Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Maisha Ya Kanisa Afrika

Askofu Salutaris Libena: waamini kuzeni moyo wa Ibada na uchaji!

Mama Kanisa anapenda kuwahimiza watoto wake kusoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku!

10/01/2018 14:44

Askofu Salutaris Melchior Libena wa Jimbo Katoliki Ifakara, Tanzania katika mahojiano maalum na Vatican News anasema, Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican walikazia sana umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha ya waamini, ili waweze kupata uzima wa milele. Waamini wanapaswa kulisoma, kulitafakari, kulimwilisha na kulirithisha kwa watoto na vijana wa kizazi kipya, ili kweli liweze kuwa dira na mwongozo wa maisha yao ya kila siku.

Neno la Mungu ni Kazi ya Roho Mtakatifu na Mapokeo ya Mama Kanisa na kwamba, kuna uhusiano hai baina ya Mapokeo na Maandiko Matakatifu matunda ya uvuvio wa Roho Mtakatifu. Hizi ni kanuni kuu za maisha ya kiimani, chakula cha roho na chemchemi safi ya daima ya maisha ya kiroho kwa watoto wa Kanisa. Ndiyo maana Neno la Mungu ni hai, tena lina nguvu. Ikumbukwe kwamba, kutojua Maandiko Matakatifu ni kutomjua Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Mababa wa Sinodi ya Maaskofu wa Afrika walihimiza sala inayobubujika kutoka katika Maandiko Matakatifu na mahubiri yaliyoandaliwa vyema.

Mababa wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA katika mbinu mkakati wake wa shughuli za kichungaji wanaielekeza familia ya Mungu kuhakikisha kwamba, inajifunza kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha yake, kama kielelezo cha imani tendaji. Neno la Mungu liwe pia ni kitovu cha maisha ya kifamilia. Sanjari na Neno la Mungu, waamini wajifunze pia utamaduni wa kusali Sala za Kanisa kama njia ya kuyatakatifuza malimwengu. Hii ni sala kwa waamini wote na wala si upendeleo kwa Wakleri na Watawa. Askofu Askofu Salutaris Melchior Libena wa Jimbo Katoliki Ifakara, anawahimiza waamini kujenga utamaduni wa kufanya Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, ili kupata nafasi ya ukimya na sala mbele ya Ekaristi Takatifu. Hii ni changamoto kwa familia kurithisha na kukuza moyo wa sala na ibada miongoni mwa watoto wao kama wanavyokazia Mababa wa Kanisa, ili kuweza kupambana na changamoto za maisha ya kiroho na kimwili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

10/01/2018 14:44