Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

CEI: Msijitafutie umaarufu wa kisiasa kwa kuwanyanyasa wahamiaji!

CEI: wanasiasa msijitafutie umaarufu wa kisiasa na kura na kusahau mateso na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha bora zaidi. - EPA

11/01/2018 16:53

Mafundisho Jamii ya Kanisa kuhusu masuala ya kisiasa yanakazia: ukweli, uhuru na haki na kwamba, mtu nafsi ndiye msingi na lengo la maisha ya kisiasa yanayopaswa pia kuzingatia kanuni msingi za maadili na utu wema; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi za binadamu; kwa kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano kati ya watu badala ya kupandikiza ndago za chuki, ubaguzi na utengano. Demokrasia ya kweli ni tunda linaloambata: utu na heshima ya binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Askofu Nunzio Galantino, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, akizungumzia kuhusu maadhimisho ya Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji Duniani 2018 inayoadhimishwa na Mama Kanisa hapo tarehe 14 Januari 2018 anasema, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji nchini Italia, haliwezi kamwe kutumiwa na wanasiasa kujitafutia umaarufu wa kisiasa na kama chombo cha kuombea kura katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Machi, 2018 nchini Italia. Jamii inahitaji wanasiasa waliokomaa katika maamuzi yao; wanasiasa wakweli na waaminifu watakaojisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wengi wa Italia.

Kanisa katika maisha na utume wake, daima limetoa kipaumbele cha pekee kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa mintarafu mwanga wa Maandiko Matakatifu. Huduma kwa wakimbizi na wahamiaji ni sehemu muhimu sana ya matendo ya huruma kama yanavyobainishwa kwenye Injili. Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, litaadhimisha Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji, tarehe 14 Januari 2018 huko Jimboni Chieti kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Askofu mkuu Bruno Forte kwa kuongozwa na changamoto zinazotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Wakimbizi na Wahamiaji kwa Mwaka 2018.

Baba Mtakatifu anakazia kwa namna ya pekee: Kuwapokea, Kuwalinda, Kuwaendeleza na Kuwahusisha! Baraza la Maaskofu Katoliki Italia linawahamasisha waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha upendo na ukarimu kwa wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta fursa mbali mbali nchini Italia. Jumuiya za Kikristo zinahamasishwa kuwa ni shuhuda wa imani tendaji kwa maneno na vitendo! Takwimu zinaonesha kwamba, Italia inatoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji milioni 5 kati yao kuna Wakatoliki milioni 1; wanaopaswa kujisikia nyumbani wanapokutana na waamini wenzao. Maadhimisho haya yawasaidie waamini kutambua kwamba, wote wanaalikwa kuchuchumilia na kuambata wokovu ulioletwa na Kristo Yesu, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

11/01/2018 16:53