2018-01-12 07:18:00

Papa Francisko vipaumbele vya Kanisa kwa Mwaka 2018: Vijana na Familia


Baba Mtakatifu Francisko katika sera na mikakati yake ya shughuli za kichungaji kwa Kanisa la Kristo kwa Mwaka 2018 anapenda kujikita zaidi katika kukuza na kudumisha Injili ya familia inayokabiliana na changamoto changamani; utume kwa vijana wa kizazi kipya; ndiyo maana ameitisha Sinodi ya Maaskofu itakayoadhimishwa hapa mjini Vatican, Oktoba 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, imani na mang’amuzi”. Hii ni fursa kwa Mama Kanisa kuwasikiliza na kuwasindikiza vijana katika safari ya maisha yao kwa imani, matumaini na ari kuu zaidi. Baba Mtakatifu anauanza mwaka 2018 kwa kufanya hija ya kitume Amerika ya Kusini kwa kutembelea Chile na Perù kuanzia tarehe 15 hadi 22 Januari 2018 ili kuishirikisha familia ya Mungu katika nchi hizi amani na matumaini!

Haya ni kati ya mambo msingi ambayo yamejadiliwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na “Vatican News”. Kanisa katika ngazi mbali mbali ya maisha na utume wake, linapenda kutoa kipaumbele cha kwanza kwa sera na mikakati ya vijana wa kizazi kipya. Huu ni mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza kwa makini vijana; kutambua matamanio yao halali, kupembua kwa kina na mapana changamoto na shida mbali mbali zinazowakumba vijana; matumaini, udhaifu pamoja na karama ambazo wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu, na ikiwa kama zitatumika vyema zitasaidia sana ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu.

Kanisa linatambua dhamana na wajibu wake kwa vijana, ndiyo maana linataka kuanzisha na kudumisha mchakato wa majadiliano kati ya Kanisa na vijana. Baba Mtakatifu anapenda kuwauliza vijana, Je, wanataka kulifanyia nini Kanisa la Kristo? Vijana wanaweza kutoa mchango gani katika mchakato mzima wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko? Vijana wanaweza kujibu changamoto hizi zote kwa njia ya upendo, ukarimu, ari na mwamko wao wa ujana.

Kardinali Pietro Parolin, anasema, Mama Kanisa kuanzia tarehe 21 hadi 26 Agosti 2018 ataadhimisha Siku ya IX ya Familia Duniani, huko Jimbo kuu la Dublin nchini Ireland, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Injili ya familia, furaha ya ulimwengu”. Hili ni tukio muhimu sana katika kukuza na kudumisha Injili ya familia, baada ya Baba Mtakatifu Francisko kuchapisha Waraka wake wa Kitume “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Huu ni muda wa kutafakari na hatimaye, kumwilisha  ujumbe huu katika uhalisia wa maisha ya ndoa na familia. Ni wakati wa kufanya upembuzi yakinifu kutokana na changamoto ambazo zimeibuliwa hivi karibuni mintarafu waraka huu wa Baba Mtakatifu, ili kuangalia matatizo ambayo bado yanalikabili Kanisa mintarafu Injili ya familia. Jambo la msingi hapa ni toba na wongofu wa ndani; waamini wawe tayari kutembea katika Mwanga wa furaha ya Injili, kwa kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao, tunu msingi za Injili ya familia, ili kuliwezesha Kanisa kukua na kustawi!

Baba Mtakatifu Francisko mwezi Machi 2018, anaadhimisha kumbu kumbu ya miaka mitano tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Hiki ni kipindi ambacho kimekuwa na changamoto kubwa, lakini kwa njia ya ushirikiano na mshikamano na Baraza la Makardinali Washauri kuna hatua kubwa ambayo imefikiwa kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Baba Mtakatifu anakazia ari, mwamko na tunu msingi za maisha ya Kikristo kuwa ni kiini cha mabadiliko anayokusudia kuyafanya kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo. Ni changamoto ya kuondokana na mambo yote yale yanayoweza kukwamisha maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Sekretarieti kuu inapaswa kuwa ni chombo cha huduma na msaada mkubwa kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kutangaza  na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kati ya watu wa Mataifa hadi miisho ya dunia! Baba Mtakatifu anaendelea bado kufanya mageuzi makubwa ndani ya Kanisa ambayo yatahitaji muda, uvumilivu na utayari.

Kardinali Parolin anaendelea kufafanua kwamba, Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 15 hadi tarehe 21 Januari 2018 anatarajiwa kufanya hija ya kitume nchini Chile na Perù, huko Amerika ya Kusini. “Amani yangu Nawapa” ndiyo kauli mbiu inayoongoza hija ya kitume ya Baba Mtakatifu nchini Chile kwa mwaka 2018; wakati ambapo familia ya Mungu nchini Perù imechagua “Umoja wa Matumaini” kuwa ndiyo kauli mbiu wakati wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini humo! Baba Mtakatifu katika hija zake za kitume, anapania kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana! Anakwenda huko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ili kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo. Anataka kukutana uso kwa uso na familia ya Mungu huko Chile na Perù. Makanisa haya mahalia yanakabiliwa na changamoto mbali mbali ambazo zinapaswa kuvaliwaa njuga! Kati ya changamoto hizi ni uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya watu mahalia, ambao kwa miaka mingi wamesahauliwa.

Kumbe, Sinodi ya Maaskofu wa Amazzonia itakayoadhimishwa kunako mwaka 2019, inapania kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji na uinjilishaji kwa watu mahalia. Uharibifu wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi ni kati ya mambo yanayotishia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Rushwa na ufisadi wa mali ya umma ni saratani inayokwamisha mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu, kiasi hata cha kuendelea kuwatumbukiza watu katika janga la umaskini wa hali na kipato. Hija hii, ina changamoto zake, lakini, Baba Mtakatifu anataka kukabiliana nazo uso kwa uso bila kupindisha maneno!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.