Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Mahubiri

Papa anawataka viongozi wa Kanisa kuwa karibu na Mungu na watu wake!

Papa Francisko anawataka viongozi wa Kanisa kuwa karibu na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala, tafakari, ushuhuda wa maisha sanjari na kuwa karibu na watu wao kwa njia ya huruma na mapendo. - AP

09/01/2018 11:34

Kristo Yesu katika maisha na utume wake alidhihirisha uwezo wake wa kuganga na kuponya, kufundisha kwa mamlaka na kuwafariji wale wote waliokuwa wamekamatwa na pepo wachafu! Kwa ufupi: aliguswa na mahangaiko ya watu, akawaonea huruma kwa uwepo wake wa karibu na kwamba, matendo yake yalishuhudia kwa dhati kile alichokuwa anakisema na kuwafundisha watu! Kamwe hakuwa na maisha ya “undumilakuwili”. Hivi ndivyo Mwinjili Marko anavyoelezea maisha ya Kristo Yesu kwamba ni kiongozi aliyefundisha kama mtu mwenye mamlaka, zawadi mpya kutoka kwa Baba yake wa mbinguni, mafundisho yaliyokuwa yanamwilishwa katika maisha na matendo yake ya kila siku!

Wakuu wa makuhani na waandishi wa watu, walifundisha bila kutenda, ndiyo maana, watu wengi waliguswa sana na mtindo wa mafundisho na maisha ya Kristo Yesu, ingawa alifundisha kama mtu mwenye mamlaka, lakini daima alijitahidi kuwa karibu na watu! Alitambua na kuguswa na matatizo, mahangaiko, dhambi na matumaini yao, kiasi cha kuwapokea, kuwaganga na kuwaponya kutokana na uwepo wake wa karibu!

Huu ni ufafanuzi uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake, Jumanne, tarehe 9 Januari 2018 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican. Wakuu wa makuhani na waandishi wa watu walikuwa wamepoteza dira na mwelekeo, kiasi hata cha kushindwa kuwa karibu na watu! Hii ni kwa sababu, wao pia walikuwa mbali na Mwenyezi Mungu na maisha yao, yakashindwa kuwa ni ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa watu! Ndiyo maana hata Kristo Yesu aliwaambia wafuasi wake, fuateni yale wanayowaambia lakini msitende kile wanachotenda wao kwani waligeuka kuwa ni makaburi yaliyopakwa chokaa na kung’aa kwa nje, lakini ndani kulikuwa na mifupa ya maiti!

Hawa ni watu waliokuwa na mafundisho mazuri, lakini yalisigana sana na maisha yao. Hii ndiyo hatma ya kiongozi wa Kanisa asiyejishikamanisha na Mwenyezi Mungu kwa njia ya sala inayomwilishwa katika huruma na ukaribu kwa watu wa Mungu kama ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Baba Mtakatifu anakaza kusema, Somo la kwanza linamwelezea Hana aliyekuwa akijisemea moyoni mwake, kiasi cha kuonekana kuwa mlevi, Mzee Eli, kuhani akamkaripia kwa kudhani kwamba, ni mwanamke mlevi! Lakini Hana akamsimulia mateso na mahangaiko ya moyo wake, yaliyokuwa ni chimbuko la sala yake mbele ya Mwenyezi Mungu.

Mzee Eli akapata ujasiri na kumkaribia na hatimaye, kumwambia “Enenda kwa amani; na Mungu wa Israeli akujalie haja yako uliyomwomba”. Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, akamjalia Hana kupata mtoto aliyemwita Samueli, maana yake “Kwa kuwa nimemwomba kwa Bwana”. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutokata tamaa katika maisha, bali wawe na matumaini katika huruma na upendo wa Mungu. Viongozi wa Kanisa wajenge utamaduni wa kuwa karibu na waamkini, kuwasikiliza kwa makini na kujibu kilio na mahangaiko yao ya ndani, daima wakijitahidi kumfuasa Kristo aliyefundisha kama mtu mwenye mamlaka, akawakaribia watu ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu unaoganga na kuponya. Viongozi wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa kile wanachofundisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

09/01/2018 11:34