Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Mnaitwa na kutumwa ili kutangaza Habari Njema ya Wokovu!

Mnaitwa na kutumwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayosimikwa katika toba na wongofu wa ndani, kikolezo muhimu cha maisha mapya! - EPA

19/01/2018 07:12

Neno utume linaendana na ufuasi. Kwa maana nyingine, mtume ni mfuasi. Leo tena neno/swala la utume linawekwa mbele yetu. Yaweza kuonekana kuwa nabii Yona hakuwa na bahati katika maisha yake ya utume kama ionekanavyo katika somo la kwanza. Lakini inaonekana wazi kuwa, Mungu ana mpango nasi na akituhitaji, ni lazima atatupata. Licha ya hali yetu ya awali, akitupata, aliyeitwa anakuwa mshindi dhidi ya ulimwengu. Neno la Mungu katika  – 1 Yn. 5:4-5 – latutafakarisha sana katika hili - kwa maana yote yaliyo na asili yake katika Mungu huushinda ulimwengu. Na ushindi ushindao ulimwengu ndiyo imani yetu. Ni nani awezaye kuushinda ulimwengu isipokuwa yeye tu asadikiye ya kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu? Yona alipoitwa hakuijua nguvu hii ya Mungu. Alidhani angeweza kuamua mwenyewe, hata kupingana na wito wa Mungu.

Tunaendelea kuona katika somo hili kwamba Yona anaitwa na kutumwa kwa watu wa Ninawi ili kuongea neno la toba. Ninawi ulikuwa mji mkuu wa Assyria. Yeye hakuwa tayari kufanya hilo. Ikumbukwe kuwa Assyria ilikuwa adui mkubwa wa taifa la Israeli. Kwa mtindo wao wa maisha na uadui wao na taifa la Israeli aliamini fika kuwa wasingekuwa tayari kusikia sauti ya unabii. Aliamini kuwa hana haja ya kupoteza muda wake. Hivyo anatoroka wito wa Mungu. Kilichotokea tumesikia katika somo la kwanza. Mambo yanakuwa kinyume na anajikuta Ninawi. La kushangaza ni kuwa baada ya neno la unabii, neno la toba – watu wote wanakuwa tayari kuongoka.

Ndugu zangu, wongofu ueleweke kama tendo la kuruka au kwenda mbele na kuuingia ufalme, kuchuchumilia wokovu ulioletwa kwa watu kwa mapenzi ya Mungu. Kabla ya Kristo, uongofu ulieleweka kama kuangalia au kurudi nyuma au kuangalia pale mmoja alipopotoka na kubadilika tena na kurudi kuangalia tena sheria zinaelekezaje. Hapa uongofu unachukua hadhi ya kimaadili, kuyatengeneza tena upya maisha yaliyoharibika. Dhana inayotawala hapa ni uongofu kwanza halafu wokovu kama huruma ya Mungu. Wakati wa Kristo ieleweke kuwa hutangulia wokovu kama zawadi ya Mungu kwetu halafu uongofu kama jibu la mtu. Mungu hasubiri kwanza mtu aongoke kama hatua ya kwanza, kubadili maisha yake, kutenda mema halafu ufuate wokovu kama shukrani ya Mungu kwa tendo hilo. Hapana. Neema inatangulia kwanza.

Ni Mungu anatenda kwanza. Na kwa namna hii ukristo unatofautina na dini nyingine zote. Siyo wongofu unaotangulia kwanza kwa maana ya kutenda matendo mema au kushika sheria sana, bali kinachotangulia kwanza ni neema yake Mungu. Ile dhana kuwa wongofu ni kwa ajili ya wapagani au wasioamini inapotea hapa. Hivyo uongofu ni hatua chanya mbele lakini chanzo chake ni neema ya Mungu. Hivyo kuongoka ni kuamini katika wokovu wake Mungu na kwa kuamini basi hupatikana uongofu. Imani ni njia ambayo kwayo mtu huingia mbinguni. Ingesemwa pengine njia ya kuingia mbinguni ni sheria fulani basi mmoja angesema mimi nimeshindwa kushika sheria hii basi nimekosa mbingu. Mlango ni imani. Mungu ametuumba huru na wenye akili ili tendo la kumwamini liwezekane. Mtakatifu Anselm anasema kile ambacho nashindwa kukipata katika imani basi Kristo ananipatia. Tendo la huruma la wokovu wake Mungu kwetu hutangulia uongofu wetu. Ni Mungu anayetualika kwa huruma yake kuongoka na anafurahi kuona mwanadamu anajibu kwa kumgeukia yeye. Mtakatifu Agustino wa Hippo anaandika wazi – tumeumbwa kwa mapenzi yake Mungu ila kupata wokovu ni juhudi binafsi. Maana yake ni kuwa, kila mmoja wetu anapaswa kushiriki kikamilifu katika mpango wa Mungu wa ukombozi.

