2018-01-17 12:00:00

Papa: Maaskofu jikiteni zaidi katika malezi, maisha, utume na sinodi


Baba Mtakatifu Francisko baada ya kukutana na kuzungumza na wakleri, watawa pamoja na majandokasisi, Jumanne, tarehe 16 Januari 2018 alipata nafasi tena ya kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Chile, kwenye Kanisa kuu la Jimbo kuu la Santiago, Chile, wakati wa hija yake ya kitume nchini humo! Katika hotuba yake kwa Maaskofu Katoliki nchini Chile, Baba Mtakatifu amewataka kutambua kwamba wao ni watu! Ametumia fursa hii kumshukuru na kumpongeza Askofu Bernardino Pinera Carvallo anayesherehekea kumbu kumbu ya miaka 60 tangu alipowekwa wakfu kuwa Askofu. Yeye ni Askofu mzee sana kuliko Maaskofu wote duniani, ambaye alibahatika kuhudhuria vikao vyote vya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, kumbu kumbu hai ya tukio hili muhimu katika maisha na utume wa Kanisa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Chile linajiandaa kwa ajili ya Hija ya Kitume, inayofanywa na Maaskofu mjini Vatican, walau kila baada ya miaka mitano, lakini, Baba Mtakatifu Francisko amependa kutumia fursa hii kukutana nao, baada ya kukutana na kuzungumza na wakleri, watawa na majandokasisi, kama ushuhuda wa uwepo wa karibu wa Maaskofu kwa mapadre na watawa wao! Wachungaji wanapaswa kuwa imara na thabiti katika maisha na utume wao, ili kuwachunga Kondoo wao, vinginevyo, hata Kondoo wanaweza kujikuta wamepoteza dira na mwelekeo wa maisha na huko wanaweza kumezwa na malimwengu!

Ubaba wa Maaskofu kwa mapadre wao ni zawadi ambayo Maaskofu wanapaswa kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia, ili waweze kuwa karibu na mapadre wao kwa mtindo na mfumo wa maisha ya Mtakatifu Yosefu, ili kuwasaidia mapadre: kukua na kukomaa; kutambua na kuendeleza karama ambazo wamekirimiwa na Roho Mtakatifu kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa Maaskofu kujisikia na kujitambua kuwa ni sehemu ya watu wa Chile, ili kuweza kukabiliana na matatizo, changamoto na fursa zinazojitokeza kwa familia ya Mungu nchini Chile. Maaskofu watambue kwamba, wao pia ni sehemu ya familia takatifu ya Mungu na kwamba, Kanisa si mali binafsi ya maaskofu, mapadre na watawa.

Kwa njia hii, Maaskofu wataweza kutekeleza dhamana na wajibu wao kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Maaskofu wameitwa na kuwekwa wakfu: kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu, kumbe, kwao uongozi ni huduma! Maaskofu watambue kwamba, utume ni wajibu wa Kanisa zima na wala waamini walei si wafanyakazi wa wakleri!  Ukuhani wa waamini wote ni jambo ambalo linapaswa kupewa msukumo wa pekee tangu katika hatua za malezi ya awali na endelevu ili kuwawezesha mapadre kuwa ni wahudumu wa watu wa Mungu. Padre ni mhudumu wa Kristo anayemwakilisha Yesu kati ya watu Mungu. Mapadre wa kesho hawana budi kufundwa barabara, ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali wanazoweza kukumbana nazo katika hali halisi ya ulimwengu na wala si katika mambo ya kufikirika. Malezi haya yajikite katika mchakato wa ujenzi wa udugu na watu wa Mungu, ili kuwasaidia waamini walei kupata mang’amuzi katika maisha na utume wa pamoja na kukuza dhana ya sinodi; mambo msingi kwa mapadre wa baadaye, ili kugusa hali halisi ya maisha ya watu. 

Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu kujikita katika ujenzi wa ndoto ya kimissionari na utume unaoweza kusaidia kuleta mchakato wa mageuzi katika mtindo wa maisha, ratiba ya huduma, lugha inayotumika na kwamba, miundo mbinu ya Kanisa inatumike kuwa kweli ni nyenzo ya uinjilishaji wa familia ya Mungu nchini Chile, huku ikijitambua kwamba, ni sehemu muhimu sana ya Kanisa. Maaskofu wawe na ujasiri wa kuvua na kutupilia mbali mambo yote yale yanayokwamisha ari, moyo na utume wa kimissionari. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko amewaweka wakleri wote nchini Chile chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Chile, akawataka Maaskofu kusali na kuwaombea mapadre, watawa na watu wa Mungu katika ujumla wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.