Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Mambo msingi, taratibu, sheria na kanuni za kuwatangaza watakatifu!

Mambo msingi katika mchakato wa kuwatangaza waamini kuwa watakatifu: karama, kifodini na miujiza iliyotendwa kielelezo cha neema ya Mungu. - ANSA

10/01/2018 15:05

Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, katika hotuba yake elekezi kwa ajili ya semina maalum, kuhusu mchakato wa kuwatangaza wenyeheri, iliyofanyika kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, mjini Roma, Jumatatu, tarehe 8 Januari 2018 amesema, Kanisa linaendelea kujipyaisha kutokana na maisha na utakatifu wa watoto wake wanaotangazwa kila wakati. Hawa ni pamoja na Mama Theresa wa Calcutta, Mtakatifu Yohane Paulo II, Mwenyeheri Oscar Arnulfo Romero na wengine wengi ambao wameshuhudia tunu msingi za maisha ya Kiinjili na kulipamba Kanisa kwa harufu nzuri ya utakatifu wao!

Amesema, kuna sheria, kanuni na taratibu ambazo Mama Kanisa anazifuata katika mchakato mzima wa kuwatangaza waamini kuwa: watumishi wa Mungu, wenyeheri na hatimaye, watakatifu. Mwaka 2017 Mama Kanisa ameadhimisha Ibada za Misa Takatifu 19 kwa ajili ya kuwatangaza watumishi wa Mungu kuwa wenyeheri, Ibada ambazo zimeendeshwa na Kardinali Angelo Amato kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, ambaye pia ameadhimisha Ibada ya Misa na kuwatangaza Watoto wawili wa Fatima yaani: Francis na Yacinta Marto kuwa watakatifu kama sehemu ya kumbu kumbu ya Jubilei ya Miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima, huko Ureno. Tarehe 15 Oktoba, 2017, Baba Mtakatifu amewatangaza wenyeheri Andrea de Soveral na Ambrose Francisco Ferro, Mapadre wa Jimbo na Matteo Moreira, mwamini mlei pamoja na mashuhuda wa imani 27 walioyamimina maisha yao kunako mwaka 1645 kuwa watakatifu.

Waamini waliotangaza kuwa watumishi wa Mungu, wenyeheri na watakatifu ni watu kutoka katika makabila, lugha na jamaa, walioishi na kushuhudia tunu msingi za maisha ya Kikristo na Kiinjili, kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, kiasi hata cha kuwa tayari kuyamimina maisha yao. Hii ni huduma nyeti na shirikishi inayohitaji umoja na mshikamano kati ya Baraza la Kipapa, “Wajenga hoja” wataalam wa historia, wanataalimungu, wanasheria wa Kanisa, Madaktari na wataalam wa Sayansi jamii. Mambo msingi yanayozingatiwa katika kuandaa nyaraka za kuwatangaza waamini katika hatua mbali mbali ni: karama, kifodini na miujiza waliyotenda.

Katika kipindi cha Mwaka 2017 Baba Mtakatifu Francisko amechapisha “Barua Binafsi kuhusu Sadaka ya Maisha” na Baraza la Kipapa likachapisha pia “Mwongozo wa masalia ya watakatifu ndani ya Kanisa: uhakika na utunzaji wake”. Mwongozo unakazia ufahamu wa masalia ya watakatifu mintarafu Taalimungu, Liturujia na umuhimu wake katika sera na mikakati ya kichungaji. Miili ya watakatifu inaheshimiwa na kuthaminiwa na Mama Kanisa kwa sababu ni “Mahekalu ya Roho Mtakatifu” na chemchemi ya utakatifu wao. Hii ndiyo miili itakayofufuliwa siku ya mwisho! Masalia ni ushuhuda wa utakatifu na Kisakramenti cha neema. Kikanisa cha Masalia ya Watakatifu katika nyumba za kitawa ni kiini cha maisha ya sala. Ndiyo maana, Makanisa mapya yanatabarukiwa kwa kuwekewa pia masalia ya watakatifu na mashuhuda wa imani. Wakati wa maadhimisho ya Liturujia ya Kuwatangaza watumishi wa Mungu kuwa wenyeheri au watakatifu, masalia yao hupelekwa Altareni kwa heshima kuu, kama ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili au sadaka ya maisha yao kama wafiadini. 

Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu limechapisha Mwongozo ambao umegawanyika katika sehemu kuu tatu: Taalimungu, Historia na Sheria. Hivi karibuni, Baraza pia limechapisha Kitabu kuhusu watakatifu na wenyeheri vijana, chachu ya utakatifu kwa vijana wa kizazi kipya na mchango makini katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu vijana itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, 2018 hapa Vatican kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito” bila kusahau Kitabu cha Papa Mstaafu Benedikto XVI “Opus Magnum” ambacho kwa sasa kimefikia Toleo la VI.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

10/01/2018 15:05