2018-01-15 14:05:00

Kardinali Sèrgio da Rocha: Maskini ni amana na utajiri wa Kanisa!


Kardinali Sèrgio da Rocha, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Brasilia, nchini Brazil katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano anasema, Kanisa linawategemea sana maskini katika maisha na utume wake, kwani maskini ni amana na utajiri wa Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima. Kimsingi, maskini ndio walengwa wakuu wa Injili. Dhana ya umaskini inajikita katika umaskini wa hali na mali; maadili na utu wema; kwani wote hawa Kristo Yesu amejisadaka kwa ajili ya kuwatangazia Habari Njema ya Wokovu.

Kardinali Sèrgio da Rocha ni kati ya Makardinali wapya walioteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko na kusimikwa rasmi wakati wa kufunga maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kwa hakika anasema, wao ni “majembe” na mashuhuda wa huruma ya Mungu miongoni mwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Brazil kwa wakati huu inakabiliwa na changamoto nyingi, hasa umaskini miongoni mwa wananchi wake, hali ngumu ya uchumi pamoja na ukosefu wa fursa za ajira, bila kusahau rushwa na mmong’onyoko wa maadili na utu wema.

Brazil imebahatika kuwa na rasilimali nyingi, lakini kwa bahati mbaya rasilimali hizi hazijafua dafu katika mapambano dhidi ya umaskini na matokeo yake, wanaofaidika ni watu wachache ndani ya jamii. Katika shida na mahangaiko ya watu, Kanisa limebahatika kugundua tunu msingi za maisha ya kiutu, kitamaduni na kiroho zinazoweza kutumiwa na Mama Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji mpya, unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa watu! Habari za kuteuliwa kwake kuwa Kardinali alipewa na waamini wake, baada ya kusikiliza taarifa ya habari ambamo Baba Mtakatifu alikuwa anawataja Makardinali wapya. 

Maskini hawa katika umaskini wao, wakaonja huruma na upendo wa Kristo kwa njia ya Baba Mtakatifu Francisko aliyethubutu kumteuwa kuwa ni kati ya washauri wake wa karibu, ili kumshirikisha utajiri na amana inayofumbatwa kutoka kwa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili watambue kwamba, kweli wao ni kiini cha Habari Njema ya Wokovu! Mwenyezi Mungu anaendelea kuwashangaza walimwengu kutokana na huruma na upendo wake kwa maskini. Kwa njia hii, anaweza kumshirikisha Baba Mtakatifu uzoefu na mang’amuzi yake yanayopata chimbuko lake kutoka kwa familia ya Mungu nchini Brazil.

Jimbo kuu la Brasilia nchini Brazil, limeundwa takribani miaka hamsini iliyopita na linawajumuisha watu wa dini, imani na madhehebu mbali mbali ya Kikristo, kumbe hapa majadiliano ya kidini na kiekumene yako nyumbani kabisa kutokana na mwingiliano wa watu hawa! Lakini, changamoto kubwa inayowakabili watu hawa ni mwingiliano wa tamaduni na watu kutoka sehemu mbali mbali, kwani wananchi wengi wa Jimbo kuu la Brasilia ni wahamiaji pamoja na Kardinali Sèrgio da Rocha mwenyewe. Ukosefu wa usawa katika masuala ya kijamii, ukosefu wa fursa za ajira na umaskini wa kutupwa ni kati matatizo na changamoto ambazo Kanisa linapaswa kuyafanyia kazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Kuna baadhi ya watu ambao ni matajiri wa kutupwa, lakini pia kuna akina “yakhe pangu pakavu tafadhali tia mchuzi”. Hawa ni wananchi zaidi ya milioni tatu. Hii  ni changamoto pevu katika mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima! Hapa kuna Ibada ambazo zinapaswa kuinjilishwa na kutamadunishwa kadiri ya tunu msingi za Kiinjili, vinginevyo, waamini wanaweza kujikuta wakiwa wanaburuzwa na imani za kishirikina mbali kabisa na misingi ya Kiinjili. Kumbe, Uinjilishaji mpya unaendelea kupewa kipaumbele cha kwanza kwa kukazia majiundo makini ya awali na endelevu ya waamini walei, ili kweli waweze kupikwa na kuiva katika shule ya Kanisa la Kristo, tayari kumshuhudia Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, Kristo chimbuko la imani, matumaini na mapendo kwa waja wake! Familia na Jumuiya za Kikristo ni mahali muafaka pa Uinjilishaji unaojikita katika tunu msingi za maisha ya Kikristo.

