2018-01-11 16:17:00

Jubilei ya Miaka 50 ya Jimbo Katoliki Nakuru, Kenya


Askofu Maurice Muhatia Makumba wa Jimbo Katoliki la Nakuru, nchini Kenya anasema, familia ya Mungu Jimboni mwake imejiandaa kikamilifu kiroho, kimwili kwa kujiwekea sera na mikakati ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jimbo Katoliki la Nakuru. Kilele cha maadhimisho haya ni Jumamosi, tarehe 13 Januari 2018. Kwa muda wa mwaka mzima, waamini wamefunga, wamesali, wametafakari na hatimaye, sasa wanataka kumshukuru Mungu kwa zawadi ya imani ambayo wameikuza, wameilinda na kuirithisha kwa wengine kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao.

Ikumbukwe kwamba, imani ni fadhila ya kimungu ambayo kwayo waamini wanasadiki katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kwa imani, mwamini hujitoa nafsi yake yote kwa Mwenyezi Mungu, ili kutafuta, kujua na hatimaye, aweze kutimiza mapenzi ya Mungu katika maisha yake. Kanisa linafundisha kwamba, mwenye haki ataishi kwa imani na kwamba, imani hai hutenda kazi kwa upendo. Imani bila matendo hiyo imekufa! Lakini, mwamini anaunganishwa kikamili na Kristo Yesu kwa njia ya imani, matumaini na mapendo! Imani inapaswa kumwilishwa katika matendo na hata ikibidi kumfuasa Kristo kwa njia ya Msalaba. Huduma na ushuhuda wa imani ni mambo msingi sana katika mchakato mzima wa wokovu!

Askofu Maurice Muhatia Makumba anawashukuru wamissionari wa Shirika la Mtakatifu Patrick, Wacomboni na wale wa Shirika la Roho Mtakatifu. Hawa ndio waliojisadaka katika maisha na utume wao, kiasi hata cha kuweka msingi wa Jimbo Katoliki la Nakuru na huo ukawa ni mwanzo wa kupandikiza mbegu ya imani, ambayo katika kipindi cha miaka 50 imeendelea kukua na kukomaa. Hii ni changamoto kubwa kwa familia ya Mungu Jimboni Nakuru, kuendelea kusimamia tunu msingi za maisha ya Kikristo, kiutu na kijamii kama kielelezo cha imani tendaji. Jimbo Katoliki Nakuru lilianzishwa tarehe 11 Januari 1968, baada ya kutenganishwa kutoka katika Jimbo la Eldoret, Kisumu na Jimbo kuu la Nairobi. Askofu Denis Newman, akawa ni Askofu wa kwanza wa Jimbo hili jipya hadi tarehe 30 Agosti 1971 na kumkabidhi Askofu mkuu Raphael Ndingi Mwana’anzeki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.