2018-01-21 15:56:00

Papa Francisko atembelea na kuwafariji waliofikwa na maafa mwaka 2017


Baba Mtakatifu Francisko Jumamosi tarehe 20 Januari 2018 baada ya kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu, kukutana na kuzungumza na wakleri, watawa na majandokasisi pamoja na kuadhimisha Ibada ya Misa takatifu kwa heshima ya Bikira Maria Mlango wa mbingu, Mama wa huruma ya Mungu na matumaini, alipata nafasi pia ya kutembelea kitongoji cha “Buenos Aires” huko Jimbo kuu la Truyillo, nchini Perù ili kujionea mwenyewe maafa makubwa yaliyosababishwa na mvua za “El Nino”, mwezi Aprili, 2017. Baba Mtakatifu amewatakia wananchi wa kitongoji hiki huruma na upendo wa Mungu katika jitihada za kuanza upya na kwamba, wasikate tamaa, bali waendelee kusindikizwa na kuajiminisha kwenye Injili ya matumaini.

Jioni, Baba Mtakatifu Francisko aliporejea tena mjini Lima, kwenye Makao makuu ya Ubalozi wa Vatican alikutana na umati mkubwa wa waamini na watu wenye mapenzi mema waliofika kumtakia heri na matashi mema. Kati yao, kulikuwepo na mapadre na watawa wagonjwa. Akasali pamoja nao na kuwataka viongozi wa Kanisa kuwa karibu sana na wagonjwa ili kuwaonjesha Injili ya matumaini katika shida na mahangaiko yao. Baba Mtakatifu amewaomba waamini pia kuwakumbuka na kuwaombea wagonjwa, ili Bikira Maria faraja ya wagonjwa aweze kuwasindikiza katika safari ya maisha yao na kuwafariji. Baadaye, akawapatia wote baraja zake za kitume! Akaifunga Jumamosi ya tarehe 20 Januari 2018 wakati wa hija yake ya kitume nchini Perù!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.