Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

Maaskofu wasikitishwa na uchomwaji wa Makanisa nchini Chile!

Baraza la Maaskofu Katoliki Chile linasikitishwa sana na uchomwaji wa Makanisa nchini humo wakati huu, familia ya Mungu nchini humo inapojiandaa kumkaribisha Papa Francisko. - AFP

14/01/2018 14:22

Baraza la Maaskofu Katoliki Chile limesikitishwa sana na wimbi la uchomaji wa Makanisa na kufuru kwa nyumba za Ibada zaidi ya nne, wakati huu wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko Amerika ya Kusini. Matukio haya ni kinyume kabisa cha ujio wa Baba Mtakatifu anayekwenda nchini humo kama hujaji na chombo cha amani. Katika moyo wa unyenyekevu, wananchi wote waliohusika na vitendo hivi vya “kihuni” watambue kwamba, haya si maoni wala mawazo ya familia ya Mungu nchini Chile. Wananchi wengi wanataka kujenga na kudumisha moyo wa uzalendo unaofumbatwa katika heshima na maridhiano kwa wananchi wote.

Haya yamesemwa na Kardinali Ricardo Ezzati Andrello, Askofu mkuu wa Santiago del Chile katika mahojiano na “Vatican News” kufuatia wimbi la kuchoma Makanisa pamoja na kuvamia Ubalozi wa Vatican nchini Chile, mahali ambapo Baba Mtakatifu anatarajiwa kuishi wakati wa hija yake ya kitume nchini Chile. Familia ya Mungu nchini Chile inahitaji kujenga na kudumisha ari na moyo wa majadiliano katika ukweli na uwazi. Wanaitaka familia ya Mungu nchini Perù kuwa na ari na moyo mkuu, tayari kumpokea, kumkaribisha Baba na hatimaye, kushiriki katika matukio mbali mbali yatakayoendeshwa na Baba Mtakatifu Francisko nchini Chile. Papa Francisko anakwenda kati yao hujaji wa amani, matumaini na mapendo kwa wananchi wote wa Chile.

Ni matumaini ya Kardinali Ricardo Ezzati Andrello kwamba, hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo kuanzia tarehe 15- 18 Januari 2018, itawasaidia kuimarisha Kanisa la Kimissionari; kukuza na kudumisha mchakato wa: mshikamano na ukarimu wa wananchi wa Chile; atawapatia ari na moyo mkuu wa kupambana na umaskini wa roho na mwili miongoni mwa wananchi wa Chile. Wachunguzi wa mambo wanasema: uchu wa mali na madaraka; ufisadi na wizi wa mali ya umma; pengo kubwa kati ya maskini na matajiri ni kati mambo ambayo yanaendelea kuchangia mpasuko wa kijamii nchini humo, kiasi hata cha kutaka kutumia hija ya Baba Mtakatifu Francisko ili waweze kutambulikana kwamba, hata wao wapo. Idadi ya waamini wanaoshiriki Ibada ya Misa Takatifu imepungua na kufikia asilimia 59% ya idadi ya waamini wote wa Kanisa Katoliki nchini Chile.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 

14/01/2018 14:22