2018-01-16 08:50:00

Mwanga wa Injili ya matumaini katika kukabiliana na changamoto Perù


Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kutembelea Perù kuanzia tarehe 19-22 Januari 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Umoja wa Matumaini”. Baba Mtakatifu anatembelea Perù ikiwa bado kwenye mtikisiko na mpasuko mkubwa wa kijamii kutokana na: rushwa, ufisadi na uvunjifu wa haki msingi za binadamu hali ambayo imepelekea mafungamano ya kijamii na kisiasa kuyumba kwa kiasi kikubwa. Ndiyo maana hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Perù inafumbatwa katika umoja na matumaini, ili kuweza kupambana kikamilifu na madonda ya kijamii kama vile rushwa, ufisadi na uvunjifu wa haki msingi za binadamu. Ni mwaliko wa kujenga tena utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu Francisko anatembelea Perù baada ya Mtakatifu Yohane Paulo II kutembelea nchini humo mara bili, yaani kati ya mwaka 1985 na Mwaka 1988 kama sehemu ya maadhimisho ya Kongamano la Ekaristi Takatifu Kitaifa na Kongamano la Bikira Maria lililokuwa linaadhimishwa nchini Bolivia. Mtakatifu Yohane Paulo II alikazia utamaduni wa amani, usawa na ujirani mwema, leo hii kuna haja ya kuongeza tena amani na kukazia usawa kama kikolezo muhimu cha mafungamano ya kijamii na umoja wa kitaifa! Akizungumza na vijana wa kizazi kipya, Mtakatifu Yohane Paulo II alikazia sana kuhusu “Heri za Mlimani” kama muhtasari wa Mafundisho Makuu ya Yesu, chachu ya matumaini mapya kwa familia ya Mungu nchini Perù.

Askofu mkuu Salvador Pineiro Garcia-Calderon, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Perù anasema hija ya kitume ya Baba Mtakatifu nchini humo inalenga pia kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano, tayari familia ya Mungu nchini Perù kujipyaisha tena kwa kujikita katika tunu msingi za maisha ya kiinjili, kiutu na kitamaduni. Baba Mtakatifu anataka kuwatangazia Injili ya furaha na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake ili kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya familia inayofumbatwa katika maisha dhidi ya utamaduni wa kifo! Perù inapaswa kukazia zaidi umoja wa matumaini katika upendo na mambo matakatifu hususan Ibada kwa Bikira Maria na heshima kwa watakatifu ambao ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu.

Askofu mkuu Salvador Pineiro Garcia-Calderon anasikitika kusema, rushwa na ufisadi ni janga la Amerika ya Kusini, hali ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa mipasuko ya kijamii na kisiasa; pengo kubwa kati ya matajiri na maskini; mambo yanayohitaji mchakato wa upatanisho, haki na amani. Biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni janga kubwa linalowatumbukiza vijana wengi katika biashara ya utumwa mamboleo na madhara yake yanajionesha katika utu na heshima ya binadamu. Baraza la Maaskofu Katoliki Perù linapenda kujikita katika Mafundisho Jamii ya Kanisa kama kikolezo cha mageuzi ya kisiasa na kijamii; kwa kukazia: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza! Ikumbukwe kwamba, utajiri mkubwa wa familia ya Mungu nchini Perù ni umati wa watakatifu wake anasema Askofu Antonio Santarsiero wa Jimbo Katoliki Huacho, nchini Perù. Watakatifu ni amana na utajiri mkubwa wa maisha na utume wa Kanisa; ni chachu ya upendo na huduma makini kwa jirani kama kielelezo cha imani tendaji inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Ni mwaliko wa kuondokana na ubaguzi wa rangi na maamuzi mbele kwa kutambua kwamba, kila binadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Askofu mkuu Nicola Girasoli, Balozi wa Vatican nchini Perù anasema, Baba Mtakatifu Francisko ni hujaji na mjumbe wa umoja na matumaini yanayopania kuganga na kuponya cheche za mipasuko na misigano ya kijamii, kisiasa na kiuchumi, ili kweli rasilimali na utajiri wa nchi ya Perù viweze kuwa ni kwa ajili ya ustawi, mafao na maendeleo ya wengi, daima maskini wakipewa kipaumbele cha kwanza. Ujenzi wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia ni changamoto nyingine inayowakabili waamini nchini Perù. Hii inatokana na kipigo kikubwa wanachopata wanawake na wasichana majumbani. Ibada kwa Bikira Maria na heshima kwa watakatifu ni chachu ya umoja na mshikamano wa kitaifa!

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko huko Amerika ya Kusini, itasaidia kwa kiasi kikubwa maboresho ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Chile na Perù, lengo ni kujenga madaraja ya kukutana na watu kwa ni hija hii kwa hakika ni neema ya Mungu kwa wananchi wa Perù. Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni changamoto pevu, endelevu na changamani kwa Jumuiya ya Kimataifa, ili kulinda utu na heshima ya binadamu. Athari za mabadiliko ya tabianchi ni matokeo ya uharibifu wa mazingira duniani. Nchini Perù bado watu wengi wameathirika kutokana na mvua za “El Nino Costero”! Hawa ni watu wanaohitaji faraja na huruma inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake!

Kardinali Juan Luis Cipriani Thorne, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Lima anasema, uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko nchini Perù ni alama ya furaha na matumaini yanayofumbatwa katika Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na watakatifu, ambao kweli wamekuwa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu huko Amerika ya Kusini. Ni changamoto ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; utu, heshima ya binadamu na haki zake msingi hasa kwa wananchi wanaoishi kwenye misitu ya Amazzonia. Hii ndiyo sababu msingi iliyomsukuma Baba Mtakatifu Francisko kuitisha Sinodi ya Maaskofu wa Amazzonia, itakayoadhimishwa kunako mwaka 2019.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.