Kardinali Sèrgio da Rocha ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil ambaye anasea, wajibu wake mkubwa ni kujenga daraja la umoja, mshikamano, upendo na imani miongoni mwa Maaskofu wenzake, ili kwa pamoja waweze kutembea katika njia ya imani na matumaini kwa ajili ya kukoleza mchakato wa Uinjilishaji nchini Brazil. Brazil ina jumla ya Maaskofu 460, Maaskofu wastaafu hadi sasa ni 150, wote hawa wanahitaji kuangaliwa kwa jicho la pekee na Kanisa kwani ni watu waliojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Nchini Brazil kuna utajiri mkubwa wa maisha ya Kikristo na changamoto endelevu katika maisha ya watu wanaoogelea katika umaskini wa hali na kipato. Ukosefu wa Mapadre wa kutosha katika mchakato wa Uinjilishaji hasa eneo la Amazzonia ni changamoto pevu. Kanisa linaendelea kuwainjilisha maskini ili waweze kutambua kwamba, wao ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa na kwamba, hata katika umaskini wao, wanaweza kuchangia kwa hali na mali katika ustawi na maendeleo ya Kanisa.

Kanisa linaendelea kuwawezesha waamini wake kiuchumi ili waweze kutekeleza majukumu yao katika familia na jamii katika ujumla wake, ili wasiwe ni wahanga wa biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya pamoja na utumwa mamboleo; mambo ambayo yanaendelea kudhalilisha utu na heshima ya binadamu. Kanisa linaendelea kuwekeza zaidi katika michezo na sanaa kama njia ya kumwilisha tunu za Injili katika maeneo haya anasema Kardinali da Rocha ambaye ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Brazil kwani michezo nchini Brazil ni sawa na chanda na pete! Wakristo wote wanakumbushwa kwamba, wao kwa njia ya Ubatizo wanashiriki: Ukuhani, Ufalme na Unabii wa Kristo Yesu, kumbe, wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Uinjilishaji kati ya jirani na ndugu zao, ili kuwaonjesha ile furaha ya Injili kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko, kwani wamekutana na Kristo Yesu katika maisha yao; na Kristo ni sababu na chemchemi ya jeuri na furaha ya maisha waliyo nayo kwa sasa!

Parokia zinaendelea kuwa ni mahali muafaka pa Uinjilishaji; mahali ambapo waamini wanakutana kwa ajili ya katekesi makini, Ibada ya Misa Takatifu ili kushiriki Neno la Mungu na chakula cha uzima wa milele, tayari kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Parokia ni mahali pa kujenga umoja na mshikamano wa Kanisa unaofumbatwa katika familia na Jumuiya ndogo ndogo za Kikristo! Dhana na ari ya kimissionari ni chemchemi ya maisha na utume wa Kanisa nchini Brazil, dhana inayovaliwa njuga na familia ya Mungu katika ujumla wake! Dhana ya Umissionari inaendelea kulipyaisha Kanisa la Mungu nchini Brazil, kwani inawawezesha wakleri, watawa na waamini walei kushirikiana kwa karibu sana katika kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Injili anasema Kardinali Sèrgio da Rocha. Mshikamano na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni changamoto endelevu katika maisha na utume wa Kanisa. Hawa ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa; ni amana na utajiri wa Kanisa unaopaswa kuheshimiwa na kuendelezwa. Kuna haja ya kumwilisha tunu msingi za Kiinjili katika uhalisia wa maisha ya watu kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina na endelevu unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.