2018-01-21 14:05:00

Wakleri na watawa: zingatieni: utambuzi binafsi, mwaliko na furaha!


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa heshima ya Bikira Maria Mlango wa mbingu, Jumamosi tarehe 20 Januari 2018 huko kwenye Uwanda wa Huanchaco (Wanchako) kwa kukazia umoja, upendo na mshikamano ili kuweza kukabiliana na Tsunami za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii, alipata bahati ya kukutana na kuzungumza na wakleri, watawa na majandokasisi, kwenye Seminari ya Watakatifu Carlos na Marcelo, Jimbo kuu la Trujillo, nchini Perù wakati wa hija yake ya kitume nchini humo! Amewashukuru viongozi wa Kanisa kwa sadaka na majitoleo yao kwa ajili ya huduma makini kwa familia ya Mungu nchini Perù.

Seminari ya Watakatifu Carlos na Marcelo, Jimbo kuu la Trujillo ni seminari ya kwanza kujengwa na Kanisa Katoliki huko Amerika ya Kusini kunako mwaka 1625 kama kitovu cha majiundo makini kwa wakleri na watawa. Seminari hii imekuwa ni chemchemi ya maisha na utume wa wamissionari wengi waliosadaka maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa. Kanisa kwa namna ya pekee linamkumbuka Mtakatifu Turibius Mogrovejo, Askofu na msimamizi wa Maaskofu Amerika ya Kusini, anayeendelea kuwasindikiza kwa sala ili wakleri na watawa waweze kuzamisha mizizi ya maisha na utume wao ili kuzaa matunda ya toba na wongofu wa ndani kwa watu wa Mungu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, bila mizizi thabiti katika maisha na utume wao, watanyauka na kutoweka kama ndoto ya mchana! Watambue kwamba, Kanisa ni Mama mwema na mwalimu; pale wakleri na watawa wanapoanza kumezwa na malimwengu, wawe na ujasiri wa kutubu na kumwongokea Mungu, kwani Kristo Neno wa Mungu amekuja kumwokoa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Imani na historia ya miito inebeba utajiri mkubwa wa kumbu kumbu hai, ili kuweza kuyaangalia yaliyopita kwa moyo wa shukrani kwani hii ni historia ambayo ina chapa ya uwepo wa Mungu. Kuyaambata ya sasa kwa moyo mkuu kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu yuko kati pamoja nao na ndiye chemchemi ya furaha ya maisha na utume wao ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Mwenyezi Mungu anawajalia “jeuri” ya kuimba na kutangaza matendo makuu ya Mungu katika maisha yao, tayari kuyaendea ya mbeleni kwa ari na moyo mkuu!

Baba Mtakatifu Francisko katika tafakari yake kwa wakleri, watawa na majandokasisi amekazia mambo makuu matatu: kwanza kabisa ni ile furaha ya utambuzi wa mtu binafsi, kwa kile anachotenda. Pili ni kutambua muda wa mwaliko wa kumfuasa Kristo Yesu na tatu ni mwelekeo wa furaha inayoshirikishwa kwa wengine. Yohane Mbatizaji ni shuhuda wa Mwana Kondoo wa Mungu, aliyethubutu kumtambulisha kati ya watu wa Mataifa, akasimamia na kushuhudia ukweli, hadi kukatwa kichwa kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ushuhuda kwa Kristo Yesu.

Mosi, Utambuzi wa mtu binafsi: karama na mapungufu yake ya kibinadamu!

Baba Mtakatifu anawaalika wakleri na watawa kuhakikisha kwamba wanamtangaza Kristo Yesu kama chemchemi ya furaha ya Injili; wanamshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili; kielelezo makini cha imani tendaji na sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Viongozi wa Kanisa watambue kwamba, wao wote ni mitume wa Kristo Yesu, wanaotumwa: kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha ya maisha na utume wa viongozi wa Kanisa na kamwe wao si Masiha. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya huduma kwa kuwaelekeza waamini mambo msingi ya kuzingatia na kumwachia Roho Mtakatifu ili aweze kutenda kazi yake katika mchakato mzima wa uinjilishaji.

Baba Mtakatifu anawataka wakleri na watawa kupambana na kishawishi cha kujitafuta wenyewe, kutaka kujikuza na kujijengea umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya! Wawe na utambuzi kwamba, wanaitwa na kutumwa; wamekirimiwa karama na mapaji, lakini pia wametwaliwa kati ya watu kwa ajili ya mambo matakatifu, kumbe, wao pia wanayo mapungufu yao ya kibinadamu yanayopaswa kurekebishwa kila wakati, ili daima waweze kuwa ni chemchemi ya furaha kati pamoja na jirani zao. Wawe ni watu wa tabasamu na kicheko; watu wa sala na tafakari; watambue karama na mapungufu yao.