Mwanamuziki maarufu – mwitaliano – Paganini – alipiga muziki kwa miaka mingi. Siku moja wakati wa mapumziko akagundua kuwa hakutumia gitaa lake ambalo hutumia kila siku na kumpatia umaarufu. Akaghadhabika sana kiasi cha kutokuwa tayari kuendelea na kipindi cha pili. Msaidizi wake alitumia nguvu ya ziada kumshawishi kuwa muziki umepigwa kama kawaida na watu wamefurahi mno. Basi kwa moyo mzito akarudi kuendelea kutumbuiza. Ila huku akiendelea kutumbuiza, alikuwa akishangaa jinsi watu walivyokuwa wanamshangilia na kufurahi. Ni toka hapo alipogundua kuwa muziki wa kweli hutoka moyoni. Chombo cha muziki ni zana inayosaidia tu. Muziki wa kweli hutoka moyoni. 

Katika somo la Injili – twaona utume wa kwanza wa hadhara wa Yesu huko Galilaya na tangazo la uwepo wa ufalme wa Mungu. Sawa na somo la kwanza, lipo tamko la toba/uongofu na imani. Katika geuko hilo, upo wito wa wafuasi wa kwanza wa Yesu. Licha ya hali yao ya kawaida, Yesu anawachagua. Ni muhimu sana hapa. Wanaacha mtindo wao wa maisha, wanakuwa wafuasi. Neema ya Mungu inafanya kazi. Somo la pili – linatupatia mwelekeo wa kile tunachotakiwa kuwa. Tutumie yote tuliyonayo na vizuri ili kumpata Kristo. Yona alionekana katika hali yake. Akaitwa na kutumwa na Mungu kama alivyokuwa. Wafuasi wa kwanza walionekana katika hali yao. Yesu akawaita. Wakaacha yote wakamfuata. Huu ndio utume au ufuasi wa kweli.

Tujaribu kuangalia nafasi yetu leo katika utume au ufuasi kama tulivyoitwa na Mungu. Tukumbuke kuwa kwa ubatizo wetu sisi sote tumeitwa kuwa mitume au wafuasi wake Bwana. Sisi sote ni wamisionari. Tutafakari katika baadhi ya changamoto zilizo mbele yetu na kuona namna ambavyo tunaitwa kutumikia; Woga ulipo katika kila mmoja wetu wa kufanya badiliko la hali ya maisha, msimamo au mitizamo binafsi  sisi tunapanga, Mungu anapangua. Tumeona jinsi Mungu anavyoita na kutuma – Yona, kina Petro. Mara ngapi tumepinga mpango wa Mungu? Wengi wetu tunaliita sana jina la Mungu na tunampenda sana Mungu. Lakini tukitakiwa kufanya kazi maalumu ya Mungu, tunasita sana na hata kukataa. Tuangalie wengi wetu tunavyokwepa uongozi katika ngazi mbalimbali za kanisa kama uongozi katika ngazi ya walei. Bado kina Yona wengi wapo kati yetu.

Ni kwa kiasi gani tunahitajika au tumehitajika na hasa pale penye shida lakini hatukufanya au hatukuwa tayari kwenda au tumekwenda kwa shingo upande? Mara ngapi tumetupia kisogo matatizo ya wengine ambapo yalihitaji waziwazi msaada wetu? Inapotokea padre au mmisionari anakataa kwenda kufanya utume sehemu au maeneo fulani kwa sababu ni sehemu maskini au watu ni maskini au pengine tunasema wale watu ni wagumu. Ninawi yetu ni wapi au kitu gani leo? – mahali gani au kitu gani katika mazingira yetu ya leo? Kwa Wayahudi wa karne ya kwanza – Ninawi ulikuwa ni mji usiomjali Mungu, umejaa dhambi na dhuluma. Ulifanya madhara makubwa kwa taifa la Israeli, ikiwa hata kuharibu hekalu la Yerusalemu. Hawakuwa na hofu ya Mungu. Hivyo kwa mcha Mungu kama Yona na Myahudi, Ninawi ulikuwa mbali na Neno la Mungu. Dhambi ilitawala na nia ya kubadilika haikuwepo. Hivyo kwenda Ninawi ilikuwa ni kupoteza muda.  Baba Mtakatifu Francisko katika fundisho lake analialika Kanisa na wakristo kutoka katika mazoea yao na kupeleka habari njema pembezoni au pasipo na matumaini – angalia Injili ya Furaha. Angalia alichofanya Yona pale Ninawi. Watu walisikia neno na wakafanya toba. Unaonaje ndugu yangu kama leo ukiamua kufanya kitu ili kuokoa hali isiyoridhisha katika mazingira yetu kiimani, kimaadili, kiuchumi, kisiasa na kijamii?

Tumsifu Yesu Kristo,

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.

19/01/2018 07:12