Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Mama Kanisa anayo maji ya Ubatizo na machozi ya Kitubio

Mtakatifu Ambrose anasema, Kanisa lina maji ya Ubatizo na machozi ya Toba - ANSA

20/01/2018 12:46

Mungu aketiye katika nuru isiyoweza kukaribiwa amependa, kwa njia ya mwanae wa pekee Bwana wetu Yesu Kristo, kumshirikisha mwanadamu uzima wa kimungu. Naye Kristo ambaye ndiye ukamilifu wa ufunuo wa Mungu na ukamilifu wa mpango wa Mungu wa wokovu kwa mwanadamu anamwalika mwanadamu kuupokea uzima huo kwa njia ya kuupokea ufalme wa Mungu. Na hiki ndicho kimekuwa kiini cha mafundisho yake yote. Maandiko Matakatifu katika dominika ya tatu ya mwaka B wa Kanisa yanayaupyaisha kwetu mwaliko wa Yesu wa kuupokea ufalme wa Mungu na tena tukiisha kuupokea yanatuelekeza namna ifaayo ya kuishi hapa duniani kama waana wa ufalme huo.

Somo la kwanza (Yona 3:1-5,10) linaeleza wito wa Yona kwenda kupeleka ujumbe wa Mungu kwa watu wa Ninawi. Hii ni mara ya pili Yona kuitwa na Mungu na kupewa ujumbe kwenda kwa waninawi. Mara kwanza alikaidi na akajaribu kutoroka kwenda Tarshishi. Katika awamu hii, Yona anakubali. Anaenda Ninawi, mji unaotajwa kuwa mkubwa na wa mwendo wa siku tatu lakini Yona anauingia kwa siku moja. Ndiyo kusema kwamba, ndani ya siku moja, badala ya Yona siku tatu kama ilivyotegemewa kulingana na ukubwa wa mji, waninawi wanaupokea ujumbe huo na wanafanya toba: wanatangaza kufunga na wanajivika magunia. Matokeo yake Mungu Mungu anaghairi kuwaadhibu.

Somo la pili (1Kor. 7:29-31) ni sehemu ya mausia ya mtume Paulo kwa Wakorinto ambapo ni kama anatoa hitimisho la mafundisho aliyokuwa amewapa kuhusu masuala mbalimbali ya kiimani, kimaadili na kijamii. Hapo anawakumbusha kuwa hawana muda mwingi kiasi cha kujishikamanisha sana na mambo ya kidunia, yawe ni ni yale yanayowapendeza au hata yale yasiyowapendeza: “wenye wake wawe kama hawana, waliao wawe kama hawalii na wale wafurahiao kama hawafurahi...” Ni hitimisho linalokazia kuwa watafanikiwa kuzishinda changamoto mbalimbali za kiimani, kimaadili na kijamii kati yao kama hawatajishikamanisha na malimwengu. Somo la Injili (Mk. 1:14-20) linaendeleza mwanzo wa utume wa hadhara wa Yesu. Yesu anaanza utume wake wa hadhara baada ya mtangulizi wake, Yohane Mbatizaji kufungwa gerezani. Ujumbe au agenda anayoanza nayo Yesu ni hii “wakati umetimia na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni na kuiamini Injili.” Kisha kuitambulisha agenda yake anawachagua mitume ambao watamsaidia kuieneza agenda hiyo ya wokovu kwa ulimwengu mzima. Nao wanaacha yote; kazi ya uvuvi wa samaki, vyombo vya uvuvi, baba na wafanyakazi, kisha wanamfuata.

