Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Tafakari ya Neno la Mungu

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili II: Mnaitwa na kutumwa kushuhudia

Wito wa kwanza ni utakatifu wa maisha unaomwilishwa katika ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko! - AP

12/01/2018 08:50

Wanasayansi ya kijamii wanakubaliana kwamba mazingira humuunda mtu kitabia. Ni vigumu sana mtu kukaa sehemu ya fujo na uovu mwingi kujengeka katika tabia njema. Kwa upande mwingine familia ambayo imejengeka katika misingi ya sala na uchamungu ni udongo mzuri wa kumkuza mtoto katika maadili mema ya kimungu na kiutu. Leo tunaalikwa kutafakari wito wa Mungu kwetu. Yeye anatuita ili tukae pamoja naye, tujifunze kwake na mwisho atutume kwenda kuufunua upendo wake kwa watu wote. Mwenyezi Mungu anatuandalia mazingira kila mmoja wetu kwa namna tofauti ili kuwa vyombo vyake vya kuieneza Injili yake. Wito kwetu ni kuisikiliza vema sauti yake na kuyashika maneno yake ili kuupata vema wito wake na kwenda kuutekeleza pale anapotutuma. Hiyo ndiyo maana pana ya wito: kwamba anayeita ni Mungu mwenyewe, sababu za kukuita anazijua Yeye mwenyewe na mahali anapotutaka twende anapafahamu Yeye mwenyewe. Kwetu sisi inahitajika utayari, utii na kujikabidhisha kwake.

Neno la Mungu Dominika ya leo linatufunulia juu ya wito wa Mungu. Somo la Injili linatuonesha wito wa wafuasi wa kwanza wa Kristo. Simulizi la Injili linatuonesha kuwa walikuwa ni wafuasi wa Yohane Mbatizaji naye ndiye anawatambusha Kristo akisema: “Tazama Mwana-kondoo wa Mungu”. Hapa tunaiona tabia ya kwanza ya wito katika nafasi ya wale ambao wanatusaidia kuisikia sauti ya Mungu anayeita. Yohane Mbatizaji alimtambua Kristo na alikubali kwamba, wajibu wake umekamilika. Sasa anapaswa kuwaelekeza wengine kwa Kristo. Alimpatia Kristo nafasi stahiki ili kutenda katika nafsi za wanadamu wote kazi yake ya ukombozi. Namna hii pia inaonekana katika somo la kwanza kwa mzee Eli ambaye anamwelekeza kijana Samweli kuitambua sauti ya Mungu.

Hapa tunaiona nafasi ya kwanza tunayopewa sisi wabatizwa ya kuwapeleka watu kwa Kristo. Katika familia nafasi hii inakasimiwa kwa wazazi. Katika Ibada ya Sakramenti ya Ndoa wanandoa huulizwa kama wako tayari kuwa pokea watoto watakaopewa na Mungu na kuwalea kama ilivyo sheria ya Kristo na Kanisa. Huu ni wajibu wa kuwaandalia mazingira mema watoto ili kujengeka katika misingi ya kiimani kwa ajili ya ufanisi wa jamii ya mwanadamu. Mazingira tunayowatembeza watoto wetu yanapaswa kutupatia fursa ya kuwaaonesha Kristo na kuwaambia: “huyu ndiye Mwana-kondoo waMungu”; yanapaswa kuwa ni maeneo ambayo yanayotoa fursa kwetu kwa kuitambua sauti ya Mungu inayochipuka ndani mwa watoto wetu. Mungu anamuita jirani yako kupitia wewe, basi ni wajibu wako kumwelekeza jirani yako na kumpatia njia sahihi kuisikia sauti ya Mungu.

Hatua ya pili muhimu katika Wito ni utayari wa kupokea wito. Katika Injili tunaona kwa namna anuai. Wale mitume wawili wa kwanza walipoulizwa na Kristo “mnatafuta nini” wao walimjibu kwa kutaka kujua nyumbani kwake: “Rabi, unakaa wapi?” Walitaka kufahamu nyumbani kwake, walitaka mwaliko wake ili wapate fursa ya kukaa naye zaidi na kujifunza. Kristo anapowakaribisha kwake Neno la Mungu linatuambia kwamba “wakakaa kwake siku ile”. Ni ishara ya utayari wa kujifunza na kumsikiliza. Hapa walijiaminisha kwake katika upendo mkubwa. Hii pia ni tabia nyingine muhimu wakati wa kuitikia wito. Walishadokezewa na Yohane Mbatizaji kuwa Yeye ni nani. Wanapomfuata basi wanapata fursa ya kumjua zaidi na hata fursa hiyo inawawezesha kwenda kumtangaza na kuwavuta wengine kwa Kristo. Andrea anampelekea habari nduguye Simoni Petro akamwambia: “Tumemwona Masiha (maana yake Kristo). Akampeleka kwa Yesu”. Hapa tunaona tena tendo la kuwapeleka wengine kwa Kristo lakini pia tunafunuliwa jinsi mkutano wao wa siku nzima na Yesu uliwafanya kumjua zaidi. Mwanzo waliambiwa na Yohane Mbatizaji kuwa ni Mwana-kondoo wa Mungu lakini sasa wamemjua zaidi kuwa ni Masiha (yaani Kristo). Katika somo la kwanza kijana Samweli anatuonesha namna nyingine ya kuitikia wito wa Mungu. “Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia”.

