2018-01-14 13:46:00

Papa Francisko sasa Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Kuadhimishwa Sept.


Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani ambayo imeadhimishwa, Jumapili tarehe 14 Januari 2018 amesema kwamba, kuanzia sasa, kutokana na sababu za kichungaji, Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji itakuwa inaadhimishwa Jumapili ya Pili ya Mwezi Septemba ya kila mwaka. Kumbe, Maadhimisho ya Siku ya 150 ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2019 yataadhimishwa tarehe 8 Septemba 2019.

Baba Mtakatifu amekazia mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha pekee katika Mafundisho Jamii ya Kanisa kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi kwa kusema kwamba ni: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha. Waamini wanapaswa kusoma alama za nyakati kwa kumtambua Kristo Yesu kati ya wakimbizi na wahamiaji wa nyati zote, ili kuweza kumfungulia malango ya maisha yao na kumkaribisha. Ameitakia heri na baraka Jumuiya ya Wananchi wa Amerika ya Kusini ya Mtakatifu Lucia inayoishi hapa Roma, kwa kuadhimisha Jubilei ya miaka 25 tangu kuanzishwa kwake. Waamini hawa ni mashuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake katika mazingira yenye matatizo na changamoto nyingi, lakini bado wameonesha furaha, sadaka na mang’amuzi ya wakimbizi na wahamiaji!

Kabla ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu amesema, Liturujia ya Neno la Mungu inaonesha ufunuo wa Bwana unaoshuhudiwa na Yohane Mbatizaji, anayewaalika wafuasi wake kumfuasa, changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, waliopata nafasi ya kumtafakari Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, wakati wa Kipindi cha Noeli, sasa umefika wakati wa kumfuasa Kristo Yesu katika uhalisia wa maisha ya kila siku kama njia ya kutafakari imani katika uhalisia wa maisha!

Hii ni imani inayofunuliwa na kumwilishwa katika ufuasi; imani inayoshuhudiwa na wito unaotekelezwa. Huu ndio ushuhuda uliotolewa na Maria Magdalena, siku ile ya kwanza ya Juma, Kristo Yesu alipofufuka kutoka kwa wafu. Ikumbukwe kwamba, daima mwanadamu ni kiumbe kinachotafuta furaha, upendo, maisha mazuri na makamilifu yanayofumbatwa katika Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai! Yohane Mbatizaji ni shuhuda anayewaelekeza wafuasi wake kumfuasa Kristo Yesu, Mwana Kondoo wa Mungu ili baada kumfuasa na kuona, waweze kumshuhudia, baada ya kuonja uzuri wa kushinda pamoja na Yesu. Hili ni tukio lililogusa sakafu ya maisha yao kiasi hata cha kukumbuka saa na huo ukawa ni mwanzo wa safari ya imani na ufuasi, changamoto na mwaliko wa kujenga mahusiano ya kudumu na Kristo Yesu. Waamini wajibidishe kumfahamu Kristo Yesu katika safari ya maisha yao, ili aweze kuwakirimia nafasi ya kushinda pamoja naye, kielelezo cha imani thabiti. Waamini watambue kwamba, wanaweza kukutana na Kristo Yesu katika: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa, chemchemi ya neema na msaada, kwa kumwambata Kristo Yesu, Mwana Kondoo wa Mungu anaye ondoa dhambi za ulimwengu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.