2018-01-12 07:39:00

Papa Francisko nchini Perù: cheche ya "Umoja wa matumaini" kwa wenyeji


Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 15 hadi tarehe 21 Januari 2018 anatarajiwa kufanya hija ya kitume nchini Chile na Perù, huko Amerika ya Kusini. Baba Mtakatifu anasema, anakwenda kati yao kama hujaji wa Furaha ya Injili, ili kushirikishana nao “Amani ya Bwana” na “Kuwaimarisha katika matumaini. Lengo ni kuweza kushirikishana amani na matumaini kwa familia ya Mungu katika nchi hizi! Anataka kukutana na kuangaliana nao mubashara: uso kwa uso, ili kuwamegea uwepo na ukaribu wa Mwenyezi Mungu kati yao. Anataka kuwaonjesha: upendo, upole na huruma ya Mungu inayowakumbatia na kuwafariji. “Umoja wa Matumaini” ndiyo kauli mbiu wakati wa hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Perù.

Familia ya Mungu nchini Perù ina hamu na shauku kubwa ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko, anayejipambanua kuwa ni mtetezi wa wanyonge na Baba wa maskini. Waamini wa Jimbo kuu la Puerto Maldonado, lililoko kwenye Ukanda wa Misitu ya Amazzonia wanayo shauku kubwa, ari na moyo mkuu. Hawa ni watu ambao, Baba Mtakatifu amewaangalia kwa jicho la huruma na kuamua kutisha Sinodi ya Maaskofu wa Amazzonia itakayoadhimishwa kunako mwaka 2019. Lengo kuu la Mababa wa Sinodi litakuwa ni kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji na uinjilishaji kwa watu mahalia. Kuangalia uharibifu wa mazingira na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ikumbukwe kwamba, rushwa na ufisadi wa mali ya umma ni saratani inayokwamisha mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu, kiasi hata cha kuendelea kuwatumbukiza watu katika janga la umaskini wa hali na kipato. Hija hii, ina changamoto zake, lakini, Baba Mtakatifu anataka kuzikabili uso kwa uso bila kupindisha maneno! Maisha ya wananchi wa Amazzonia yako hatarini sana kutokana na uharibifu wa mazingira. Hii ni Jamii inayotegemea sana sekta ya uvuvi, uwindaji na misitu kwa ajili ya kujipatia mahitaji yake msingi, lakini mambo yote haya kwa sasa yako hatarini! Ratiba elekezi inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu anatarajiwa kukutana na wananchi wa Amazzonia Ijumaa, tarehe 19 Januari 2018. Atakutana na kuzungumza na watoto wa Utoto Mtakatifu na viongozi mahalia. Baba Mtakatifu anatarajiwa kuwaachia ujumbe wa matashi mema, mshikamano na matumaini katika mapambano na hali yao ya maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.