2018-01-17 06:00:00

Papa Francisko asema, hata wafungwa bado wanayo ndoto ya matumaini!


Baba Mtakatifu Francisko akiwa nchini Chile, Jumanne, tarehe 16 Januari 2018 amepata nafasi ya kutembelea Gereza la Wanawake la Santiago linalojulikana kama “Gereza la “San Joaquin” lililoanzishwa kunako mwaka 1864 na Mwaka 1996 likakabidhiwa kuendeshwa na Shirika la Masista wa Kristo Mchungaji Mwema. Hili ni gereza ambamo kuna wafungwa wagonjwa, waathirika na wafanyabiashara ya dawa za kulevya. Gereza hili lina uwezo wa kupokea wafungwa 855. Amesikiliza shuhuda kutoka kwa  viongozi wa gereza na wafungwa gerezani hapo walioshuhudia Injili ya maisha dhidi ya utamaduni wa kifo; unyenyekevu na ushupavu wa kuomba msamaha kutokana na makosa waliyotenda!

Katika hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amekazia kuhusu mambo makuu matatu: Mama, Watoto na Maua! Baba Mtakatifu anasema, kuomba msamaha ni tendo la kiutu na utambuzi kwamba kila siku binadamu anaitwa kuanza upya, kwani wote wametenda dhambi na wametindikiwa na neema ya Mungu. Huu ni unyenyekevu unaomwonesha mwanadamu udhaifu na uwezo wa kutenda dhambi, tayari kupiga moyo konde na kusonga mbele. Hapa hakuna mantiki ya mtenda haki na mdhambi! Baba Mtakatifu amewapongeza akina Mama wafungwa ambao wameweza kuchukua mimba na hatimaye, kuzaa watoto wao, kwa kutambua kwamba, umama wao ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, changamoto ya kuendelea kuwalea, kuwatunza na kuwajengea leo na kesho iliyo bora zaidi, kwani kimsingi watoto ni zawadi ya jamii nzima na kamwe wasikate tamaa na kupoteza Injili ya matumaini katika maisha yao! Katika mazingira ya gerezani humo watambue kwamba bado wanayo ndoto na matumaini ya kufanya toba na wongofu wa ndani, ili kubadilika na hatimaye, kuwa watu wema zaidi, mapambano haya yatazaa matunda kwa wakati wake!

Baba Mtakatifu anasema, watoto ni nguvu na matumaini ya kusonga mbele ili kujenga leo na kesho iliyo bora zaidi, bila ya kukatishwa tamaa na wale wote wanaowatazama kwa “jicho la kengeza” kama ilivyokuwa kwa yule Mkuu wa Sinagogi, lakini kutokana na imani yake kwa Kristo Yesu, mtoto wake aliweza kufufuliwa, kwani alimruhusu Yesu kuingia katika maisha yake na kumsaidia kusimama tena. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza Wakristo wanaofuata nyayo za Yesu kwa kuwasaidia jirani zao kuweza kusimama tena! Gereza liwe ni mahali pa kujenga matumaini ya kesho iliyo bora zaidi. Vyombo vya ulinzi na  usalama wa raia visaidie kuzuia uhalifu, vitoe nafasi za kazi, elimu na maisha ya kijumuiya.

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, maisha yataendelea kuchanua kama mtende wa Lebanon na kutoa harufu nzuri ya manukato ya maisha mapya; kwa kushirikiana bega kwa bega katika kazi. Baba Mtakatifu amewashukuru na kuwapongeza Askari Magereza na familia zao na kwamba, anawaombea. Ni matumaini yake kuwa, Serikali itaweza kuwajengea mazingira bora zaidi ya kazi kwa kuzingatia utu unaodumisha utu na heshima ya binadamu. Bikira Maria, Mama wa wote awaombee na kuwafunika kwa joho lake la kimama, ndugu, jamaa na marafiki zao! Baba Mtakatifu anawaomba waendelee kumsindikiza kwa sala katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.