2018-01-18 15:15:00

Papa: Tangazeni Injili ya furaha kwa kudumisha haki msingi za binadamu


Habari Njema ya Wokovu ni chemchemi ya furaha vizazi baada ya vizazi na kwamba, Wakristo nao wamerithi furaha ya Injili, changamoto na mwaliko kwa waamini kumwilisha imani kwa Kristo na Kanisa lake. Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Chile imemwezesha kutembelea na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Mlima Carmeli, Alhamisi tarehe 18 Januari 2018 na hatimaye, kusali kwa ajili ya kuwaombea watu wa Mungu nchini Chile. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake anasema, yuko kati yako ili kushiriki imani yao na maisha yao ya kiroho yanayowashirikisha na kuwaambata watu wote kijijini.

Waamini wana uwezo wa kusherehekea  ukuu wa Mungu kwa kuimba na kucheza kama njia ya kutambua uwepo na upendo wake wa daima unaowapyaisha kutoka katika undani wa maisha yao na kuwakirimia uvumilivu hata wa kuweza kuubeba Msalaba katika maisha ya kila siku na kwamba, amani itakuwa ni kazi ya haki na jangwa litakuwa ni shamba lizaalo sana. Sehemu hii ya ardhi ni jangwa kubwa kuliko sehemu nyingine yoyote ya dunia, lakini imevikwa kwa shamrashamra za Siku kuu kwa heshima ya Bikira Maria, ili furaha hii iweze kudumu daima. Bikira Maria kama: Mama mwema anayeangalia yote kwa jicho la huduma, kiasi hata cha kumshirikisha Mwanaye Mpendwa, kwa kusema, “Hawana divai”. Huyu ndiye Bikira Maria anayeguswa na shida na mahangaiko ya watoto wake hata yale yanayoonekana kuweka “kiwingu moyoni” mwao na kuwaamuru kutenda yale atakayosemwa na Kristo Yesu! Arusi ya Kana ukawa ni mlango wa miujiza ya Yesu inayowashirikisha rafiki zake kwani ujio wa Kristo unalenga kutekeleza mapenzi ya Baba yake wa mbinguni na waamini wote ni sehemu hai ya Fumbo la mwili wake, yaani Kanisa, kumbe, kila mwamini anasukumwa kutenda muujiza kwa ajili ya jirani yake.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Iquique ni nchi ya ndoto ambayo imetoa hifadhi kwa watu na tamaduni mbali mbali, waliokuwa na matumaini ya kupata maisha bora zaidi! Ni watu ambao wamebeba ndani mwao: hofu na mashaka ya mambo yanayoweza kuwapata. Iquique ni ukanda wa wahamiaji unaowakumbusha watu umuhimu wa kushirikiana ili kuendeleza maisha badala ya kujikita katika kinzani na mipasuko isiyokuwa na tija wala mashiko! Wahamiaji hawa ni watu ambao wanaishi kwa shida sana kama ilivyokuwa kwa Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.

Baba Mtakatifu anawataka wananchi wa Iquique kuwa ni mashuhuda wa furaha ya Kikristo na ukarimu, kwa kuwafungulia malango ya maisha yao na isiwe kama ilivyotokea kwa Maria na Yosefu ambao hawakupata nafasi. Waamini wawe na jicho la huruma na mapendo kwa watu wasiokuwa na uwezo wa kusherehekea; wawe wasikivu kwa kilio na mahangaiko ya watu wa Mungu; wasimame kidete kupambanana na ukosefu wa haki msingi za binadamu na utumwa mamboleo kiasi cha kuwafanya watu hawa kupoteza hamu ya Siku kuu. Wawe makini kuwasaidia watu wasiokuwa na fursa za ajira ambao wanashindwa kutekeleza dhamana na wajibu kwa familia zao na matokeo yake, Injili ya maisha inawekwa rehani. Wawe makini kusimama na kutetea haki msingi za wakimbizi na wahamiaji ili wasitumbukie katika mikono na mitego ya wajanja wachache katika jamii.

Waamini wawe makini kuzisaidia familia zisizokuwa na makazi, ardhi na ajira, ili kwa pamoja waweze kuthubutu kama Maria kumwambia Kristo Yesu, “Hawana Divai”. Waamini wawe tayari kuwasaidia jirani zao kama kielelezo cha mshikamano na dhamana yao katika kutetea haki. Wawe na ujasiri wa kujifunza kutoka kwao: kuhusu tunu msingi za maisha ya kiroho, historia, hekima na imani ambayo wakimbizi na wahamiaji wanabeba ndani mwao kama amana na hazina ya maisha yao. Wenyeji wawe na ujasiri wa kupokea yale mema yanayotolewa na wakimbizi pamoja na wahamiaji na baadaye, kumwachia Kristo Yesu, kukamilisha muujiza, kwa chapa ya uwepo wake wa daima katika Jumuiya na nyoyo za waamini, chemchemi ya furaha ya Injili, kwani Mungu yuko pamoja nao na amepewa hifadhi kati yao. Huu ni mwaliko wa kuwatangazia wote Habari Njema bila kumtenga mtu awaye yote! Bikira Maria anayeheshimiwa sana kwenye eneo hili aendelee kumwambia Kristo Yesu, kwamba, “Hawana Divai”, tayari pia kumwilisha maneno ya Yesu katika uhalisia wa maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.