2018-01-19 06:47:00

Ni kipindi cha toba na wongofu wa ndani na ushuhuda wa imani tendaji


Dhumuni la ujio wa Kristo duniani ni kumkomboa mwanadamu kutoka dhambini na kurudisha uhusiano wake na Mwenyezi Mungu. Tendo hili la upendo linatufafanulia udumifu wa upendo wa Mungu kwetu sisi wanadamu. Baada ya anguko la wazazi wetu wa kwanza Adamu na Eva, Mwenyezi Mungu hakumwacha mwanadamu. Alimtangazia tangu awali kuwa atamwokoa kutoka kwa huyo mwovu kwa kuweka uadui naye (Rej Mw 3:15). Haya yote yanathibitishwa na matendo yake makuu katika historia nzima ya wokovu inayoelezewa katika Maandiko Matakatifu na kuhitimishwa na fumbo la Bwana wetu Yesu Kristo, nafsi ya pili ya Utatu Mtakatifu wa Mungu kutwaa mwili na kukaa kati yetu. Wakati wa kutangazwa kuja kwake haiba yake ya ukombozi ilidadavuliwa kwa uwazi kabisa akitajwa kama Yeye ambaye “atawaokoa watu wake na dhambi zao” (Mt 1:21).

Kristo anapoanza utume wake anaonesha waziwazi hiyo nia yake. “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni na kuiamini Injili”. Ni tangazo la utimilifu wa ukombozi wa mwanadamu katika nafsi yake Kristo ambaye ndiyo hiyo habari njema. Utimilifu wa wakati unafika katika nafsi ya Kristo. Ni habari njema kwani ujio wa Mungu kati ya watu wake unadhihirika, ujio ambao unaaguliwa na Nabii Isaya aliposema: “Wewe uhubiriye Sayuni habari njema… paza sauti yako usiogope; iambie miji ya Yuda, ‘Tazameni Mungu wenu!’ Tazameni, Bwana Mungu atakuja kama shujaa, na mkono wake ndiyo utakaomtwalia” (Is 40:9 – 10). Bila shaka watu wa Sayuni ambao ni uwakilishi wa ubinadamu wote ulisubiria kwa muda mrefu ujio huo wa Mungu katikati ya watu wako, ujio ambao unatimilika katika nafsi ya Kristo kama tulivyomshangilia siku za karibuni wakati wa sherehe za Noeli.

Mwaliko huu unatutaka kufanya toba na kuiamini Injili, yaani kugeuza mienendo yetu na kumsikiliza Yeye aliye utimilifu wa ukombozi wetu. Tangazo la toba na kuwa na imani katika Injili linaonekana kama ni hitajiko muhimu kwa ustawi wa ufalme wa Mungu. Ufalme huu unapokaribia hatuna budi kufanya toba na kuwa na imani katika Injili. Huu ni mwaliko wa kufanya mageuzi katika maisha yetu na kusikiliza kile ambacho tunaelekezwa na Kristo ambaye ndiye Habari njema. Hapa ndipo tunaiona mantiki ya tangazo la Kristo tukiunganisha na makusudi ya utume wake yaani, ukombozi wa Mwanadamu. Kristo aliye utimilifu wa Ukombozi huo anatuambia tangu mwanzoni kwamba hakuna njia nyingine zaidi isipokuwa kugeuza mienendo yetu na kumrudia Mungu. Ni kwa namna hiyo tu tutaukaribisha utawala wa Mungu nafsini mwetu. Hivyo anapoanza utume wake wa hadharani analiweka tangazo hilo la toba kama hitajiko la kwanza na la msingi.

Katika somo la kwanza tunaiona habari ya Yona anayetumwa katika mji wa Ninawi kwa ajili ya kuwapelekea ujumbe wa toba. Ujumbe huu ulitoka kwa Mungu na uliambatana na matokeo ya jinsi Ujumbe huo utakavyopokeleka. Yona alisema: “Baada ya siku arobaini Ninawi utaangamizwa”. Ilikuwa ni Uchaguzi kwao: ama kuzigeuza njia zao na kumwongokea Mungu au kubaki katika njia zao na kuangamizwa. Hapa tunaona kwamba tangazo la toba toka kwa Mungu linabeba sura mbili. Kwanza linaheshimu uhuru wa mwanadamu katika kuamua. Ukombozi wake hautujii kwa kulazimishwa vinginevyo, Mungu atajipinga mwenyewe katika kazi yake ya uumbaji kwani alimuumba mwanadamu katika uhuru wa utashi kamili.

