2018-01-22 15:10:00

Papa: Watakatifu wa Mungu ni mashuhuda wa imani, upendo na matumaini!


Mama Kanisa anafundisha na kusadiki kwamba, ushirika wa watakatifu ndilo Kanisa hasa, kwani huu ni ushirika wa mema ndani ya Kanisa, lakini kubwa zaidi, ni ushirika wa mambo matakatifu na ushirika kati ya watu watakatifu. Ni ushirika wa imani, karama na mapendo unaowaunganisha wote kuwa chini ya Kristo Yesu, Mchungaji mkuu.  Historia inaonesha kwamba, nchi ya Perù ni chimbuko la watakatifu huko Amerika ya Kusini. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Perù, Jumapili, tarehe 21 Januari 2018 amepata nafasi ya kutembelea Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane Mwinjili na kutoa heshima yake, mbele ya masalia ya watakatifu kutoka nchini Perù. Tukio hili limehudhuriwa na idadi kubwa ya watu wa Mungu, Jimbo kuu la Lima.

Baba Mtakatifu Francisko katika sala yake mbele ya masalia ya watakatifu wa Perù, amemshukuru Mwenyezi Mungu ambaye kwa njia ya Kristo Yesu amelianzisha Kanisa chini ya msingi wa Mitume na kuongozwa na Roho Mtakatifu, ili liweze kuwa duniani alama ya upendo wa Mungu wenye huruma. Anamshukuru Mungu kwa utakatifu unaoendelea kuchipuka huko Amerika ya Kusini, lakini zaidi katika Jimbo kuu la Lima, ambalo ni matunda ya kazi na jasho la Mtakatifu Turibius Mogrovejo aliyekita maisha yake katika sala, toba na upendo; wengine ni watakatifu Rosa wa Lima, Mtakatifu Martin de Porres na Francesco Solano, waliojipambanua kwa ari na moyo wa kimissionari, bila kusahau huduma ya upendo wa Kiinjili uliotangazwa na kushuhudiwa na Mtakatifu Yohane Macìas; aliyebarikiwa kutoa ushuhuda wa Kikristo, bila kuwasahau watakatifu wote ambao kweli wamekuwa ni waaminifu kwa Injili na mchango wao katika maisha na utume wa Kanisa unaonekana.

Baba Mtakatifu anamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwajalia watu wa Mungu nchini Perù kuwa waaminifu kwa amana waliyoipokea na kuirithi. Anamwomba Mwenyezi Mungu ili alijalie Kanisa liweze kuwa na ari na moyo wa kutoka katika undani wake, na kuwaendea watu wote, hasa zaidi maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Awafundishe kuwa mitume wamissionari wa Kristo Yesu, Bwana wa miujiza, kwa kuhakikisha kwamba, wanamwilisha upendo, daima wakitafuta umoja na kujizatiti katika kumwilisha huruma ya Mungu katika maisha ya watu wanaowazunguka. Waamini wakiwa wanalindwa kwa tunza ya Bikira Maria, Mama wa uinjilishaji, waweze kuishi na kutangaza furaha ya Injili ulimwenguni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.