2018-01-10 07:22:00

Kardinali Angelo Amato: Masalia ya watakatifu na Sadaka ya Maisha


Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu anasema, kuna njia mbali mbali ambazo waamini wanaweza kushuhudia utakatifu wa maisha yao: kwa kumwaga damu yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake; kwa njia ya huduma ya upendo; ushuhuda wa karama za waamini zinazomwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa. Katika kipindi cha Mwaka 2017 Baba Mtakatifu Francisko amechapisha “Barua Binafsi kuhusu Sadaka ya Maisha” na Baraza la Kipapa likachapisha pia “Mwongozo wa masalia ya watakatifu ndani ya Kanisa: uhakika na utunzaji wake” “Le Relique nella Chiesa: autenticità e conservazione”. Baba Mtakatifu Francisko kwa barua yake binafsi, “Motu Proprio” “Maiorem hac dilectionem” yaani “Kuhusu sadaka ya maisha” amefungua njia ya kutangazwa wenyeheri waamini ambao hali wakisukumwa na upendo, wamesadaka maisha yao kwa ajili ya jirani zao kwa kukubali na kupokea kifo kabla ya wakati kama njia ya kumfuasa Kristo Yesu kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu. (Rej. 1Yoh. 3:16).

Kama inavyoeleweka kadiri ya Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa Katoliki kwamba, mwamini anaweza kutangazwa kuwa Mwenyeheri kwa njia ya kifo dini, kielelezo cha pekee katika kumfuasa Kristo, lakini, ikumbukwe kwamba, kielelezo cha juu kabisa cha ushuhuda kwa Kristo na Kanisa lake ni upendo kwa Mungu na jirani. Kifodini kadiri ya ufahamu wa Kanisa ni kupokea kwa hiyari kifo kama kielelezo cha upendo kwa Kristo! Ni kupokea kifo kutokana na chuki za kiimani, au fadhila nyinginezo za Kikristo. Kifodini ni kielelezo cha unyenyekevu kwa mwamini anayesamehe kama njia ya kumuiga Kristo Yesu, ambaye alipokuwa pale juu Msalabani aliwaombea watesi wake msamaha kutoka kwa Baba yake wa mbinguni!

Njia ya pili inayomwezesha mwamini kutangazwa kuwa ni Mwenyeheri ni katika mchakato wa kumwilisha fadhila za kishujaa zinazotekelezwa kwa haraka, bila kusita na kwa moyo mkunjufu, kiasi cha kuonekana kuwa ni fadhila kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si tu nguvu za kibinadamu. Huu ni mwelekeo unaomwezesha mwamini kufikiri na kutenda mintarafu mwanga wa Injili. Fadhila zinazozungumziwa hapa ni zile fadhila tatu za Kimungu yaani: Imani, Matumaini na Upendo bila kusahau fadhila kuu nne yaani: Busara, Haki, Nguvu na Kiasi. Fadhila zote hizi zinafumbatwa kwa namna ya pekee kabisa katika Mashauri ya Kiinjili, au Nadhiri kama zinavyojulikana na wengi: Ufukara, Utii, Usafi kamili na Unyenyekevu.

Njia ya tatu inayomwezesha mwamini kutangazwa kuwa Mwenyeheri, ambayo waamini wengi hawaifahamu sana, lakini imefafanuliwa katika Sheria, Kanuni na Tararibu za Kanisa katika Sheria za Mwaka 1917 inayojulikana kama kutangazwa Mwenyeheri kwa kutumia kanuni ya “Equipollente” ambayo kimsingi inatumika kwa nadra sana katika Kanisa kwa ajili ya kesi maalum. Hizi ni njia ambazo Mama Kanisa anazitumia kwa ajili ya kuwatangaza waamini wake kuwa wenyeheri na watakatifu, lakini kadiri ya historia inavyozidi kusonga mbele, njia hizi zinazonekana kana kwamba, zinawatenga baadhi ya waamini ambao wamekuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa kwa njia ya ushuhuda wa upendo wenye mvuto na mashiko! Yesu mwenyewe anasema, hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake. (Rej. Yoh. 15:13).

Njia ya nne inayotolewa sasa na Baba Mtakatifu Francisko ni sadaka ya maisha ambayo pengine inafumbata baadhi ya mambo msingi yaliyokwisha kufafanuliwa katika hatua tatu zilizotangulia, inataka kutoa kipaumbele cha pekee kwa ushuhuda wa Kikristo unaofumbatwa katika upendo, kama kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ushuhuda kwa Kristo na Kanisa lake; ushuhuda unaopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya mwamini kama njia ya kutafuta ukamilifu wa maisha na hatimaye, utakatifu. Sadaka ya maisha inafumbwata kwa namna ya pekee katika fadhila ya : Imani, Matumaini, Busara pamoja na nguvu.

Kardinali Angelo Amato anasema, Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, mwaka 2017 limechapisha “Mwongozo wa masalia ya watakatifu ndani ya Kanisa: uhakika na utunzaji wake” “Le Relique nella Chiesa: autenticità e conservazione”. Kanisa linatambua na kuheshimu masalia ya watakatifu kwani siku moja miili yao itafufuliwa kutoka kwa wafu! Hapa duniani, miili yao imekuwa ni Hekalu la Roho Mtakatifu na chombo cha utakatifu wao. Mwongozo huu unatoa vigezo msingi vya kutambua masalia ya watakatifu na wenyeheri ili kuweza kuhifadhiwa mahali salama.

Masalia hayawezi kuheshimiwa na waamini bila kuwa na kibali cha kiongozi wa Kanisa anayethibitisha ukweli wake kadiri ya sheria, kanuni na taratibu za Kanisa Katoliki sanjari na maelekezo ya kutembeza masalio ya watakatifu. Jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, masalia ya watakatifu yanahifadhiwa mahali pa usalama na kuheshimiwa kwa ibada, ili kuepuka uwezekano wa baadhi ya watu kutumia masalia haya kwa imani potofu na mambo ya ushirikina. Heshima ya masalia ni kwa ajili ya wenyeheri na watakatifu peke yao ambao tayari wametambuliwa na kutangazwa na Mama Kanisa kuwa ni Wenyeheri au Watakatifu.

Kardinali Angelo Amato anasema, ni dhamana ya Maaskofu mahalia kuhakikisha kwamba, wanatekeleza  mwongozo huu kikamilifu na kamwe yasitumike kwa ajili ya biashara au kuhifadhiwa mahali ambapo hapastahili. Mwongozo huu ni tafakari ya miaka mingi ndani ya Kanisa kwa kutambua kwamba, masalia ya watakatifu na wenyeheri yamekuwa yakiheshimiwa sana na waamini, kwani miili yao hapa duniani imekuwa ni Hekalu la Roho Mtakatifu na chombo cha utakatifu wao. Masalia haya yanaweza kuwa ni mwili mzima wa Mtakatifu au Mwenyeheri “Relique Insigni” na masalia mengine yanajulikana kama “Relique non Insigni” haya ni masalia ya vitu ambavyo vimetumiwa na watakatifu pamoja na wenyeheri. Yote haya yanapaswa kulindwa na kutunzwa vyema.

Mwongozo huu ni muhimu sana kwa Maaskofu na viongozi wa Kanisa katika ujumla wake kama sehemu ya mchakato wa kutambua uhakika, jinsi ya kuyasafirisha pamoja na kupata vibali kutoka kwa viongozi wa Kanisa na Serikali pale inapobidi bila kusahau kwamba, Baraza la Kipapa la Kuwatangaza Waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu lina dhamana na wajibu kwa masalia ya watakatifu na wenyeheri kwa niaba ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.