2018-01-19 09:00:00

Papa Francisko afungisha ndoa angani wakati akielekea Jimboni Iquique


Mama Kanisa anafundisha kwamba, agano la ndoa ambalo kwa njia yake, mwanaume na mwamke huunda kati yao jumuiya kwa maisha yote, kwa tabia yake ya asili liko kwa ajili manufaa yao na kwa ajili ya kuzaa na kulea watoto. Agano hili kati ya wabatizwa, limeinuliwa na Kristo Bwana kwa hadhi ya Sakramenti. Baba Mtakatifu Francisko katika hija yake kitume nchini Chile, wakati akitoka Jimbo kuu la Santiago kuelekea Jimbo Katoliki la Iquique, nchini Chile, Alhamisi tarehe 18 Januari 2018 ameshuhudia ndoa ya wafanyakazi wawili wa Shirika la Ndege lililokuwa linamsafirisha Baba Mtakatifu pamoja na msafara wake.

Wanandoa hawa wapya ambao ni Paula Podestà Ruiz mwenye umri wa miaka 39 na Carlos Cuffando Elorriaga, mwenye umri wa miaka 41, walilazimika kuahirisha ndoa yao Kanisa kunako mwaka 2010 kutokana na tetemeko kubwa lililoitikisa Chile na kuacha maafa makubwa kwa watu na mali zao na badala yake, wakafunga ndoa ya kiserikali. Baba Mtakatifu ameamua kuwafungisha ndoa baada ya kusikiliza historia ya maisha yao na vikwazo walivyopambana, akamua kuwaunganisha kama Bwana na Bibi katika Sakramenti ya Ndoa, tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya ndoa na familia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.