake: sera zinazokazia: haki, wajibu na usawa katika utekelezaji wa sera na mikakati hii katika maisha ya watu. Uongozi katika ngazi ya kimataifa unaendelea kumeguka kati ya Serikali na Taasisi, hali inayopelekea uwapo wa watu wapya, mashindano ya kiuchumi na itifaki za makubaliano ya kiuchumi. Maendeleo ya sayansi na teknolojia katika mchakato wa uzalishaji yanaendelea kuibua mifumo mbali mbali ya uchumi katika ulimwengu mamboleo. Matokeo yake ni ongezeko la uchu wa mali, madaraka pamoja na faida kubwa, mambo yanachangia kukua na kukokamaa mipasuko ya kijamii, ubinafsi na ubaguzi. Kumekuwepo na ongezeko kubwa la watu wasiokuwa na ajira, hali inayochangia kuongezeka kwa wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani bila kusahau kinzani za kijamii na kifamilia zinazochangiwa kwa kiasi kikubwa na utandawazi usiojali wala kuguswa na mateso na mahangaiko ya watu wengine. 

Maendeleo ya sayansi na ukuaji wa uchumi ni masuala ambayo yamekuwa na mvuto na mashiko katika maisha ya hadhara ya Jumuiya ya Kimataifa na matokeo yake, binadamu anashindwa kupewa kipaumbele cha pekee katika sera na mikakati ya maendeleo! Binadamu anageuzwa na kuwa kama bidhaa au mlaji wa kupindukia; maisha ya binadamu hayana thamani kubwa na matokeo yake ni nyanyaso na madhulumu! Huu ni ujumbe ambao Baba Mtakatifu Francisko, amemwandikia Professa Klaus Schwab, Mwenyekiti mtendaji wa Jukwaa la Uchumi Duniani kwa mwaka 2018, ambalo limefunguliwa rasmi tarehe 22 Januari 2018 na ujumbe wa Baba Mtakatifu kusomwa na Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Endelevu ya Binadamu. Jukwaa hili linatarajiwa kufungwa tarahe 26 Januari 2018 huko Davos, nchini Uswiss.

Baba Mtakatifu anakazia kwa namna ya pekee, utu na heshima ya binadamu na umuhimu kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika kukuza na kudumisha mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu, kwa kuibua na kutekeleza sera na mikakati inayotoa kipaumbele kwa familia, uhuru wa binadamu na haki zake msingi, ili kweli watu waweze kuwa ni wadau wakuu wa mchakato mzima wa maendeleo yao. Nguvu za soko hazina budi kuratibiwa na haki msingi za wafanyakazi. Kumbe, mifumo ya kiuchumi haina budi kuzingatia sheria na kanuni za maendeleo endelevu ya binadamu, daima mwanadamu na haki zake msingi akipewa kipaumbele cha kwanza.

Vikwazo vya haki msingi za binadamu na upweke hasi ni mambo ambayo yanapaswa kuvaliwa njuga duniani ili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano, kwa leo na kwa siku za usoni, ili kutoa mwelekeo mpya wa uchumi duniani. Sayansi na teknolojia rafiki haina budi kutumika ili kusaidia mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu; ulinzi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu anasikitika kusema, kwamba, watu wengi sana duniani, utu wao umejeruhiwa na kwamba, kuna mambo mengi yanayoendelea kuwatumbukiza watu katika dimbwi la umaskini na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanapaswa kutambua kwamba, ni wajibu na dhamana yao ya kimaadili kuwashirikisha watu wengi katika mapambano dhidi ya umaskini na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Huu ni mwaliko wa kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani na kwamba: ulimwengu una wajasiria mali wengi na uwezo wa kufanya mageuzi ya busara ili kuongeza tija na ubora wa huduma na bidhaa zinazozalishwa. Inawezekana kabisa kutengeneza nafasi za ajira kwa kuheshimu sheria za kazi; kwa kupambana na rushwa na ufisadi wa mali ya umma; kwa kuendeleza haki jamii na usawa katika matumizi ya faida inayopatikana.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hii ni dhamana nyeti sana inayopaswa kutekelezwa kwa kufanya mang’amuzi makubwa, kwani maamuzi yake ni muhimu sana katika kuunda ulimwengu ujao unaofumbatwa katika usalama na ustawi na mafao ya wengi kwa kuzingatia tunu msingi za maisha; kwa kujikita katika mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu pamoja na utunzaji bora wa mazingira, kwa ajili ya ustawi wa binadamu.  Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, Jukwaa la Uchumi Duniani kwa mwaka 2018, itakuwa ni nafasi: wazi, huru na mahali pa heshima, ari na hamu ya kutaka kujenga na kudumisha mafao ya wengi. Kauli mbiu ya mwaka 2018 ni ”Kutengeneza kesho inayowashirikisha watu katika ulimwengu uliomeguka”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.