2018-01-22 13:30:00

Papa Francisko akazia: Huduma ya upendo, utamadunisho, malezi na umoja


Umoja wa Matumaini unaofumbatwa katika huduma ya mapendo kwa watu wa Mungu nchini Perù, kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji na utamadunisho wa Habari Njema ya Wokovu; Uinjilishaji unaojikita katika Injili ya upendo na majiundo makini ya wakleri na watawa ni chemchemi ya umoja na mshikamano wa Kanisa. Haya ndiyo mambo msingi ambayo Baba Mtakatifu Francisko amekazia alipokutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Perù, Jumapili, tarehe 21 Januari 2018 huko kwenye Makao makuu ya Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Lima.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, bado anayo kumbu kumbu hai ya hija yao ya kitume, inayofanyika walau kila baada ya miaka mitano mjini Vatican. Uwepo wake miongoni mwa watu wa Mungu nchini Perù umemwezesha kusikiliza, kuona na kushuhudia imani na maisha ya wananchi wa Perù na kwa namna ya pekee kabisa, amebahatika kugusa imani ya watu wanaowahudumia. Umoja wa Matumaini ndiyo kauli mbiu inayoongoza hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Perù kwa mwaka 2018 na kwa namna ya pekee, amemtaja Mtakatifu Turibius Mogrovejo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Lima, Msimamizi wa Maaskofu wa Amerika ya Kusini, aliyejisadaka katika ujenzi wa umoja wa Kanisa, akathubutu kupiga kasia hadi kuvuka ng’ambo ya pili ya mto! Nyuma yake kulikuwepo na umati mkubwa wa watu uliokuwa unamfuata kama kiongozi katika mchakato wa uinjilishaji.

Huu ndio mfano bora wa kuigwa, ambao Baba Mtakatifu Francisko amependa kuwaonesha Maaskofu Katoliki Perù . Tangu mwanzo wa maisha na utume wake, Mtakatifu Turibius Mogrovejo, alijipambanua kuwa ni “Baba na Mchungaji”, aliyejisadaka katika imani, kiasi hata cha kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili kuvuka ng’ambo ya pili, ambako umati mkubwa wa watu ulikuwa unamsubiri kwa hamu. Katika maisha na utume wake kama Askofu, alijitahidi kwenda kwa watu na mazingira yaliyokuwa yanahitaji uwepo wake. Katika kipindi cha miaka 22 ya utume wake kama askofu mahalia, miaka 18 aliitumia nje ya makao makuu ya askofu kwa ajili ya huduma na kwa kuwatembelea na kuwa karibu zaidi na watu wake, kama mtindo wake wa shughuli za kichungaji, ili kuwagawia watu wa Mungu, Mafumbo ya Kanisa, dhamana aliyoitekeleza kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake mwenyewe, akawaalika wakleri wake kuiga mfano huo. Akawa mstari wa mbele katika mchakato wa uinjilishaji, ili kuwatangazia watu wa Mungu furaha ya Injili katika hali na mazingira yao.

Ni kiongozi aliyethubutu kuvuka ng’ambo ya pili si tu kijiografia bali hata kitamaduni kwa kuhakikisha kwamba, Katekisimu zinatafsiriwa katika lugha za watu mahalia, wakleri wanajifunza lugha, mila na desturi njema ili kuhakikisha kwamba, Injili ya Kristo inatamadunishwa katika mazingira ya watu mahalia, ili kufahamika na hatimaye, kukita mizizi yake katika sakafu ya mioyo ya waamini. Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu kusoma alama za nyakati, hasa katika kipindi hiki cha maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ili waweze kufikisha furaha ya Injili kwa watu wao sanjari na kutambua lugha ya vijana wa kizazi kipya, ili kweli imani iweze kuzama na kuota mizizi katika maisha yao. Hii ni dhamana kwa Maaskofu kuhakikisha kwamba, Neno la Mungu linafahamika na kuzama katika maisha ya watu wao kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji wa utamadunisho.

Baba Mtakatifu Francisko anakazia pia uinjilishaji wa upendo unaowawezesha waamini kushirikishana upendo na jirani zao, kwa kujizatiti zaidi katika misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Uinjilishaji wa upendo, uliwezeshe Kanisa nchini Perù kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu; ustawi na maendeleo ya wengi, huku utu na heshima ya binadamu vikipewa kipaumbele cha pekee. Mtakatifu Turibius Mogrovejo, mara baada ya maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Trent, alianzisha seminari ndogo kwa ajili ya majiundo makini ya wakleri mahalia na kwamba, utambulisho wao mkubwa ulifumbatwa katika utakatifu wa maisha na wala si kabila au mahali alipotoka padre.

Ni Askofu aliyekazia malezi na majiundo ya wakleri wake, akawafahamu kwa kina na mapana na hivyo kuwasaidia katika mahitaji yao msingi: kiroho na kimwili. Alisimama kidete, kulinda na kuwatetea watu mahalia, kama alama Mchungaji mwema. Alikazia umoja wa familia ya Mungu Jimboni mwake na matunda ya juhudi hizi ni umoja wa imani, sheria na kanuni za shughuli za kichungaji, ustawi na maendeleo endelevu ya Amerika ya Kusini.  Alikutana na changamoto, kinzani na mipasuko, lakini akawa tayari kukabiliana na changamoto hizi kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi, kiasi cha kufanikiwa kuwa hata na umoja katika maisha. Huu ni mfano bora wa kuigwa kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki ulimwenguni.

Maaskofu wanakumbushwa kwamba, wanaitwa na kutumwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Sakramenti ya umoja kama kielelezo makini cha mchakato mzima wa uinjilishaji. Changamoto kwa Kanisa nchini Perù ni kuendelea kushikamana katika mambo matakatifu kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Turibius Mogrovejo hadi dakika ya mwisho, alipoitupa mkono dunia. Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa kusema, huu ndio urithi ambao anapenda kuwaachia Maaskofu wenzake anapohitimisha hija yake ya kitume nchini Perù.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.