Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

Matumaini na madonda ya watu wa Chile yanayomsubiri Papa Francisko

Papa Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Chile anatarajiwa kukutana na matumaini ya wananchi pamoja na madonda yao ya ndani yanayopaswa kugangwa na kuponywa kwa njia ya Injili ya amani. - REUTERS

13/01/2018 14:13

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 15 Januari 2017 anafanya hija yake ya kitume kimataifa kwa kutembelea kwanza kabisa Chile, tarehe 19 anatarajiwa kuwa nchini Perù na tarehe 22 Januari, 2018 atarejea tena mjini Vatican. Akiwa nchini Chile, Baba Mtakatifu anatembelea mji wa Santiago, Temuco na Iquique. Nchini Chile kuna pengo kubwa kati ya matajiri na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”, changamoto kwa familia ya Mungu kujibidisha katika ujenzi na umwilishaji wa Injili ya upendo unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama njia ya kupambana na umaskini wa hali na kipato.

Mji wa Santiago katika miaka ya hivi karibuni umekuwa ni mji ambao umepokea na kutoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji kutoka katika nchi mbali mbali za Amerika ya Kusini, hali ambayo inawawajibisha wananchi wa Chile kujenga utamaduni wa upendo na mshikamano; utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana anasema Kardinali Ricardo Ezzati Andrello, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Santiago, katika mahojiano maalum na Vatican News inayofuatilia kwa kirefu na mapana hija ya Baba Mtakatifu Francisko huko Amerika ya Kusini!

Wakimbizi na wahamiaji wanasema, wanaguswa sana na jitihada za Baba Mtakatifu Francisko ambaye anaendelea kusimama kidete kuwatetea wakimbizi na wahamiaji kwenye Jukwaa la Kimataifa kwa kukazia: utu na heshima yao kama binadamu; haki zao msingi; umoja na mshikamano wa kidugu! Hili ni kundi linalopambana na changamoto za maisha na hata wakati mwingine, lina nyanyaswa na kunyonywa; linatumbukizwa hata katika biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo. Utu wa binadamu unapaswa kupewa kipaumbele cha pekee sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, chanzo kikuu cha maafa na majanga yanayomwandama mwanadamu!

Kardinali Ricardo Ezzati Andrello anasema, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake nchini Chile, atakutana na kuzungumza na  wenyeji wa Mapuche, watu Mahalia, ambao kwa miaka mingi wamenyanyaswa na kudhulumiwa, ili kuwaonesha uwepo wa Mungu katika historia na maisha yao, licha ya mateso na magumu wanayokabiliana nayo katika maisha! Kuna madonda makubwa ya uvunjifu wa haki msingi za binadamu, ukosefu wa amani, utulivu na usawa kati ya watu! Wenyeji wanasema, hija ya Baba Mtakatifu nchini humo inalenga kuwatia shime, kujizatiti zaidi katika mchakato wa amani ya kweli inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu! Wanataka kumwona na kama ilivyokuwa kwa yule mwanamke aliyetokwa damu kwa miaka kumi na miwili bila kupona, waguse hata walau pindo la mavazi ya Baba Mtakatifu.

Gereza Kuu la Wanawake wa Pequeno Cottolengo ni kati ya maeneo ambayo Baba Mtakatifu Francisko anatembelea wakati wa hija yake ya kitume nchini Chile. Gereza hili linatoa hifadhi kwa wafungwa elfu tatu, ambao wengi wao wameathirika kutokana na magonjwa mbali mbali. Hawa ni watu ambao katika undani wa maisha yao, wameonja machungu na ule utamaduni wa kutojali wala kuguswa na  mahangaiko yaw engine. Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema, kuwaendea na kuwaonjesha watu kama hawa ile furaha ya Injili inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake, licha ya matatizo na changamoto za maisha; watu wanapaswa kukazia mambo msingi zaidi katika maisha na wala si kujikita katika mambo ya mpito yasiyokuwa na mvuto wala mashiko!

Baba Mtakatifu atatembelea Madhabahu ya Mtakatifu Alberto Hurtado, SJ., Hapa pamekuwa ni kitovu cha uinjilishaji na Ibada kwa Bikira Maria ambaye ni msimamizi na mwombezi wa familia ya Mungu nchini Chile. Mwaka huu wa 2018 wanaadhimisha Jubilei ya Miaka 250 ya Uhuru wa Chile na Miaka 250 tangu BikiraMaria awekwe kuwa msimamizi wa Chile. Hapa ni mahali muafaka kwa Baba Mtakatifu Francisko kukutana na vijana wa kizazi kipya, kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana kwa kutambua kwamba, vijana ni matumaini ya Kanisa wanaoitwa na kutumwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Baba Mtakatifu atapata nafasi pia ya kukutana na kuwaonjesha vijana wasomi kutoka Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Chile upendo na huruma ya Kristo katika maisha yao, tayari kutumwa kama wamissionari vijana kumwilisha Injili ya Kristo katika maisha yao! Hii ni changamoto ya vijana kuondokana na tabia ambazo zinakinzana na tunu msingi za maisha ya Kikristo, kiutu na kijamii! Maandalizi ya hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Chile inayopambana na umaskini mkubwa imekuwa ni changamoto kubwa, inayolipa kwa matumaini kwamba, Baba Mtakatifu anakwenda kwao ili kuwapatia amani ya Kristo itakayojenga umoja, upendo, mshikamano, imani na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi kwa familia ya Mungu nchini Chile!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

13/01/2018 14:13