Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Hotuba

Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani 2018 na changamoto zake!

Licha ya cchangamoto, matatizo na fursa mbali mbali zinazojitokeza kutokana na wimbo kubwa la wakimbizi na wahamiaji, hawa ni sehemu ya maisha na utume wa Kanisa la Kristo Yesu. - REUTERS

13/01/2018 13:41

Tema ya haki, amani na mshikamano si ngeni sana katika Mafundisho Jamii ya Kanisa. Hata katika kipindi cha Mwaka 2018, baada ya Mwaka 2017 kuwa ni ”Mwaka wa kutisha” mintarafu tema ya ukarimu “Annus horribilis” kutokana na kuibuka kwa nadharia za ubaguzi mpya wa kinazi, Baba Mtakatifu Francisko bado anaendelea kusimama kidete kutangaza na kushuhudia umuhimu wa ukarimu kwa wahamiaji na wakimbizi katika ujumbe wake wa Siku ya 51 ya Kuombea Amani Duniani, iliyoadhimishwa hapo tarehe Mosi, Januari 2018.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 51 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2018 anakazia mbinu mkakati unaopaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa kwa kuhakikisha kwamba, inatoa fursa kwa watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa, wakimbizi na wahamiaji: kwa kuwakaribisha kwani kwa kufanya hivi, watu wengi wamewakaribisha Malaika hata bila ya wao kutambua! Utu, heshima na haki zao msingi zinapaswa kulindwa na kudumishwa na wote. Kuna haja ya kuwa na mikakati ya maendeleo endelevu kwa wakimbizi na wahamiaji: kwa kuhakikisha kwamba, watoto wao wanapata elimu bora ili kuwajengea uwezo wa kujadiliana kwa kina na mapana. Mwishoni, wakimbizi na wahamiaji wanapaswa kushirikishwa kikamilifu katika maisha ya jamii mpya inayokarbisha, ili kutajirishana kwa njia ya ushirikiana na huduma makini.

Baba Mtakatifu Francisko anayapembua mambo haya makuu yanayopaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa kwa ajili ya huduma kwa wakimbizi na wahamiaji yaani: kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha. “Kuwapokea maana yake ni kutoa fursa kwa wakimbizi na wahamiaji kutumia njia za halali za uhamiaji na wala si kuwasukumizia watu hawa katika maeneo ambamo wanaweza kukabiliana na dhuluma na vita kwa kuweka uwiano mzuri kati ya usalama wa taifa na umuhimu wa kulinda haki msingi za binadamu. “Kuwalinda” ni dhamana ya kutambua haki msingi, utu na heshima ya binadamu kwa wakimbizi na wahamiaji wote wanaokimbia hatari za maisha kwa kutafuta hifadhi ya kisiasa, usalama na kuhakikisha kwamba, hawanyonywi.

Baba Mtakatifu anasema “Kuwaendeleza” ni dhana inayojikita katika mchakato mzima wa maendeleo endelevu ya wakimbizi na wahamiaji: Biblia inafundisha kwamba “Mungu anampenda mgeni, anamvisha na kumpatia chakula” kumbe, “wapendeni wageni kwani hata ninyi mlikuwa wageni nchini Misri”. “Kuwahusisha” maana yake ni kuwawezesha wakimbizi na wahamiaji kushiriki kikamilifu katika maisha ya jamii inayowakirimia kama sehemu ya mchakato wa kutajirishana na ushirikiano unaodumisha maendeleo endelevu ya Jumuiya mahalia.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, Umoja wa Mataifa katika kipindi cha Mwaka 2018 utatoa muswada na hatimaye kutoa Mkataba wa Kimataifa kuhusu; usalama, taratibu na kanuni za uhamiaji na Mkataba wa pili utawahusu wakimbizi. Mikataba hii inapaswa kusimikwa katika: huruma, mwono mpana na ujasiri, ili kutumia kila fursa inayojitokeza kwa ajili ya kudumisha mchakato wa ujenzi wa amani duniani, ili kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kudumisha majadiliano na uratibu ili kuwahudumia vyema wakimbizi na wahamiaji. Kitengo cha wakimbizi na wahamiaji cha Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu kimechapisha mbinu ishirini zinazoposwa kuvaliwa njuga na Jumuiya za Kikristo pamoja na jamii nzima katika ujumla wake. Hii ni sehemu ya mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha Ujumbe wake wa Siku ya 51 ya Kuombea Amani Duniani kwa Mwaka 2018 kwa kusema kwamba, ikiwa kama wakimbizi na wahamiaji watashirikishwa kikamilifu, “ndoto ya amani duniani” inaweza kutimia, kwa watu kujenga umoja wa familia ya binadamu ulimwenguni. Jambo hili si nadharia inayoelea kwenye ombwe! Kanisa linamkumbuka Mtakatifu Francis Xavier Cabrini, kwa kutimiza miaka 100 tangu alipofariki dunia. Ni mwanamke wa shoka, aliyesimama kidete kwa ajili ya huduma kwa wahamiaji, kiasi cha kutangazwa kuwa ni Msimamizi wa wahamiaji. Amewafundisha watu jinsi ya kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwashirikisha wakimbizi na wahamiaji katika sera na mikakati ya maendeleo endelevu, kiasi hata cha kupandikiza mbegu ya amani kwa wale wanaojenga amani duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.

13/01/2018 13:41