2018-01-17 14:48:00

Papa Francisko: Jengeni utamaduni wa umoja, upatanisho na kusikilizana


Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa hija yake ya kitume nchini Chile, Jumatano, tarehe 17 Januari 2018 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya maendeleo ya watu kwenye Uwanja wa Ndege wa Maquehue huko Temuco kwa kukazia upatanisho na Mwenyezi Mungu, umoja na mshikamano kati ya watu. Ametembelea nyumba ya “Madre de la Santa Cruz”, yaani “Nyumba ya Mama wa Msalaba” inayomilikiwa na kuendeshwa na Shirika la Msalaba Mtakatifu lililoanzishwa kunako mwaka 1844 huko Uswiss. Baadaye, Baba Mtakatifu amepata chakula cha mchana na wawakilishi wa watu Mahalia nyumbani hapa, tukio la kihistoria, kielelezo cha mshikamano wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na watu mahalia kama sehemu ya mchakato wa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki zao msingi kama binadamu!

Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Ibada ya Misa Takatifu, amekazia umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; umoja na mshikamano unaojikita katika tofauti msingi; upatanisho na amani ya kudumu miongoni mwa wananchi wa Chile katika ujumla wao! Baba Mtakatifu amemshukuru Mwenyezi Mungu kwa utajiri na rasilimali unaofumbatwa katika eneo hili la Chile, chemchemi ya upendo wa vizazi na vizazi nchini Chile. Baba Mtakatifu ametambua uwepo wa watu mahalia katika Ibada hii ya Misa Takatifu na kuwataka watu kuguswa na mateso, dhuluma na nyanyaso ambazo watu hawa wamekumbana nazo katika safari yao ya maisha.

Papa amesema, Ibada ya Misa Takatifu ni alama ya shukrani na masikitiko makubwa kutokana na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu. Kumbe, Ibada ya Misa Takatifu ni kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea wale wote waliosadaka maisha yao kwa ajili ya kutetea haki msingi za binadamu; bila kuwasahau wale wote wanaoendelea kuteseka ili waweze kutambua kwamba, Kristo Yesu, kwa njia ya sadaka yake Msalabani, amebeba mateso na mahangaiko ya waja wake! Kristo katika ile Sala yake ya Kikuhani, aliwaombea mitume wake ili wote wawe wamoja, ili kushinda kishawishi cha kinzani na mapambano ambayo yamesababisha machozi ya watu wengi sana kumwagika! Ibada hii ya Misa Takatifu iwe ni ushuhuda unaounganisha mateso na mahangaiko ya watu mahalia, ili hatimaye, kuweza kumtolea Kristo Yesu, ili wote wawe wamoja kwa kushinda kishawishi cha mapambano na kinzani. Umoja ambayo Yesu aliwaombea wafuasi wake ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wote wa Mungu, ili kusiwepo tena na mambo yanayochafua na kuharibu zawadi ya Mungu kwa mwanadamu, ili kila mwananchi aweze kuwa ni mdau na mshiriki katika ujenzi wa historia ya nchi yake

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kuna tofauti kubwa kati ya umoja na usawa. Umoja unatambua na kuthamini tofauti msingi zilizopo; ni mchakato wa amani na utulivu kati ya watu pasi na shuruti kiasi hata cha watu kushirikishana hekima. Umoja si matokeo ya matumizi ya mabavu na nguvu, bali ni mwaliko kwa kila kabila, tamaduni na jamaa kushirikisha katika ardhi hii iliyobarikiwa na kuondokana na kiburi cha baadhi ya watu kudhani kwamba, wao ni bora zaidi kuliko wengine; kila jambo lipewe umuhimu kwa wakati wake. Mchakato wa umoja unawataka wadau wote kweka uwiano bora katika ujenzi wa vijiji, barabara na mahali pa mapumziko na watu kukutania. Hii ni sanaa inayofumbatwa katika utamaduni wa kusikiliza na kuthamini changamoto zinazoweza kujitokeza kwa siku za usoni!

Utamaduni wa kusikiliza unafumbatwa katika zawadi ya amani inayowaelekeza watu katika mshikamano kama njia ya kumwilisha umoja ili kujenga historia; kwa kutegemeana na kukamilishana katika kudumisha msitu wa matumaini, ndiyo maana, waamini wanasali ili kuombea umoja! Baba Mtakatifu anakaza kusema, umoja huu unajikita katika upatanisho unaotekelezeka katika vipaumbele vya maisha ya watu, kinyume kabisa cha ghasia zinazoharibu matumaini. Utamaduni wa kuthaminiana unafumbatwa katika haki na amani dhidi ya ghasia na kinzani zinazotishia usalama na maisha ya watu. Ghasia mara nyingi huchochea ghasia, kinzani na utengano. Kumbe, kuna haja ya kukataa katu katu ghasia zinazosababisha uharibifu. Wananchi wawe na ujasiri wa kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa siasa ya amani; majadiliano yatakatodumisha umoja na kwamba, wote wanahamasishwa kuwa ni vyombo na wajenzi wa umoja, kwa kuishi vyema! Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wananchi mahalia kumwomba Mwenyezi Mungu ili awawezeshe kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa umoja!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.