Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Mahubiri

Papa: Jitahidini kualika, kufahamiana na kujitambulisha na watu!

Papa Francisko anawaalika waamini kujenga utamaduni wa kualika, kufahamiana na kujitambulisha kati ya watu. - AFP

14/01/2018 11:15

Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee kabisa, amependa maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2018, yapambwe kwa Ibada ya Misa Takatifu ambayo ameiongoza, Jumapili tarehe 14 Januari 2018 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa familia ya Mungu inayotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Liturujia ya Neno la Mungu imejikita zaidi katika wito kwani kila mwamini anaitwa kwa jina na kwamba, ameumbwa kwa sura na mfano na Mungu na kila mtu anayo nafasi na dhamana yake katika historia ya dunia. Injili inawaonesha wafuasi wawili wa Yohane Mbatizaji wanaomuuliza Yesu anakaa wapi, naye anawaalika kwenda kuona mahali anapoishi, Papa anasema, hii ni changamoto ya kualika, kufahamiana na kujitambua kati ya watu wengine.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, kila mgeni anayebisha hodi kwenye malango yao ni fursa ya kuweza kukutana na Yesu, anayejitambulisha kuwa ni mgeni anayepokelewa au kukataliwa kwa kila nyakati! Hii pia ni nafasi kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa, kwani kwao kila mlango wanaobisha hodi inakuwa ni nafasi ya kukutana na Yesu.  Njoni nanyi mtaona, ni mwaliko wa Yesu unaotolewa kwa watu wote ukiwataka kuvuka woga ili kuweza kukutana na wengine, kwa kuwakaribisha, kuwafahamu na kujitambua kati yao.

Baba Mtakatifu anasema huu ni mwaliko wa kutoa nafasi ili kujenga ujirani mwema utakaomwezesha mgeni kuona mahali na jinsi wanavyoishi wenyeji wake; kutambua na kuheshimu sheria za nchi, tamaduni na mapokeo ya nchi inayowapatia hifadhi. Hii ina maanisha pia kutambua wasi wasi na matarajio yao kwa siku za usoni! Wenyeji wanahamasishwa kutambua na kuthamini utajiri unaofumbatwa katika utofauti wao bila ya kuathirika na maamuzi mbele; kwa kutambua uwezo na matumaini ya wageni waliofika hivi punde, bila kusahau hali yao tete na mashaka yaliyo wajaa mioyoni!

Mchakato wa watu kukutana unafumbatwa kwa namna ya pekee katika mambo makuu manne ambayo Baba Mtakatifu Francisko ameyabainisha katika ujumbe wake kwa Siku ya wakimbizi na wahamiaji duniani kwa Mwaka 2018 ambayo ni: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha. Kwa kutekeleza haya yote, waamini na watu wenye mapenzi mema wataweza kumpokea na kumkirimia Kristo Yesu anayejitambulisha kuwa kati ya wakimbizi na wahamiaji hawa. Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, waamini wanatekeleza kwa dhati matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Mchakato wa kukutana na Kristo Yesu ni chemchemi ya wokovu inayopaswa kutangazwa na kushuhudiwa kwa wengine kama walivyofanya wale wafuasi wa Yohane Mbatizaji, waliowashirikisha ndugu zao mang’amuzi juu ya Masiha waliokutana naye njiani!

Baba Mtakatifu Francisko anakiri kwamba, si rahisi sana kuweza kujiingiza kwenye tamaduni za watu wengine, ili kutambua mawazo, uzoefu na mang’amuzi yao na matokeo yake, watu wanajenga kuta za utengano, ili kujilinda wao wenyewe. Ni wasi wasi kwamba, wageni watawapora utajiri wao ambao wameupata kwa jasho kubwa. Wageni wanaowasili nao wana wasi wasi na woga wa kukutana na wenyeji wao, kuhukumiwa, ubaguzi na hatimaye kushindwa kutekeleza ndoto zao. Kibinadamu, wasi wasi na mashaka haya ni mambo ya kawaida na wala si dhambi.

Baba Mtakatifu anasema, mambo haya yanageuka kuwa dhambi pale ambapo woga na wasi wasi unaathiri majibu na maamuzi yao kiasi hata cha kushindwa kuheshimiana na kuoneshana ukarimu na matokeo yake chuki na kukataliwa vinatawala. Ni dhambi kushindwa kukutana na wengine, kuonana na watu walio tofauti nawe a una jirani yako, kwani hii ni nafasi maalum ya kukutana na Kristo Yesu. Yesu anaendelea kujifunua kwa njia maskini, wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, wanaotafuta hifadhi ya kisiasa, wakimbizi na wahamiaji, ambao kwa Siku ya Jumapili wameombewa kwa namna ya pekee. Hii ni nafasi pia kwa wakimbizi na wahamiaji kusali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi na Jumuiya zinazowakirimia.  Mwishoni mwa mahubiri yake, Baba Mtakatifu Francisko amewadhaminisha wakimbizi na wahamiaji chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, kwa kuyaweka matumaini yao na matarajio ya wenyeji wao ili yaendane na Amri kuu ya upendo, kwa kujikifunza kuwapenda hata wakimbizi na wahamiaji kama wanavyojipenda wao wenyewe!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

14/01/2018 11:15