Pili ni kutambua muda wa mwaliko wa kumfuasa Kristo Yesu. Hili ni tukio ambalo linaacha chapa ya kudumu katika historia ya maisha ya mfuasi wa Kristo, kiasi hata cha kukukumbuka ile saa ya kufanya maamuzi machungu katika maisha, baada ya kukutana na Kristo, akamwangalia kwa jicho la huruma na mapendo, kiasi cha kubadilisha mwelekeo mzima wa maisha yake kama ilivyokuwa kwa wafuasi wa Yohane Mbatizaji. Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, iwasaidie wakleri na watawa kumsikiliza Kristo Yesu kutoka katika undani wa maisha yao; kumpatia nafasi ya kuwagusa, kuwaganga na kuwaponya udhaifu wao; tayari kuwatasa na kuwatuma kwenda kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; Injili ya upendo dhidi ya ubinafsi na uchoyo; Injili ya huruma ya Mungu kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii bila ya kujitafutia umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko kama walivyokuwa wanafanya Mafarasayo.

Baba Mtakatifu amekumbushia umuhimu wa kuendeleza ile misingi ya imani waliyorithi kutoka kwa wazazi na walezi wao ndani ya familia. Huu ndiyo moyo wa ibada na uchaji wa Mungu; moyo wa hija, toba na matendo ya huruma na wongofu wa ndani; msamaha na upatanisho. Haya ni mazingira ambayo, kwa wakleri na watawa wengi, yamekuwa ni chemchemi ya maisha na miito yao ya kipadre na kitawa! Waheshimu ibada za watu mahalia; wawe ni mifano bora ya sala na maisha ya kiroho.

Hapa kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu anamkumbuka Mtakatifu Francisco Solano, mhubiri mkuu na rafiki wa maskini anayetambua kuwa vyote alivyo navyo ni mali ya Mungu inayopaswa kutumiwa katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika Injili ya upendo na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa kuwaganga na kuwatibu kwa mafuta ya furaha na shukrani! Kwa hakika watu wa Mungu anasema Baba Mtakatifu Francisko wanawatambua  mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya matendo yao na wala si “ngembe” wanazopiga kwenye mimbari!  Wakleri na watawa wawe na ujasiri wa kusikiliza na kupokea ushauri kutoka kwa waamini wao ili kujenga utamaduni wa kusikilizana, kuaminiana, kupendana na kukamilishana. Wakleri na watawa wajipatie muda wa mapumziko, ili kuwatembelea wazazi, ndugu na jamaa zao kama njia ya kujipyaisha tena katika maisha na utume wao.

Tatu ni mwelekeo wa furaha inayoshirikishwa kwa wengine. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Wafuasi wa Yohane Mbatizaji walikuwa na furaha kubwa, ambayo waliwashirikisha pia ndugu zao na kuwapeleka kwa Kristo Yesu. Hii ni changamoto kwa wakleri na watawa kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni maabara ya miito mitakatifu ndani ya Kanisa kwa njia ya ushuhuda wa maisha na utume wao kwa Kristo na Kanisa lake. Viongozi wa Kanisa wawe kweli ni mashuhuda wa furaha ya Injili kwa watu wanaowahudumia, ili kutoa nafasi kwa watu kuonja uwepo endelevu wa Kristo Mwana wa Mungu aliyekuja kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Kristo daima anapenda kupyaisha furaha kwa waja wake!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, furaha ya Injili ni zawadi ambayo waamini wanaitwa na kutumwa ili kuwashirikisha jirani zao, kwani Mwenyezi Mungu anapenda kuwakomboa binadamu wakiwa wameshikamana kwa dhati, kwani Mungu ni upendo. Vita, kinzaji, utengano na mipasuko mbali mbali katika: maisha na utume wa Kanisa; kwenye nyumba za kitawa na kwenye Mabaraza ya Maaskofu, ni hatari sana kwa maisha na utume wa Kanisa mahalia. Wakleri na watawa watambue kwamba, wanaitwa kuwa ni vyombo na wajenzi wa umoja na mshikamano; kwa kutambua na kuthamini: tofauti msingi zinazoweza kujitokeza minatarafu karama, tamaduni au mahali anapotoka mtu kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye peke yake utimilifu wa karama zote.

Wakleri na watawa waondokane na kasumba ya ubinafsi na uchoyo kama ilivyooneshwa kwenye simulizi la Baba mwenyehuruma. Uongozi ndani ya Kanisa ni kielelezo cha utume na huduma kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Wajenge utamaduni wa kusikiliza na kujadiliana na vijana wa kizazi kipya na “Vijana wa zamani”; kwa kuwapokea na kuwasikiliza kwa dhati. Kanisa lijenge na kudumisha utamaduni wa kuwakutanisha watu ili kuzungumza na kujadiliana; mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha tafakari yake kwa kusema, viungo vyote vya Fumbo la Mwili wa Kristo, vipewe fursa ya kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa kama kielelezo cha utume wa kinabii! Vijana wanayo tabia ya kutembea kwa haraka, lakini njia inafahamika na wazee. Wakleri na watawa wawe ni vyombo na mashuhuda wa upendo na mshikamano wa umoja wa matumaini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.