2018-01-16 15:07:00

Papa Francisko awataka viongozi nchini Chile kusikiliza kilio cha watu


Baba Mtakatifu Francisko amewasili nchini Chile Jumatatu usiku, tarehe 15 Januari 2018 na kupokewa kwa heshima ya kitaifa na viongozi wa Serikali na Kanisa chini ya Rais Michelle Bachelet Jeria wa Chile na baada ya nyimbo za mataifa haya mawili kupigwa, kukagua gwaride la heshima na hatimaye, kutambulishana viongozi muhimu wa pande hizi mbili, Baba Mtakatifu aliondoka na kuelekea kwenye Makao makuu ya Ubalozi wa Vatican nchini Chile. Akiwa njiani, Baba Mtakatifu amesimama kwa kitambo kidogo kwenye Parokia “San Luis Beltràn” ili kutoa heshima yake kwa Askofu Enrique Alvear Urrutia, aliyefahamika sana kama “Askofu wa maskini”.

Baba Mtakatifu Francisko ameianza Siku ya Jumanne, 16 Januari 2018 kwa kukutana na kuzungumza na viongozi wa Serikali, wanadiplomasia na viongozi wa vyama vya kiraia na kuwashukuru kwa makaribisho makubwa yanayojikita katika tunu msingi za maisha ya watu wa Chile ambayo kimsingi ni utenzi wa sifa kwa ardhi ambayo ni amana, changamoto na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi kwa wananchi wote wa Chile. Tofauti zao msingi za kikabila, kitamaduni na kihistoria ni utajiri mkubwa wa tamaduni mbali mbali zinazowaunganisha pamoja.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kumpongeza Rais Sebastian Pinera Echenique aliyechaguliwa hivi karibuni, ili kuongoza Chile katika kipindi cha miaka mine kuanzia sasa! Huu ni ushuhuda wa ukomavu wa kisiasa na kidemokrasia wakati huu, Chile inapoadhimisha Jubilei ya Miaka 200 tangu ilipojipatia uhuru wake. Huu ukawa ni mwanzo wa uhuru na haki na mwaliko wa kupambana na changamoto mbali mbali zilizojitokeza katika historia kwa kubeba machungu ambayo yanapaswa kutazamwa na hatimaye, kusonga mbele ili kuimarisha ndoto ya waasisi wa taifa la Chile.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, wananchi wote wanao wajibu wa kujenga na kuendeleza nchi yao, ili iweze kukua na kuzaa matunda yanayofumbatwa katika: heshima, moyo wa shukrani na utekelezaji wa wajibu na dhamana unaowapatia jeuri ya kujisifia kama taifa na dhamana ya kutekeleza kama raia! Baba Mtakatifu anawaalika wananchi wa Chile kujikita katika mchakato wa kukuza na kudumisha misingi ya: upendo, haki na mshikamano ili kukabiliana na ukosefu wa haki ndani ya jamii. Changamoto kubwa kwa wakati huu, ni kuendeleza ujenzi wa demokrasia ili iweze kuwa ni fursa ya kuwakutanisha wananchi wote katika mchakato wa ujenzi wa nyumba ya wote, familia na taifa katika ujumla wake. Familia ya Mungu nchini Chile iendelee kujipambanua kwa ukarimu, kwa kupenda historia na utulivu; familia yenye matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi, dhamana inayopaswa kutekelezwa kwa ari na moyo mkuu kama anavyokazia Mtakatifu Alberto Hurtado.

Baba Mtakatifu amekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikilizana nchini Chile yenye utajiri mkubwa wa makabila, tamaduni na historia inayopaswa kulindwa na kudumishwa, kwa ajili ya mafao ya wengi. Kuna haja ya kuwasikiliza watu wasiokuwa na fursa za ajira wasioweza kutekeleza wajibu kwa familia zao; watu mahalia ambao mara nyingi wanasahauliwa, wananyimwa haki zao msingi, ili utamaduni wao uweze kulindwa na kudumishwa kwani ni sehemu ya utajiri wa taifa! Wajenge utamaduni wa kuwasikiliza wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta maisha bora kwa watu wengi zaidi; wasikilize matamanio halali ya vijana hasa katika masuala ya elimu ili kweli waweze kujisikia kuwa ni wadau katika ujenzi wa Chile tayari kupambana na matumizi haramu ya dawa za kulevya.

Wazee na watoto wasikilizwe na hapa Baba Mtakatifu anasikitishwa sana na kashfa za viongozi wa Kanisa dhidi ya watoto wadogo na ametumia fursa hii kuungana na Maaskofu Katoliki Chile kuomba msamaha na kuendelea kujizatiti ili vitendo hivi visijirudie tena. Ni mwaliko wa kusikiliza na kujikita zaidi katika utunzaji bora wa mazingira ili kukabiliana na changamoto za uchafuzi wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi, kwa kufanya mageuzi katika sera, siasa, elimu, mtindo a maisha pamoja na kutafuta teknolojia rafiki itakayolinda mafao ya wengi. Mwishoni mwa  hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko anasema, busara ya wenyeji idumishwe katika kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote na hivyo kuachana na tabia ya ulaji wa kupindukia! Wananchi wa Chile wanao wito wa uwepo na utashi wa kuishi, kwani ni utamaduni wa kushirikishana na kutegemeana kama sehemu ya mchakato wa kulinda Injili ya uhai.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.