Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

Maaskofu: Imani inatuwajibisha kuwapokea wakimbizi na wahamiaji!

Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa linasema, linasukumwa na imani kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kadiri ya uwezo wake. - AP

12/01/2018 15:49

Askofu mkuu Georges Paul Pontier, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa anasema, familia ya Mungu nchini humo itahukumiwa na kizazi kijacho ikiwa kama kweli imetumia kwa kikamilifu changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji katika mchakato wa mageuzi makubwa nchini humo! Imani yao kwa Kikristo Yesu na Kanisa lake na mshikamano wa kidugu unawawajibisha kuwaonjesha ukarimu wageni na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi nchini Ufaransa.

Askofu mkuu Pontier ameyasema haya hivi karibuni kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani inayoadhimishwa na Mama Kanisa, tarehe 14 Januari 2018. Si rahisi sana kwa Ufaransa kuweza kuwapokea na kuwakirimia wakimbizi na wahamiaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia, lakini wanaweza kuboresha zaidi mchakato wa kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha kikamilifu katika maisha ya wananchi wa Ufaransa kama anavyosisitiza Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani.

Askofu mkuu Georges Paul Pontier anasikitika kuona kwamba, Ufaransa inajitahidi kila inavyoweza kufunga malango ya matumaini kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa nchini humo. Maaskofu Katoliki Ufaransa wanasema, uwepo wa wakimbizi na wahamiaji ni changamoto pevu ya kuangalia msingi wa wongofu wa kidugu. Kanisa nchini Ufaransa ni shuhuda wa upendo, ukarimu, umoja na mshikamano wa kidugu ambao umetekelezwa katika maisha na utume wake kama kielelezo cha imani tendaji! Ni matumaini ya Askofu mkuu Pontier kwamba, Serikali na Jumuiya za Kiraia zitajikita katika mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kuangalia ni kwa jinsi gani huduma kwa  wakimbizi na wahamiaji inaweza kuboreshwa zaidi kwa serikali kuhakikisha kwamba, inashiriki kikamilifu katika mchakato wa kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

12/01/2018 15:49