2018-01-15 08:12:00

Majadiliano, uwajibikaji na huruma kwa ajili ya haki nchini Chile!


Baraza la Maaskofu Katoliki Chile linasema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei kuu ya huruma ya Mungu imekuwa ni fursa kwa waamini kutafakari na kumwilisha huruma ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao! Hii ni changamoto endelevu katika maisha na utume wa Kanisa inayopaswa kumwilishwa katika sera na mikakati ya shughuli za kitume na kichungaji nchini humo. Uso wa huruma ya Mungu unajionesha kwa namna ya pekee kwa njia ya Kristo Yesu, chemchemi ya huruma ya Mungu kwa binadamu. Hii ni sehemu ya tamko lililotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Chile baada ya mkutano wao uliofanyika hivi karibuni.

Maaskofu wanawataka viongozi wa Serikali kuguswa na mahangaiko pamoja na changamoto zinazojitokeza miongoni mwa wananchi wao, tayari kuwasikiliza kwa makini na kuwapatia majibu muafaka. Huu ni mwaliko wa kuwasikiliza maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Maandalizi na hatimaye uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo mwishoni mwa Mwaka 2017 kisiwe ni kisingizio cha kushughulikia matatizo na changamoto za wananchi wa Chile, hasa wale maskini. Hapa kuna haja ya kuendelea kudumisha demokrasia, utawala wa sheria, ustawi na maendeleo ya wengi, daima binadamu akipewa kipaumbele cha kwanza.

Baraza la Maaskofu Katoliki Chile katika tamko lake linalojulikana kama: Majadiliano, uwajibikaji na huruma kwa ajili ya Chile inayosimikwa katika haki” linapenda kuonesha wasi wasi wake kutokana na kuteteleka kwa huduma za afya katika sekta ya umma sanjari na hali ngumu ya maisha hasa kwa wale wanaopokea mshahara wa kima cha chini kiasi kwamba, wanashindwa kutekeleza wajibu kwa familia zao. Kuna umati mkubwa wa watu wasiokuwa na fursa za ajira; kuna mahangaiko makubwa kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta fursa za maisha bora zaidi, bila kusahau sheria iliyopitishwa hivi karibuni, inayokumbatia utamaduni wa kifo, kwa watoto ambao bado hawajazaliwa. Madhara ya sheria hii ni makubwa kwa wanawake na wasichana.

Baraza la Maaskofu Katoliki Chile linaitaka Serikali kutoa elimu makini itakayozingatia ukuaji, ustawi na maendeleo ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Watoto na vijana wanapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika mfumo wa elimu utakaowasaidia kupambana na mazingira yao, ili hatimaye, kuyafanya kuwa ni mahali bora zaidi pa kuishi. Wanakumbusha kwamba, wazazi ni walimu wa kwanza wa tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili, kumbe, wanapaswa kupewa fursa ya kuwaunda na kuwafunda watoto wao mintarafu tunu msingi za Kiinjili, kiutu na kimaadili, bila kuyumbishwa na sera za usawa wa kijinsia zinazotaka kupindisha mpango wa Mungu katika maisha ya binadamu!

Kamwe wananchi wa Chile wasitumbukizwe kwenye ukoloni mamboleo unaofumbatwa katika sera za usawa wa kijinsia kinyume cha utu na heshima ya binadamu! Haki msingi za binadamu, huduma na mazingira bora ya kufanyia kazi ni kambo muhimu sana katika uzalishaji, tija na huduma kwa jamii. Kumbe, hapa kila mwananchi anapaswa kujituma na kujisadaka ili kuhakikisha kwamba, anatekeleza dhamana na wajibu wake barabara, kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Siasa inapaswa kuwa ni huduma kwa ajili ya wananchi ili kukuza mchakato wa demokrasia, utawala bora na ushirikishwaji wa wananchi katika kupanga, kuamua na kutekeleza sera na mikakati yao ya maendeleo: kiroho na kimwili na kamwe siasa kisiwe ni kichaka cha ubinafsi, rushwa, uchu wa mali na madaraka. Wananchi wengi hawaridhishwi na mwenendo wa wanasiasa nchini Chile, kiasi cha kuanza kupoteza imani katika masuala ya kisiasa. Ikumbukwe kwamba, wananchi wana haki ya kuwawajibisha wabunge wao, ili kweli fursa waliyopewa na wapiga kura wao, inatumiwa vyema kwa ajili ya maendeleo ya wengi na wala si kwa ajili ya uchu wa mali na madaraka. Kumbe, Serikali inawajibu wa kuhakikisha kwamba, inasikiliza kwa makini na kujibu kilio, matumaini na matarajio ya wananchi wake kadiri ya fursa zilizopo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.