Sura ya pili inaonekana katika kile kitakachotokea kutegemea namna Ujumbe wa Neno la Mungu unavyopokelewa. Pamoja na Uhuru anaompatia mwanadamu, mwenyezi Mungu anaufunua ukamilifu wake. Neno lake kwetu ni maelekezo kuelekea ukamilifu. Yeye ndiye analiyetuumba na anatufahamu kwa namna zote. Upendo wake kwetu ni mkubwa sana na hivyo daima anatuelekeza katika ukamilifu. Pamoja na kwamba ametuacha huru kuchagua lakini Neno lake kwetu ni kutupeleka katika mema. Hekima ya kimungu inapaswa kutuongoza na kuutumia vyema uhuru wetu kusudi kuchagua njia ya Mungu. Ndiyo, sisi tupo huru lakini Neno lake ni kweli tupu na ni katika huo ukweli ndipo tutakuwa huru (Rej. Yoh (8:32). Ni kana kwamba tunashauriwa kuutekeleza uhuru wetu katika msingi wa Mungu ili kutembea katika kweli na kuishi.

Mtume Paulo anatupatia hekima yake katika somo la pili kama nyenzo ya msaada ya kutufikisha katika kuchagua ya Mungu na kujinasua katika mambo ya ulimwengu huu. Yeye anatutaka tusijigandamanishe na mambo ya ulimwengu huu kiasi cha kuacha kuisikia sauti ya Mungu kwani “mambo ya ulimwengu huu yanapita”. Iwe ni mambo ya ndoa, yawe ni mambo ya huzuni au furaha, yote yatapita lakini Neno la Mungu litabaki daima. Hii ni taadhari kwetu ya kutoka katika kujishikamanisha na vionjo na mienendo ya kidunia kiasi cha kushindwa kulisikia tangazo la toba na hivyo kutokuiamini Habari Njema iletwayo na Kristo. Kwa maneno mengine, tunapaswa kuyaona yote katika ulimwengu huu katika mwono wa Mungu. Maisha yetu ya kila siku yaongozwe na Neno lake na si mawazo na vionjo vyetu vya kinadamu.

Leo hii tupo katika jamii yenye changamoto sana. Wazazi katika familia wanatumia nguvu na rasilimali zao nyingi kuwekeza zaidi katika mambo ya kidunia. Viongozi wetu wa kijamii wanatutengenezea taratibu na kutuandalia mazingira yasiyo rafiki na habari ya injili. Haya yote yanatutengenezea ubutu katika maisha yetu ya kiroho na katika hali mbaya zaidi yanatuelekeza kuyatafsiri hata mambo ya kimungu katika muono wa kidunia. Katika muktadha huu tangazo la toba na habari njema ya Kristo linakosa udongo mzuri na hivyo kuonekana kutokuwa na mashiko. Ufalme wa Mungu unapokaribia kati yetu unatutaka kubadilisha mwenendo wetu wa maisha. Tufumbue macho yetu na kuwekeza kwanza kwa Mungu kusudi tuweze kukabiliana na changamoto za kidunia.

Mungu ametupatia ulimwengu huu ili tuutawale na kuuratibisha. Tunapomwondoa Yeye katika ulimwengu na matendo yetu tunamdhulumu na kujidhulumu nafsi zetu sisi wenyewe. Tuutumie vyema ulimwengu huu na kuukaribisha utawala wa Mungu katikati yetu. Kristo ndiyo Injili yetu. Tuusikilize Ujumbe wake kwanza na kwa njia hiyo tuyageuze maisha yetu yarandane na hicho anachotufunulia. Tusali pamoja na mzaburi tukisema: “Ee Bwana, unijulishe njia zako, unifundishe mapito yako, uniongoze katika kweli yako na kunifundisha”.

Mimi  ni Padre Joseph Peter Mosha,

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.