Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani 2018: Onesheni mshikamano!

Siku ya wakimbizi na wahamiaji duniani kwa mwaka 2018. Jengeni madaraja ya kuwakutanisha watu katika huduma ya umoja, upendo na udugu! - REUTERS

13/01/2018 14:55

Monsinyo Michael Czerny, Katibu mkuu msaidizi Idara ya Wakimbizi na Wahamiaji, Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu anasema hakuna sababu ya kuwaogopa wakimbizi na wahamiaji, bali wananchi wajenge na kudumisha madaraja ya watu kukutana na kusaidiana kama njia ya kushirikishana utajiri wa imani, tamaduni, mila na mapokeo ya watu. Ulimwengu wa utandawazi unakabiliana na changamoto kubwa za mageuzi katika medani mbali mbali za maisha kwa mfano katika mawasiliano ya jamii, kutoka kwenye Radio, Luninga, Computa na sasa Simu za viganjani. Hii ni fursa inayopaswa kutumiwa kwa ajili ya kutajirishana, ili kuendeleza mchakato wa mageuzi ya ustaarabu wa binadamu kwa kuambata tunu msingi za maisha!

Mama Kanisa katika maisha na utume wake, daima amekuwa akitoa kipambele cha kwanza katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji kwani hii ni changamoto ambayo inafumbatwa pia hata katika Maandiko Matakatifu. Hawa ni watu wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Ni watu wanaokimbia: vita, nyanyaso, majanga asilia, umaskini na ukosefu wa fursa za ajira. Wakimbizi na wahamiaji ni hazina na amana kubwa kwa nchi zinazotoa hifadhi na hata kwa zile nchi zao za asili. Kanisa linakazia sana utu, heshima na haki msingi za binadamu zinazofumbatwa hasa katika changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko yaani hawa ni watu wanaopaswa: kupokelewa, kulindwa, kuendelezwa na kuhusishwa katika sera na mikakati ya jamii inayowahifadhi.

Waathirika wakuu ni wakimbizi na wahamiaji; watu wanaomba hifadhi ya kisiasa bila kuwasahau waathirika wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu limetoa mapendekezo ishirini ambayo tayari yameingizwa kwenye Nyaraka za Umoja wa Mataifa ili yaweze kuifanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa sanjari na utekelezaji wa “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji wa mwaka 2018”. Huu ni Mkataba wa Umoja wa Mataifa unaolenga kuratibu na kuboresha mchakato wa wahamiaji na wakimbizi duniani, ili kulinda na kudumisha haki msingi, utu na heshima ya wahamiaji! Unakazia umuhimu wa jamii kusikiliza na kujibu kilio cha wakimbizi na wahamiaji duniani; kwa kukusanya maoni; kwa kupunguza gharama za kuwahudumia wahamiaji sanjari na kudumisha usalama na kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao.

Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa wahamiaji unapania pamoja na mambo mengine kuboresha: ulinzi na usalama; haki msingi za binadamu pamoja na kupatiwa huduma ya msaada wa kisheria pale haki zao zinapovunjwa. Mkataba huu unawatupia jicho wakimbizi na wahamiaji hatari kwa maisha na usalama wa raia wengine. Watu hatari wanaweza kurejeshwa makwao; uwezekano wa kudhibiti uhuru wa wakimbizi. Kimsingi “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji” unapania kutokomeza ubaguzi na maamuzi mbele; kuongeza fursa za ushirikishwaji wa wahamiaji katika maisha ya nchi wahisani; kupunguza gharama za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambazo kwa sasa umekuwa ni mzigo mkubwa kwa baadhi ya serikali pamoja na kuangalia umuhimu wa kutumia nguvu ya wakimbizi katika kuzalisha na kutoa huduma, mwishoni ni suala la udhibiti wa mipaka! Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete kupambana kufa na kupona na biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, mambo yanayonyanyasa na kudhalilisha utu, heshima na haki msingi za binadamu. Mapambano haya yanawagusa na kuwahusisha hata watu wa kawaida ambao wanapenda kuwatumikisha wenzao ili kujipatia faida kubwa sanjari na kupunguza gharama ya maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

13/01/2018 14:55