Mwanzoni mwa tafakari hii nimedokeza athari za mazingira kati kuilea tabia ya mtu. Tunapozungumzia wito wa Mungu lazima kuangalia pia na umuhimu wa kumwekea mazingira stahiki kwa sauti yake kupenya. Kijana Samweli na wafuasi wa mwanzo wa Kristo walikuwa katika mazingira rafiki na waliongozwa na watu sahihi. Samweli “alikuwa amelala katika hekalu la Bwana, palipokwa na sanduku la Mungu” na wafuasi hawa wa mwanzo wa Kristo walikuwa wanaongozana na Yohane Mbatizaji. Sauti ya Mungu inawajia si kwa nasibu. Sauti ya Mungu inawajia na kuukuta udongo wenye rutuba. Waswahili wanasema: Mtoto umleavyo ndiyo akuavyo. Mazingira rafiki tunayowapatia wenzetu ndiyo msaada kwao kuisikia sauti ya Mungu.

Jamii yetu leo hii ipo katika hali ya ukame mkubwa ya ukosefu miito, changamoto ambayo inaambatana na kuporomoka kwa maadili ya kikristo. Moja ya sababu zake kubwa ni kupotea kwa hofu ya Mungu baina ya wanajamii. Maisha yetu ya kiroho yamesawazishwa na mambo ya kidunia na hivyo yale ambayo huitaji majibu ya kiroho yanakosa mashiko na kusukumiziwa pembeni. Haya ni mashitaka kwetu kwa namna tunavyowaandalia wenzetu mazingira ya kumjua Mungu. Ni miujiza tu itakayomfanya mtoto anayekuzwa katika kutegemea na kuona umuhimu katika mambo ya kidunia kuitikia wito wa Mungu. Leo hii tunawajaza mambo ya teknolojia, tunawatajirisha kwa michezo na matukio ya kidunia ambayo katika ujumla wake hayana nafasi kwa Mungu na mbaya zaidi tunawaibia haki yao watoto wetu katika mambo ya kiroho kwa kusingizia kwamba wataamua wenyewe wakiwa wakubwa.

Vijana wetu leo hii wanaitwa na Mungu kumtumikia katika miito mbalimbali lakini wanahitaji msaada wa kuelekezwa ili kuitikia kama atakavyo Mungu. Msingi mzuri wa kiimani tunaowajengea ni nyenzo ya msaada kwao kumwitikia Mungu ipasavyo. Nafasi ya mzee Eli inajitambulisha kwetu katika nafasi mbalimbali kama wazazi, walezi au viongozi wa kiroho. Kijana anapotujia kwa kutaka maelekezo kwa kile anachokisikia tunapaswa kuwaelekeza kuitikia kama atakavyo Mungu. Lakini tutawezeshwa kuitikia wajibu huu kama nasi tunajiweka vema na kuwa na ukaribu na Mungu. Urafiki wetu na Mungu ni chachu ya kuwafanya wengine kuyaona maneno ya  Mungu kwao kupitia sisi yana tija. “Matendo hunena zaidi ya matendo”. Ukitaka kumwelekeza mmoja juu ya faida na umuhimu wa kujitoa kwa ajili ya wengine unapaswa kwanza wewe kuwa mfano kwa matendo yako.

Mtume Paulo anatukumbusha juu ya wito wetu wa kwanza wa kufanyika Wakristo. Wito huu unatuunganisha na Kristo na kuwa viungo vyake. Hivyo tutendapo dhambi katika miili yetu tunauathiri mwili wa Kristo. Kwa kuungana na Kristo tunakubali kuitikia wito wake na kutenda kwa ukamilifu katika Yeye. Dhambi ya uzinzi inalichafua hekalu la Mungu. Mungu anapotuita nasi kuitikia wito wako anatuchukua wazima wazima mwili na Roho na Yeye ndiye anayejua na kutuelekeza nini tunachopaswa kukifanya. Himizo hili la kitume linaitukuza asili ya mwanadamu kuwa ni mwili na Roho. Athari juu ya kimoja hukifikia pia kingine. Muunganiko wetu na Mungu, mwitiko wetu kwa wito wa Mungu si nusu nusu bali ni mwanadamu mzima mwili na roho. Basi tujikabidhishe kwake Yeye wazima na kumwachi atufundishe njia zake na kutuelekeza kile alichonuia sisi kukifanya kwa ajili ya wokovu wa watu wote.

Padre Joseph Peter Mosha.

Vatican News!

12/01/2018 08:50