Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Wakristo: Mnaitwa na kutumwa kumtangaza na kumshuhudia Mwana Kondoo

Wakristo wanaitwa, wanatumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kiini cha imani na wito wao katika maisha ya Kikristo! - EPA

13/01/2018 10:24

Maandiko Matakatifu katika dominika ya 2 ya mwaka B wa Kanisa yanakazia juu ya Wito na Ushahidi kwa Mwanakondoo wa Mungu katika maisha ya mkristo. Ndiyo kusema, mkristo ameitwa kumfuata mwanakondoo wa Mungu - ndiye Bwana wetu Yesu Kristo. Njia ya ufuasi anayoalikwa kuipitia si nyingine bali ni njia ya ushahidi yaani kuwa shuhuda wa Kristo katika maisha ya kila siku. Kama anavyofundisha Papa Francisko, mkristo asiyemshuhudia Kristo katika maisha yake ni kama mti wa matunda usiozaa kamwe matunda, na katika mantiki hiyo ni mti usio na faida. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani kwa Mwaka 2018 tunayoiadhimisha leo tarehe 14 Januari 2018 anakazia kwa namna ya pekee umuhimu wa “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowakirimia.

Somo la kwanza (1Sam. 3:3b-10,19) linaeleza juu ya wito wa Samweli anayeitwa kuchukua nafasi ya Eli. Eli alikuwa kuhani lakini Mungu alimkataa asiendelee kuwa kuhani wake kwa sababu alishindwa kutekeleza vema majukumu yake ya kikuhani. Alishindwa kwa mfano kuwakemea watoto wake Hofni na Fineas ambao walikuwa wakizifanyia kufuru dhabihu zilizokuwa zinatolewa kwa Bwana altareni (rej. 1Sam. 2:27-36). Mwenyezi Mungu anamwita Samweli mara tatu. Mara zote hizo Samweli anashindwa kuelewa ni nani anayemwita, anakwenda kwa Eli. Baada ya mara hizo tatu ndipo Eli anaelewa kuwa Mungu anamwita Samweli. Anamwelekeza namna ya kuuitikia wito huo na kisha kuuitikia wito Samweli hakuliacha kamwe Neno la Bwana.

Somo la pili (1Kor. 6:13-15,17-20) linaeleza juu  ya utakatifu wa mwili. Utakatifu unaohitaji kuuchukulia daima mwili kwa heshima na uadilifu. Somo hili ni sehemu ya mafundisho ya mtume Paulo kwa Wakorinto dhidi ya mmomonyoko mkubwa wa maadili waliokuwa nao. Mmomonyoko huo ulihalalishwa na kanuni yao iliyokuwa ikisema“vyote ni halali kwangu” na kwa hiyo walifanya yoyote waliyotaka kutimiza haja zao za kimwili. Mtume Paulo aliinukuu kanuni hiyo awali (1Kor. 6:12) na kutoka hapo akaanza kuwaonesha namna ya kuenenda inayofaa kwa mkristo. Mtume Paulo anaeleza kinagaubaga kuwa mwili si kwa ajili ya zinaa, ni  wa Bwana. Mwanadamu hana uhuru wa kuutumia anavyotaka isipokuwa anavyotaka Bwana. Na namna ifaayo ya kuutimia mwili ni kwa ajili ya kumtukuza Mungu kwa sababu mwili wa mwanadamu ni hekalu la Roho Mtakatifu.

Somo la Injili (Yoh. 1:35-42) linaendeleza dhamira ya somo la kwanza na kueleza wito wa wanafunzi wa kwanza wa Yesu. Hawa awali walikuwa ni wanafunzi wa Yohane Mbatizaji. Yohane anawaonesha kwa Yesu nao wanamfuata. Wanaenda kuona “anapokaa” na wanakaa naye hadi saa kumi, namba ya kibiblia inayomaanisha kuwa wanakaa hadi muda wa kufanya maamuzi. Wanafunzi hao wanatoka na kwenda kumleta Simoni ambaye Kristo alimpa jina Petro.

