Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Mahubiri

Papa Francisko: Ukatili na unyanyasaji ni madhara ya dhambi ya asili

Papa Francisko anasema dhuluma, nyanyaso na ukatili dhidi ya jirani ni matokeo ya dhambi ya asili. - REUTERS

09/01/2018 10:30

Dharau, nyanyaso na dhuluma dhidi ya maskini na wanyonge ni kazi ya shetani kama inavyofafanuliwa na vifungu mbali mbali ya Maandiko Matakatifu, kwani shetani hana hata chembe ya huruma kwa binadamu kwani anataka kumwangamiza. Kitabu cha kwanza cha Nabii Samuel kinaelezea kwa kina na mapana dhuluma na nyanyaso alizofanyiwa Hana aliyekuwa amefungwa tumbo na Mwenyezi Mungu. Penina aliyebahatika kupata watoto badala ya kumfariji mke mwenza akawa anamnyanyasa na kumwona si mali kitu, kwa kumchokoza na kumsikitisha sana ili kumtonesha kidonda cha ugumba wake.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumatatu, tarehe 8 Januari 2018. Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, hali kama hii ilijitokeza pia kwa wanawake wa Abram yaani Hajiri na Sarai pia kuna wanawake katika Maandiko Matakatifu wanaooneshwa kuwadharau na kuwanyanyasa wanaume wao, chanzo kikuu ni wivu usiokuwa na mashiko unaofanywa na shetani.

Ukatili kama huu wanafanyiwa hata watoto hasa wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, wananyanyaswa kiasi cha kugeuzwa kuwa kama ni mpira wa kupigwa danadana! Hali kama hii inajionesha hata katika mazingira ya shule, kuna wanafunzi wanaowanyanyasa wenzao kutokana na maumbo yao, uwezo wao darasani au ulemavu walionao! Nyanyaso, dhuluma na uonevu unajionesha katika maisha ya mwanadamu ni kazi ya shetani, hata kama wataalam mbali mbali wanaweza kutoa maelezo tofauti! Haya ni madhara ya dhambi asili, yanayopelekea mtu kutaka kumfuta jirani katika kutoka katika uso wa dunia, kwani shetani kamwe hana huruma wala upendo. Pale mwamini anapojikuta anasukumwa kutenda mema, atambue kwamba, hii ni kazi ya Roho Mtakatifu, lakini pale anapotenda kinyume chake, afahamu fika kwamba, hapo shetani yuko kazini “anafanya mambo yake”. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kumwomba Mwenyezi Mungu awakirimie neema ya kuwa na huruma kwa maskini na wanyonge, kwani Mwenyezi Mungu ni dira na mwanga wa maisha ya waja wake, anayewasaidia kutembea katika mwanga kwa kutenda mema!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

09/01/2018 10:30