Ufalme wa Mungu umeanza kwa ujio wa Kristo na unaendelea kujengwa kwa kazi ya ukombozi ya Kristo ambayo inaendelea kwa njia ya Kanisa. Ni ufalme ambao utakamilika atakaporudi kwa mara ya pili kwa utukufu pale atakapokuwa “yote katika yote” na kutawala juu ya yote.   Ufalme huu haufungamanishwi na mahali. Unaanza tukingali hapa hapa duniani kwa njia ya ubatizo: kumkataa shetani, kuikataa dhambi na kukubali kuishi maisha yanayotawaliwa na kuongozwa na uwepo wa Mungu. Ndiyo kusema kuwa, katika dunia hii hii kuna namna ya kuishi duniani ukiwa ndani ya ufalme wa Mungu na kuna namna ya kuishi duniani ukiwa nje ya ufalme wa Mungu. Kristo katika sala yake ya kikuhani hakumwomba Mungu awaondoe duniani wafuasi wake bali awalinde na yule mwovu kwa vile wao wanaishi duniani ilhali si wa duniani (rej Yoh. 17:15-16). Maandiko Matakatifu siku ya leo yanatualika tuishi katika maisha ya hapa duniani tukiwa  ndani ya ufalme.

Mausia ya mtume Paulo kwa Wakorinto (somo la pili) pamoja na kutoa mausia yaliyohusu changamoto za wakati, yanatupatia kanuni ifaayo kuishi duniani kama wana wa ufalme wa Mungu. Mtume Paulo hana maana ya kutualika tujitenge na dunia, tusishughulikie ustawi wa jamii wala kuitikia changamoto mbalimbali za wakati. Anachotualika ni kuishi maisha ya imani tukiwa duniani kiasi kwamba tusiwe mateka wala tusimezwe na malimwengu. Tusipelekwe mkumbo na mivuto ya dunia na maelekeo yake hata tukapoteza imani au utambulisho wetu kuwa sisi ni akina nani. Mlango wa kuingia katika ufalme wa Mungu hufunguliwa kwa sakramenti ya Ubatizo, sakramenti ya imani na ya wongofu. Na kwa njia ya toba, tunaendelea kuupokea mwaliko wa ufalme katika kila siku ya maisha yetu. Mtakatifu Ambrose anafundisha kuwa katika Kanisa kuna wongofu kwa njia ya maji na kwa njia ya machozi. Njia ya maji ndio Sakramenti ya Ubatizo na njia ya machozi ndiyo toba - Sakramenti ya kitubio (Rej. KKK 1429). Hizi ndizo hatua mbili muhumu katika kupanda ngazi kuuelekea ufalme wa Mungu. Ni ngazi anazozitaja Kristo anaposema “tubuni na kuiamini injili”.

Mwaliko wa Kristo, kutubu na kuiamini injili ni mwendelezo wa ujumbe wa toba ambao tangu mwanzo Mungu amewaalika watu wake Israeli kwa njia ya manabii mbalimbali aliowatuma kwao. “jitakaseni, jiosheni, jitengeni na uchafu....” ni maneno yanayotumiwa karibu na kila nabii ili kuwarudisha waisraeli kila wanapoenda nje ya agano lao na Mungu. Kwa njia ya Sakramenti ya Kitubio, tunaona kuwa mwaliko huu wa Kristo unakwenda hatua zaidi na kutaka kuwa matendo ya nje kama vile kuvaa magunia, kufunga na kujikatalia yanapaswa kuambatana na toba ya ndani ya moyo ambayo ni kuugeuza moyo kumuelekea Mungu. Ni toba hii inayoleta matunda zaidi kama maondoleo ya dhambi na kurudisha neema ya utakaso.

Mwisho wa tafakari hii tunapata nafasi ya kujihoji wenyewe: Ninataka kuishi duniani nikiwa ndani ya ufalme wa Mungu au nikiwa nje? Ninajitahidi kiasi gani kupambana na changamoto za kiimani na kimaadili katika maisha maisha yangu, imani niliyoikiri kwa ubatizo na kuishuhudia kwa maisha yangu ya Kikristo? Ninaungama na kufanya toba mara kwa mara au ninaingia katika kishawishi cha kusema muda bado nitatubu sikukuu ya Noeli au Pasaka ikikaribia? Wakati umetimia na ufalme wa Mungu umekaribia. Nitubu sasa na kuiamini Injili

Padre William Bahitwa,

VATICAN NEWS.

20/01/2018 12:46