2018-01-15 13:30:00

Hija ya Kitume Amerika ya Kusini inapania kuimarisha Kanisa mahalia!


Baba Mtakatifu Francisko ameanza hija yake ya ishirini na mbili ya kimataifa huko Amerika ya Kusini, ambako anatembelea Chile na Perù kuanzia tarehe 15 Januari hadi tarehe 22 Januari 2018 atakaporejea tena mjini Roma kuendelea na utume wake. Hii ni safari ya masaa kumi na sita angani. Kabla ya kuondoka mjini Roma, Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza kwa sana katika hija hii ambayo ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa Amerika ya Kusini.

Akiwa njiani, Baba Mtakatifu ametuma salam na matashi mema kwa wakuu wa nchi kadhaa ambamo amepitia wakati akielekea nchini Chile. Salam hizi zimetumwa kwa Rais Sergio Mattarella wa Italia, Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa, Mfalme Filipe VI wa Hispania, Mfalme Mohammed VI wa Morocco; Rais Jorge Carlos Fonceca wa Visiwa vya Cape Verde, Rais Macky Sall wa Senegal, Rais Michel Temer wa Brazil, Rais Horacio Cartes wa Paraguay pamoja na Rais Mauricio Macri wa Argentina. Wote hawa amewatakia: amani, furaha na utulivu; ustawi na maendeleo; neema, baraka na nguvu pamoja na kuwaomba kuendelea kumsindikiza katika hija hii kwa sala zao!

Baba Mtakatifu katika salam zake kwa Rais Sergio Mattarella wa Italia, amemwelezea lengo la hija yake ya kitume nchini Chile na Perù kwamba, inapania kuimarisha mchakato wa maisha na utume wa Kanisa mahalia katika nchi hizi pamoja na kuwatangazia ujumbe wa matumaini. Anawatakia wananchi wote wa Italia ustawi na maendeleo ya maisha ya kiroho na kimwili. Naye kwa upande wake, Rais Sergio Mattarella wa Italia amemshukuru Baba Mtakatifu kwa kumtakia safari na utume mwema. Italia na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake, inatambua fika umuhimu wa hija hii ya kitume ambayo inajikita kwa namna ya pekee katika fadhila ya matumaini, utamaduni na Mapokeo ya Kikristo. Uwepo wake kati ya wananchi wa Chile na Perù ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa ujenzi wa jamii inayosimikwa katika msingi wa haki na usawa. Baba Mtakatifu Francisko amewapatia wananchi wote wa Italia baraka zake za kitume! Mtakatifu Yohane Paulo II alitembelea Chile kunako mwaka 1987 na nchini Perù kunako mwaka 1985 na Mwaka 1988.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.