2018-01-12 11:02:00

Papa Francisko: Imani na Ujasiri ni chimbuko la Sala ya Kikristo!


Sala ya Kikristo inapaswa kukubujika kutoka katika msingi wa imani kwa Kristo Yesu, inayompatia mwamini ari, nguvu na ujasiri wa kusonga mbele licha ya matatizo na changamoto za maisha. Huu ndio ambao umekuwa ni msingi wa maisha na utume wa watakatifu wengi ndani ya Kanisa. Imani thabiti inawawezesha waamini kupata neema na baraka kutoka kwa Kristo Yesu kama inavyoshuhudiwa kwenye Maandiko Matakatifu pale Yesu alipomponya na kumtakasa mgonjwa wa Ukoma; anaposamehe dhambi na kumponya wenye ugonjwa wa kupooza kule Kapernaumu.

Hawa ni watu waliojibidisha sana kwa kusukumwa na imani thabiti kwa Kristo Yesu. Mgonjwa wa ukoma, alitumpia Yesu changamoto akimwambia, ikiwa kama alitaka angeweza kumtakasa! Na Yesu, mara moja anamtakasa na kumponya ugonjwa wa Ukoma. Katika matukio haya ya Injili, Mama Kanisa anapenda kuwafundisha watoto wake kwamba, ikiwa kama wanaomba kwa imani kweli wataweza kukirimiwa. Miujiza yote hii inapata chimbuko lake kutoka katika imani na kumwilishwa katika ujasiri sanjari na kushuhudia kwa ari na moyo mkuu wa kuthubu kuomba kama alivyofanya mgonjwa wa Ukoma au wale watu waliokuwa wamembeba mgonjwa mwenye kupooza, walipoamua kutoboa dari pale alipokuwapo Yesu naye akaiona imani yao! Huu ndio ushuhuda wa sala inayomwilishwa katika imani tendaji!

Haya yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 12 Januari 2018 wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko hapa mjini Vatican. Hii ni changamoyo kwa waamini kujifunza kusali vyema na wala si kupayuka payuka au kusali kama Kasuku. Katika shida na mahangaiko ya ndani, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu zawadi ya imani, ili aweze kuwasaidia kupambana na hali pamoja na mazingira yao. Hii ndiyo imani inayoshuhudiwa na mgonjwa mwenye kupooza. Wanaonesha na kushuhudia ari na moyo mkuu inayowawezesha hata kumkaribia Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anawataka waamini kujenga utamaduni wa uvumilivu, ujasiri pamoja na kukesha katika misingi ya imani mambo msingi yanayofumbatwa katika ujasiri.

Baba Mtakatifu anaendelea kukaza kwamba, Mtakatifu Monica, Mama yake Mtakatifu Agostino, Askofu na mwalimu wa Kanisa, aliteseka na kulia sana kwa ajili ya toba na wongofu wa mtoto wake Agostino, ambaye baadaye, alibahatika kuongoka. Huu ni ushuhuda wa ari, ujasiri na moyo mkuu uliooneshwa na watakatifu, kiasi hata cha kumchangamotisha Kristo Yesu. Ikumbukwe kwamba, Sala ya Kikristo inapata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu. Abrahamu, Baba wa imani, aliamini kwa thabiti, hata akiwa na umri wa miaka mia moja, akabahatika kupata mtoto. Baba Mtakatifu anakaza kusema, imani inapaswa kumwilishwa katika matendo. Sala ya Kikristo inapata chimbuko lake katika imani na ujasiri wa kuthubutu kutenda kwa moyo mkuu! Sala inayokosa ujasiri, hiyo anasema Baba Mtakatifu ina mapungufu makubwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.