2018-01-15 13:43:00

Ratiba elekezi ya hija ya kitume ya Papa Francisko nchini Perù, 2018


Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kutembelea Perù kuanzia tarehe 19     Januari 2018 hadi tarehe 22 Januari 2018 atakaporejea tena mjini Vatican kuendelea na maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hija hii nchini Perù inaongozwa na kauli mbiu “Umoja wa matumaini” na kiini chake ni pale ambapo Baba Mtakatifu Francisko atakapokutana na kuzungumza na wawakilishi wa wananchi wa Amazzonia ili kuwatangazia Injili ya matumaini inayosimikwa katika: utu, haki msingi za binadamu sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Mkutano huu utafanyika kwenye Uwanja wa Puerto Maldonado, Ijumaa tarehe 19 Januari 2018.

Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican anafafanua kwamba, mkutano huu ni utangulizi wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu wa Amazzonia, itakayoadhimishwa mwaka 2019 hapa mjini Vatican. Lengo ni kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji na uinjilishaji wa kina kwa watu mahalia. Uharibifu wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi ni kati ya mambo yanayotishia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu anatarajiwa pia kutembelea nyumba ya watoto yatima, atatembelea Kikanisa cha Kambi ya Jeshi, kumtembelea Rais na baadaye, atafanya mkutano wa faragha na Wayesuiti kwenye Kanisa la “San Pedro”, Jimbo kuu la Lima.

Ratiba elekezi inaonesha kwamba, Jumamosi, tarehe 20 Januari 2018 atatembelea mji wa Trujillo ambako ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu; atatembelea Kanisa kuu na baadaye atakutana na kuzungumza na mapadre, watawa na majandokasisi kutoka Perù kwenye Seminari kuu ya Watakatifu “Carlos y Marcello”. Baadaye ataadhimisha Ibada kwa Bikira Maria na hatimatye kurejea tena mjini Lima. Jumapili tarehe 21 Januari 2018 Baba Mtakatifu atainza siku kwa kusali na watawa wa ndani kwenye Madhabahu ya Bwana wa Miujiza “Senor de los Milaros”, atakutana na Maaskofu Katoliki nchini Perù, atasali Sala ya Malaika wa Bwana na baadaye, Baba Mtakatifu Francisko pamoja na msafara wake watapata chakula cha mchana na Maaskofu Katoliki nchini Perù na baadaye jioni, kuagana na wenyeji wake, tayari kuanza safari ya kurejea mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 22 Januari 2018 ambako anatarajiwa kuwasili majira ya mchana!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.