Katika masomo ya Liturujia ya Neno la Mungu leo,, dhana ya wito na dhana ya ushuhuda zinatawala. Dhana hizi zinawekwa katika namna inayoonesha kwamba kila moja huhitaji nyingine na kila moja hukamilishwa na nyingine. Ndio kusema kuwa wito hutekeleza lengo lake pale unapokuwa ni nafasi ya kutoa ushuhuda. Wale mitume wa kwanza wanaupata wito wao na kumfuata Kristo kutokana na ushuhuda Yohana Mbatizaji. Ushuhuda aliokwisha utoa hapo awali na hata sasa kwa maneno akiwaambia wanafunzi wake “Tazama mwanakondoo wa Mungu”, nao wanafunzi wanamfuata Yesu.  Baada ya kukaa na Yesu hadi muda muafaka wa kufanya maamuzi ya kuupokea wito huo, wao pia wanaenda kutoa ushuhuda kwa wengine: Andrea anamfuata Simoni anamleta kwa Yesu naye anapewa jina Petro. Wito wa wanafunzi hao wa kwanza ulianza kwa ushuhuda na unaendeleza ushuhuda. Tofauti na wanafunzi hao Eli kuhani wa Agano la Kale anakuwa ni mfano wa wale wanaoshindwa kuushuhudia wito wao. Ananyang’anywa nafasi ya ukuhani na badala yake Mungu anamwita Samweli.

Hali kadhalika wito wa kuwa mkristo ni wito unaoambatana na jukumu la kutoa ushuhuda kwa Kristo. Jina lenyewe m-kristo, sambamba na kumpa mtu hadhi mpya, linaashiria jukumu hilo. “Nanyi mtakuwa mashahidi wangu” (Mdo. 1:18) aliwaagiza Yesu wanafunzi wake alipokuwa akipaa kwenda mbinguni. Mkristo anakuwa shahidi wa Kristo kwa kuendeleza kazi ya ukombozi ya Kristo; kutangaanza kifo chake na kuutukuza ufufuko wake hata atakapokuja. Hivi hufanya: anaposhiriki maadhimisho ya sakramenti na ibada; anapopokea mafundisho ya Kristo, kuyaamini, kuyaishi na kuyaeneza; na anapoyaunda maisha yake katika maadili ya kikristo.

Tukirejea katika masomo ya leo, tunaona kuwa somo la pili linaunganisha dhamira hizi na kutualika kutoa ushuhuda kwa kulinda utakatifu na heshima ya mwili wa binadamu. Anakazia Mtume Paulo kuwa mwili si kwa ajili ya zinaa na matendo ya uchafu bali ni kwa ajili ya kumtukuza Mungu. Mwili si tu kama chombo tu kinachobeba roho, kama baadhi ya falsafa zinavofundisha bali unabeba sura na mfano wa Mungu; “...na tumuumbe mtu kwa sura na mfano wetu”, alitamka Mungu katika kumuumba mwanadamu na huyo kwa mwili na roho yake anabeba sura na mfano wa Mungu. Zaidi ya hayo, Mtume Paulo anaongeza kuwa mwili huu “ulinunuliwa kwa thamani” yaani ulikombolewa na Kristo kwa kumwaga damu yake. Kwa jinsi hii mwanadamu anawajibika mbele ya Mungu kwa mwili wake na wa binadamu wengine.

Mwaliko huu wa Mtume Paulo si mwaliko wa kuuangalia mwili tu, bali ni mwaliko wa kuyaangalia katika ujumla wake maadili ya maisha ya mkristo kama namna ya kutoa ushuhuda kwa wito wa kuwa mkristo. Kama ilivyokuwa kwa wakorinto, hata leo dhana ya uhuru wa mwanadamu inaleta changamoto kubwa katika maadili yake. Kwa kuweka msisitizo juu ya uhuru alionao mwanadamu wa kuchagua aina ya maisha yake, mwanadamu amejikuta anahalalisha hata yale yasiyokuwa ndani ya uhuru huo. Na zaidi ya hapo kuona kuwa kila kinachowezekana kufanyika basi ni halali kufanyika. Alitukumbusha Mwalimu Nyerere kuwa “uhuru bila mipaka ni uendawazimu”. Mipaka ya uhuru wa mwanadamu ni kanuni za kikristo za maadili katika maisha. Kanuni hizi ni zile zinazopata kama sehemu ya misingi yake katika amri kumi za Mungu, kanuni asili ya mwanadamu, Neno la Mungu na Mafundisho ya Kanisa. Mwisho wa tafakari hii tunakumbuka maneno ya Mtakatifu Yohane Paulo II alipokuwa akiwaandaa waamini kuadhimisha Jubilei Kuu ya Mwaka 2000 kuingia milenia ya tatu akisema... milenia hii mpya itahitaji ushuhuda si sana kwa njia ya kumwaga damu bali kwa njia ya utakatifu wa maisha.

Bikira Maria Malkia wa Mashahidi, utuombee.

Pd. William Bahitwa

Vatican News!

13/01/2018 10:24